
Dar es Salaam. Mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere jana Ijumaa Agosti 16, 2019 alitembelewa na wanawake walioshiriki harakati za kupigania uhuru wa Kenya nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa wanawake hao uliongozwa na mwanaharakati, Muthoni Likimani (94) na mwenyeji wao, Dan Kazungu ambaye ni balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, kupokewa na Mama Maria, Balozi Getrude Mongela; Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu.
Walisema lengo la kuja Tanzania ni kumjulia hali Mama Maria kama ilivyo ada kwa viongozi kutembeleana.
Wakati Mama Maria akiwakaribisha wageni hao, Makinda amesema ni jambo la kushukuru Mungu kwa wanawake kukutana pamoja.
“Huu ni undugu ndani ya damu, umri wao ni mkubwa lakini wamepanda ndege na kuja nchini,” alisema Makinda.
Naye Ummy amesema, “Hii ndio asili ya jamii zetu ukiwa una wageni waalike na wenzako. Nimesisimka sana, nakiri wizara yetu haijafanya kuhusu wazee, tunaahidi kila mwaka kutenga siku na kukaa na wazee hasa wanawake walioleta ukombozi wa Taifa.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Likimani aliwataka wanawake wa mataifa hayo kusimama imara na kukataa masuala ya fujo kwenye jamii.
“Tukatae fujo kwa sababu ikitokea kina baba wanakimbia lakini nyie mnabaki na hamuwezi kukimbia. Simameni imara na msipende kutukanana,” amesema Likimani.
No comments:
Post a Comment