Friday, August 30, 2019

Kilichojiri ndege ya Air Tanzania kukamatwa Afrika Kusini


Dar es Salaam. Jopo ya wanasheria waliopelekwa na Tanzania kupinga amri ya kushikiliwa kwa ndege ya Air Tanzania wameiambia mahakama ya Gauteng, Afrika Kusini kwamba amri ya kushikiliwa ndege hiyo ilitolewa kimakosa.
“Tumeonyesha kwamba amri ya kuishikilia ndege ya  Air Tanzania aina ya airbus A220-300 ilitolewa kimakosa dhidi ya Serikali, kwa hiyo tumetaka iondolewe,” wakili  Ngaukaitobi aliiambia mahakama.
Wakili Roger Wakefied anayemwakilisha mkulima Hermanus Steyn amesisitiza kuwa kuna kesi ya msingi ya kujibu na ameitaka mahakama hiyo kuangalia vigezo vya madai hayo na kuvitendea haki.
Kwa mujibu wa Wakefield hatua ya kwanza ya vigezo vya kesi hiyo vimeshathibitishwa.
Ndege hiyo ilishikiliwa Agosti 23, 2019 nchini humo kutokana na mvutano wa kisheria uliodumu kwa miongo kadhaa kati ya Serikali ya Tanzania na mkulima  Hermanus Steyn.
Mali za Steyn ikiwemo kampuni ya mbegu ya Rift Valley Seed Company Limited na mali nyinginezo zilitaifishwa na Serikali ya Tanzania Januari 1982. Amekuwa akiidai Serikali Sh373 milioni.
Hata hivyo, Julai 9, 2010 Jaji mstaafu Josephat Mackanja wa mahakama kuu alimpa Steyn tuzo ya Dola za Kimarekani 36,375,672.81.
Kuna ushahidi kuwa baada ya kutolewa kwa tuzo na Mahakama hiyo kulikuwa na makubaliano kati ya pande mbili yaliyoishusha hadi kufikia Dola 30 milioni na Serikali ya Tanzania ililipa kiasi kikubwa cha deni hilo kupunguza madai hayo.
Akizungumza na gazeti la Daily News, Wakili mkuu wa Serikali, Ally Possi amesema timu ya mawakili wanane kutoka ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali watapambana kwenye kesi hiyo iliyotajwa Agosti 21, 2019  ambayo hati ya dharura iliwekwa na kampuni ya mawakili ya Werksman’s Attorneys ikitaka ndege yoyote ya ATCL ili kufanikisha malipo ya tuzo hiyo.

Thursday, August 29, 2019

Rais Magufuli abainisha changamoto za umaskini Afrika

Rais John Magufuli wa Tanzania,Ikulu ya Dar es Salaam nchini Tanzania , Samia Suluhu,mwananchi, habari mwananchi,


