
Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), Rais John Magufuli amehamishia dhamira yake ya kutaka kuwapo kwa kasi ya maendeleo nchini katika jumuiya hiyo.
Katika hotuba yake ya kwanza mara baada ya kukabidhiwa wadhifa huo jana, Rais Magufuli alianza kwa kuishukia Sekretarieti ya Jumuiya hiyo akisema imeshindwa kuzishauri nchi wanachama namna ya kuondokana na mkwamo wa kiuchumi.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza utendaji kazi usiokuwa wa mazoea, kujituma ili kuwasaidia wananchi hasa wanyonge kujikwamua kuichumi.
“Sisi siyo maskini,” alisema Rais Magufuli jana katika hotuba yake baada ya kukabidhiwa rasmi wadhifa huo na mtangulizi wake, Rais Hage Geingob wa Namibia.
Huku akitumia takwimu, mwenyekiti huyo mpya alitoa takwimu za miaka 10 kuonyesha namna gani ukuaji wa kiuchumi ulivyo wa kusuasua huku sekretarieti ikishindwa kutoa majibu au hata kuzishauri nchi wanachama namna ya kuvuka vikwazo vya kiuchumi.
Alisema takwimu za ukuaji wa uchumi kwa nchi za Sadc haujawahi kufika asilimia tano na kwamba mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2008 ambako ulikuwa kwa asilimia 5.7 na kusema sekretarieti hiyo imeonyesha upungufu katika utendaji wake.
Huku akishangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa ufunguzi uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, mwenyekiti huyo alisema; “nchi zetu siyo maskini. Tuna rasilimali zote zinazoweza kutuondoa kwenye umaskini.”
No comments:
Post a Comment