Thursday, August 15, 2019

Rais Magufuli, Ramaphosa watangazia fursa za uwekezaji



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewakaribisha wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja kuwekeza nchini humo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo sekta za afya, hoteli, utalii wa fukwe na uchakataji wa madini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 15,2019 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye aliwasili nchini jana Jumatano kwa ziara ya siku mbili kisha kushiriki mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema Tanzania inatenga kila mwaka zaidi ya Sh270 bilioni kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba na asilimia 98 ya fedha hizo zinakwenda kununua nje ya nchi. Hivyo, amewakaribisha kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa sababu ni fursa kubwa.
Pia, amewakaribisha kuwekeza kwenye sekta ya utalii hasa kwa kujenga hoteli na kuendeleza utalii wa fukwe wa kilomita 1,400 kuanzia Moa mpaka Msimbati. Amesema eneo hilo linahitaji wawekezaji ili kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.
“Kupitia Rais Ramaphosa, nimewaalika wafanyabiashara kuja kujenga viwanda nchini ikiwemo viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vya madawa na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye madini,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amemhakikishia Rais Ramaphosa kwamba Tanzania itanunua vifaa ambavyo vinatengenezwa Afrika Kusini badala ya kwenda kununua nchi za mbali.

Amesema tayari wameanza kutekeleza hilo kwa kununua pikipiki ambazo zitatumika kwenye mkutano wa SADC.
Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amewakaribisha wafanyabiashara kwenda kuwekeza Afrika Kusini.
Amesema ni muhimu kwa nchi hizo kutumia fursa zinazojitokeza kwa manufaa ya wananchi wao.
Pia, Ramaphosa amesema nchi yake iko tayari kutumia fursa ya kujifunza lugha ya Kiswahili licha ya kuwepo kwa lugha mbalimbali zinazozungumzwa nchini mwake.
Amesema Afrika Kusini itatoa ushirikiano katika kipindi chote ambacho Tanzania itakuwa mwenyekiti wa SADC.
“Tunatambua Rais Magufuli anakuwa mwenyekiti wa SADC, nimemhakikishia kwamba tutampatia ushirikiano wote katika kudumisha amani, biashara na ushirikiano baina yetu,” amesema kiongozi huyo wa Afrika Kusini.

No comments:

Post a Comment