Dar es Salaam. Rais John Magufuli wa Tanzania amesema masalia ya fikra za kikoloni walizonazo Waafrika wengi ni miongoni mwa sababu zinazofanya Bara la Afrika kushindwa kusimamia rasilimali zake ili kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Ameyasema hayo jana Alhamisi Agosti 29,2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokuwa akihutubia kongamano la viongozi la 2019 akisema dhana ya uhuru haiwezi kutenganishwa na kujitegemea.
“Kama hujitegemei huwezi kuwa huru, kwani uhuru wako utakuwa mikononi mwa unayemtegemea.”
“Maana hasa ya kupigania uhuru ni kurejesha rasilimali zetu na hasa rasilimali zetu, lakini pia kuwa na uamuzi kamili wa namna ya kuzisimamia na kuzitumia wa kuzitumia ili kuleta ukombozi wa kiuchumi,” amesema Rais Magufuli.  
Amesema kutokana na kutoelewa dhana kamili ya uhuru, nchi za Afrika zinadhani watawala wa zamani ndiyo wenye uwezo wa kusimamia na kusaidia na kuendeleza rasilimali.
Ametaja pia sababu ya kushindwa kusimamia rasilimali na kuleta mageuzi ya kiuchumi, akisema fedha siyo msingi wa rasilimali.  
“Fedha ni matokeo ya mwisho kabisa ya matumizi ya rasilimali zetu na siyo msingi wa maendeleo. Hata hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alisema ili tuendelee tunahitaji watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora. Hakutaja pesa, alijua itakuja tu kama yale tutayatimiza,” amesema.
Ametaja pia ukosefu wa ubunifu na teknolojia ya viwanda akisema Afrika haitaweza kusimamia na kutumia rasilimali zake kiuendelevu bila kuwa na viwanda.
Mbali na viwanda, ametaja kukithiri kwa migogoro na hali tete ya siasa barani Afrika akisema inasababishwa na mabeberu wanaotaka kuendelea kutumia maliasili za Afrika kwa manufaa yao.
“Wakati sisi tunapigana wao wanakula na kamwe hawatataka tuwe na amani, kwani migogoro ndiyo mtaji wao,” amesema.
Ameendelea kutaja pia tatizo la mikataba na makubaliano yanayoingiwa na wawekezaji katika kutumia rasilimali akisema, “Na hapa nchi yetu imeliwa sana kutokana na mikataba mibovu na hasa kwenye madini.”
Kuhusu uharibifu wa mazingira, Rais Magufuli amesema unasababishwa na ukataji hovyo wa msitu kwa ajili ya nishati ya majumbani kutokana na gharama kubwa za umeme na gesi asilia.  
“Chanzo kingine ni uchafuzi wa mazingira unaofanywa na mataifa mengine yaliyoendelea na yenye viwanda vingi, lakini Afrika ndiyo inayoathirika zaidi a machafuko hayo,” amesema.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa na Serikali, Rais Magufuli amesema imetungwa sheria ya kulinda utajiri na rasilimali na maliasili ya 2017 na kupitiwa upya na kurekebisha mikataba ya uchimbaji na madini isiyo na manufaa kwa Taifa.
“Tumeweka msukumo mkubwa kwenye ujenzi wa viwanda na ukuzaji wa teknolojia ya viwanda ili mazao yanayotokana na rasilimali zetu yasindikwe kwanza kabla ya kuuzwa nje,” amesema
Alitaja pia uanzishwaji wa mradi wa bwawa la Nyerere utakaozalisha MW 2115 kwenye bonde la mto Rufiji kama njia ya kutunza mazingira, kudhibiti nidhamu za watumishi wa umma na kupamba na rushwa na ufisadi.  
Wageni maarufu waliohudhuria mkutano huo walikuwa marais wastaafu kutoka baadhi ya nchi za Afrika akiwemo Thabo Mbeki wa Afrika Kusini, Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wa Tanzania.

Wednesday, August 28, 2019

Waziri mkuu ataka ATCL kuanza safari za mauritius

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa,Shirika la Ndege la Tanzania,ATCL,

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema umefika wakati wa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kuanza safari za Mauritius ili kuvutia watalii zaidi.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Agosti 28, 2019 alipokutana na waziri mkuu wa nchi hiyo, Pravind Kumar nchini Japan wakati akiwakaribisha wafanyabiashara wa Mauritius kuwekeza Tanzania.
Taarifa iliyotolewa na ofisi ya waziri mkuu leo inaeleza kuwa wafanyabiashara hao wanaweza kuwekeza katika uzalishaji wa sukari, uvuvi na kujenga viwanda vya nyuzi za pamba na nguo.
Majaliwa amesema kuanzishwa kwa safari za moja kwa moja kwenda Mauritius kutachangia kuwahamasisha watalii kuwekeza nchini.
“Umefika wakati wa ATCL kufikiria kuhusu safari za kwenda  Mauritius ili  kuwarahisishia wanaokwenda kufanya utalii wa fukwe  katika nchi hiyo inayofanya vizuri katika sekta hiyo na kwa sababu Tanzania ina fukwe za bahari na maziwa kupitia ushirikiano huo utatuletea tija,” amesema.
Naye Pravind ameihakikishia Tanzania kuwa nchi  hiyo ipo  tayari kufanya mazungumzo na wizara na taasisi zinazohusika na uwekezaji nchini.

“Tunataka kupata taarifa za kutosha zitakazotuwezesha kuwashawishi wafanyabiashara wa nchi yangu waje kuwekeza Tanzania.” Amesema Pravind

Sunday, August 25, 2019

Sababu ya Air Tanzania kuzuiwa Afrika kusini



Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema Mahakama Kuu nchini Afrika Kusini imezuia ndege ya Air Tanzania kuondoka nchini humo  kuanzia jana Jumamosi Agosti 24, 2019 kutokana na kesi ya madai iliyofunguliwa na Hermanus Steyn.
Steyn,  raia wa Afrika Kusini anadai fidia baada ya mali zake kutaifishwa na Serikali ya Tanzania mwaka 1980.
Hayo yameelezwa leo Jumapili Agosti 25, 2019 na msemaji wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas wakati akihojiwa na Shirika la Utangazaji nchini (TBC).
Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 imeshikiliwa katika uwanja wa Oliver Tambo jijini Johannesburg baada ya kufanya safari kadhaa tangu Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) lianze kufufua ruti zake za nje ya nchi.
Katika maelezo yake Dk Abbas amesema Steyn aliridhia mali hizo kutaifishwa lakini hoja ikaja alipwe fidia kiasi gani.
“Ndege zetu zipo salama kwa maana ya ndege sita ambazo Air Tanzania kwa sasa inaziendesha isipokuwa hii moja ambayo tumetoa taarifa kuwa imezuiwa kwa ajili ya kesi.”

“Watu wanahusisha jambo hili na madeni ya zamani kwenye shirika  kati ya Air Tanzania na Shirika la ndege Afrika ya Kusini. Niseme tu kuwa hii kesi haihusiani kabisa na hilo,” amesema Dk Abbas.
Ameongeza, “Alikuwa (Steyn) na mashamba, mifugo na mali nyingi kwa hiyo Serikali kwa wakati huo ikaona ni sahihi hizi mali zitaifishwe kwa hiyo ukitaka kuchimbua mgogoro huu asili yake unatoka miaka ya 1980.”
Amesema ilipofika miaka ya 1990 walikubaliana fidia atakayolipwa, miaka ya 2000 akalipwa na kuna kiasi kilichobaki ambacho mhusika amefungua kesi akitaka amaliziwe kulipwa.
“Ukiangalia awamu zote (za uongozi) kulikuwa na makubaliano, ukiangalia hatua za kimahakama wanakubaliana lakini malipo hayakufanywa lakini yalikuja kufanyika katika awamu ya nne,” amesema Dk Abbas.
Dk Abbas amesema mdai  huyo amekwenda Afrika Kusini kwa taratibu za mahakama, akibainisha kuwa zipo nchi ambazo mtu anaruhusiwa kuiomba hukumu ya nchi nyingine itekelezwe kwenye nchi aliyopo, akisisitiza kuwa ni  taratibu za kawaida kwenye sheria.
“Sisi tunaheshimu utawala wa sheria kwa sababu ni mfumo wa kawaida. Sheria itafuata mkondo wake, ukisoma ile hukumu inaturuhusu kuipinga.”
“Nafikiri  wanasheria wetu wataichambua na wataona hatua gani za kuchukua lakini ni mfumo wa kisheria ambao Serikali tunaufuata na tunauheshimu. Tunawahakikishia Watanzania kuwa tunasimamia maslahi ya Taifa,  ndege yetu itarudi na itaendelea na shughuli zake za kawaida,” amesema Dk Abbas.
Amesema kesi ya msingi haijasikilizwa kwa sababu anayedai fidia  ametumia sheria za Afrika Kusini kuomba kutekeleza hukumu ya nchi nyingine.
“Kesi ya msingi ya kiasi kilichobaki kwamba tukilipe haikusikilizwa, yeye aliomba maombi madogo ambayo pia yana sehemu mbili,  kusikilizwa wote (Serikali ya Tanzania na mdai) na mahakama au kusikilizwa yeye mwenyewe kama alivyofanya,” amesema Dk Abbas.

Friday, August 23, 2019

Air Tanzania yazuiwa kuruka na mahakama Afrika kusini



Dar es Salaam. Ndege ya Air Tanzania iliyokuwa inatoka Afrika Kusini kwenda jijini Dar es Salaam, Tanzania imezuiwa kuruka kwa amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg nchini humo.
Taarifa iliyotolewa jana Ijumaa   Agosti 23, 2019 na katibu mkuu Wizara ya Ujenzi,  Uchukuzi na Mawasiliano, Dk Leonard Chamuriho inaeleza kuwa Serikali ya Tanzania kupitia ofisi ya mwanasheria mkuu inafuatilia suala hilo ili ndege hiyo iachiwe na kuendelea na safari zake kama kawaida.
"Waziri wa Ujenzi,  Uchukuzi na Mawasiliano anaomba radhi kwa usumbufu uliojitokeza kwa abiria wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) waliokuwa wanasafiri leo kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Oliver Tambo,  Johannesburg kuja Dar es Salaam kufuatia ndege hiyo kushindwa kufanya safari kama ilivyopangwa, " inaeleza taarifa hiyo.
Inabainisha kuwa kwa mujibu wa taarifa ambazo Serikali imepokea kutoka kwa balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, ndege hiyo imezuiwa kwa amri ya mahakama hiyo.

Thursday, August 22, 2019

Rais Magufuli ataka mabalozi wajitathimini



Rais wa Tanzania, John Magufuli


Dar es Salaam. Mabalozi wa Tanzania wanaoiwakilisha katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa nchi hiyo, John Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.
Mabalozi hao 43 ambao wapo Tanzania tangu  Agosti 13, 2019 wametoa pongezi hizo leo Alhamisi Agosti,22, 2019 walipokutana na kuzungumza na Rais Magufuli Ikulu Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya miradi waliyoitembelea mabalozi hao ni ujenzi wa bwawa la Nyerere litakalozalisha megawati 2,115 katika mto Rufiji, ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa, jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere na ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nojuma.
Pia, walitembelea Zanzibar katika ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, ujenzi wa jengo la tatu la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi na ujenzi wa barabara ya Kaskazini - Bububu – Mkokotoni .
Mabalozi hao wameeleza utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali ya Tanzania katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Akizungumza baada ya kuwasikiliza Mabalozi hao, Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha nchi na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.

Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.
“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” amesema Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc)
Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.
“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Rais Magufuli.
Kuhusu changamoto mbalimbali walizomueleza, Rais Magufuli ametoa wito kwa Mabalozi hao kuzishughulikia pale ambapo wao wenyewe wana uwezo na amemtaka Wizara ya Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi kufanyia kazi taarifa wanazopelekewa na Mabalozi  hao kwa wakati.

Wednesday, August 21, 2019

Tanzania Kukopeshwa sh.3.9 Trilioni na Benki ya Dunia



Dar es Salaam.  Benki ya Dunia (WB) imesema ipo tayari kuipaTanzania mkopo wa masharti nafuu wa Dola 1.7 bilioni ambazo ni zaidi ya Sh3.9 trilioni.
Fedha hizo ni zile zilizobaki katika fungu awamu ya 18 ya mgao wa chama cha kimataifa cha maendeleo (IDA) kilichopo ndani ya WB ambacho hujihusisha na kuzisaidia nchi masikini zaidi duniani kupambana na umasikini.
Leo Jumatano Agosti 21, 2019 mkurugenzi mtendaji wa WB anayesimamia nchi 22 zilizoko Kanda ya Afrika, Anne Kabagambe amemueleza Waziri wa Fedha na Mipango wa Tanzania, Dk Philip Mpango kuwa kiasi hicho cha fedha kinatarajiwa kutolewa kabla ya kuanza mgao mpya wa 19 wa IDA utakaoanza Julai 2020.
Kabagambe ambaye yupo nchini kwa  ziara ya kikazi amesema fedha hizo zitatolewa mara baada ya kukamilisha taratibu zote za upatikanaji wake.
”Fedha hizi zitaelekezwa katika kutekeleza miradi kadhaa muhimu ikiwemo ya elimu, afya, mradi wa kusaidia kaya masikini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) awamu ya pili na uendelezaji wa miji na masuala ya uchumi jumuishi  Zanzibar,” amesema Kabagambe
Taarifa iliyotolewa na wizara ya fedha imeeleza  Kabagambe amepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali ya Tanzania katika kupiga vita rushwa na ufisadi pamoja na kutekeleza miradi ya jamii ikiwemo reli na kufua umeme.

Kwa upande wake, Dk Mpango ameiomba benki hiyo kuisaidia Serikali kwa kuipatia fedha za kufanikisha ujenzi wa miundombinu hiyo ya umeme, reli, maji safi na salama, kuimarisha sekta ya kilimo, viwanda, bandari, rasilimali watu na masuala ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Amesema miradi hiyo itachochea zaidi ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa wananchi kwa kuwa nishati ya umeme itachochea ukuaji wa sekta ya viwanda hivyo na kukuza ajira, na reli itaimarisha sekta ya usafiri na uchukuzi.

Tuesday, August 20, 2019

Ajari ya moto Morogoro waliofariki wafikia 99


  • Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Morogoro (RC) nchini Tanzania, Dk Stephen Kebwe amesema vifo vinavyotokana na ajali ya lori la mafuta ya petroli kuanguka kisha kuwaka moto imefikia 99 baada ya majeruhi wawili kufariki dunia.
Majeruhi hao waliofariki ni kati ya 18 waliokuwa wamelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo jioni Jumanne Agosti 20,2019, Dk Kebwe amesema, “Kwa taarifa ambazo tumezipata kutoka Muhimbili hadi leo saa 10 jioni, majeruhi wawili kati ya 18 wamefariki dunia na kufikisha idadi ya vifo 99.”
“Kwa maana hiyo kwa sasa kuna majeruhi 16 huku Morogoro na 16 Muhimbili wakiendelea na matibabu,” ameongeza mkuu huyo wa mkoa.
Ajali hiyo ya lori ilitokea asubuhi ya Jumamosi Agosti 10, 2019 eneo la Msamvu mkoani Morogoro baada ya kuanguka kisha kulipuka.

Monday, August 19, 2019

Uchaguzi Serikali za Mitaa waziri Jafo atoa tamko

Image result for jafo


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania imesema inatarajiwa kutangazwa tarehe maalum ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa huku kampeni za uchaguzi huo zikifanyika kwa siku saba kabla ya siku ya uchaguzi.
Pia, uandikishwaji wa wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi huo utafanyika siku 47 kabla ya uchaguzi.
Hayo yalisemwa jana Jumatatu Agosti 19,2019 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Suleimani Jaffo katika mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha Azam.
Alisema kutakuwa na tukio rasmi la kutangaza tarehe ya uchaguzi ambayo pia itaenda sambamba na ugawaji wa kanuni zitakazosimamia uchaguzi.
“Hakuna mtu anayejua tarehe ya uchaguzi, japokuwa vyama vyote vya siasa vilivyosajiliwa vilishiriki katika uandaaji wa kanuni, katibu tawala, asasi za kiraia, wakuu wa wilaya na mikoa,” alisema Waziri Jafo
Akizungumzia kujiandikisha alisema licha ya kufanyika kwa uchaguzi kama huo mwaka 2014 na watu kujiandikisha lakini hawatakuwa na sifa ya kupiga kura mwaka 2019.

“Kutakuwa na daftari jipya, kila kanuni inakuja na daftari lake, watu watajiandikisha katika mitaa yao na itakuwa ni siku 47 kabla ya.”
“Na kabla ya uchaguzi, kutakuwa na siku saba za kampeni na kwa serikali za mitaa ni nyingi sana kwa sababu siku moja wanaweza kumaliza mitaa yote na kwa hizo siku tulizotoa si ajabu wakapita nyumba kwa nyumba,” alisema Jaffo.

Air Tanzania yatumika kumrudisha wazari mkuu wa Eswatini



Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Eswatini, Sibussiso Dhlamini ameondoka  jijini Dar es Salaam, Tanzania leo Jumatatu Agosti 19, 2019 kurejea katika nchi hiyo kwa kutumia ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Ameondoka leo mchana na  ndege aina ya Airbus A220-300 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) huku akisindikizwa na Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa.
Dhlamini alikuwa nchini Tanzania kuhudhuria mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) uliomalizika jana Jumapili.

Magufuli sasa ahamishia nguvu SADC



Dar es Salaam. Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (Sadc), Rais John Magufuli amehamishia dhamira yake ya kutaka kuwapo kwa kasi ya maendeleo nchini katika jumuiya hiyo.
Katika hotuba yake ya kwanza mara baada ya kukabidhiwa wadhifa huo jana, Rais Magufuli alianza kwa kuishukia Sekretarieti ya Jumuiya hiyo akisema imeshindwa kuzishauri nchi wanachama namna ya kuondokana na mkwamo wa kiuchumi.
Tangu alipoingia madarakani mwaka 2015, Rais Magufuli amekuwa akisisitiza utendaji kazi usiokuwa wa mazoea, kujituma ili kuwasaidia wananchi hasa wanyonge kujikwamua kuichumi.
“Sisi siyo maskini,” alisema Rais Magufuli jana katika hotuba yake baada ya kukabidhiwa rasmi wadhifa huo na mtangulizi wake, Rais Hage Geingob wa Namibia.
Huku akitumia takwimu, mwenyekiti huyo mpya alitoa takwimu za miaka 10 kuonyesha namna gani ukuaji wa kiuchumi ulivyo wa kusuasua huku sekretarieti ikishindwa kutoa majibu au hata kuzishauri nchi wanachama namna ya kuvuka vikwazo vya kiuchumi.
Alisema takwimu za ukuaji wa uchumi kwa nchi za Sadc haujawahi kufika asilimia tano na kwamba mara ya mwisho ilikuwa mwaka 2008 ambako ulikuwa kwa asilimia 5.7 na kusema sekretarieti hiyo imeonyesha upungufu katika utendaji wake.

Huku akishangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo wa ufunguzi uliofanyika katika ukumbi wa Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere, mwenyekiti huyo alisema; “nchi zetu siyo maskini. Tuna rasilimali zote zinazoweza kutuondoa kwenye umaskini.”

Sunday, August 18, 2019

Ajari ya moto Morogoro vifo vyaongeezeka



Dar es Salaam. Idadi ya waliokufa kutokana na ajali ya moto iliyotokea mkoani Morogoro imefikia 95 baada ya majeruhi mmoja aliyekuwa amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kufariki jana usiku Jumamosi  Agosti 18, 2019.
Hadi jana mchana waliofariki katika ajali hiyo walikuwa 94 baada ya majeruhi mwingine kati ya 21 waliokuwa wamelazwa MNH kufariki.
Jana alasiri hospitali hiyo ilipokea majeruhi mwingine kutoka hospitali ya Mkoa wa Morogoro na kufanya idadi yao kuwa 21 lakini sasa wamebaki 20 baada ya mwingine kufariki jana saa nne usiku.
Ajali hiyo ilitokea Agosti 10, 2019 katika mtaa wa Itingi, Msamvu barabara ya Morogoro-Dar es Salaam baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka moto muda mfupi baada ya watu kuanza kuchota mafuta.
Akizungumza leo Jumapili Agosti 18, 2019 mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa MNH, Aminiel Aligaesha amesema aliyefariki dunia ni Rajabu Ally.
Amebainisha kuwa wagonjwa 20 wapo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU), madaktari wanafanya jitihada kuokoa maisha yao.

Amewaomba watu wa kada mbalimbali kuendelea kuchangia damu kuwasaidia majeruhi hao.

Saturday, August 17, 2019

Magufuli aitaka sekretarieti Sadc kujitathmini

Rais John Magufuli akizungumza kwa ajili ya


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli jana Jumamosi Agosti 17, 2019 amekabidhiwa uenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika na kuitaka sekretarieti ya jumuiya hiyo kujitathmini kuhusu ukuaji duni wa uchumi kwa nchi wanachama.

Akizungumza katika mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo,  Magufuli amesema kama hakuna jitihada kubwa zitakazofanywa na sekretarieti itakuwa vigumu kufikia lengo husika.
Katika mkutano huo uliofanyika  katika ukumbi wamikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Magufuli amesema changamoto kubwa ni uchumi, kwamba nchi wanachama zinapaswa kutumia mafanikio ya kisiasa kufikia mafanikio ya kiuchumi.
“Malengo ilikuwa kufikia asilimia saba ya ukuaji uchumi kwa nchi husika lakini tupo mbali na malengo yetu kiuchumi. Kuna sababu nyingi uchumi wetu kudorora. Mei mwaka hii nilitembelea nchi tano za Sadc kwa bahati mbaya tatu kati yake zilikuwa zimekumbwa na njaa na zilikuwa kwenye mchakato wa kuagiza chakula kutoka nje.”
“Wakati huo Tanzania ilikuwa na tani milioni 3.5 za chakula cha ziada. Matatizo mengi kama haya sekretarieti inafaa kuyaangalia na itusaidie, naamini tungepata majibu kutoka kwao kwa nini miaka 10 uchumi wa pato la ndani unashuka,” amesema Magufuli.

Tanzania mfano wa kuigwa SADC yavuka vigezo



katibu mtendaji wa Sadc, Dk Stegomena Tax

Dar es Salaam. Tanzania imetajwa kuvuka vigezo vya ukuaji uchumi kati ya nchi 16 wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc).
Imetajwa kuwa ni nchi ambayo imefanikiwa kukua kiuchumi kwa muda mfupi.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Agosti 17, 2019 na katibu mtendaji wa Sadc, Dk Stegomena Tax  wakati akifungua mkutano wa kilele wa jumuiya hiyo unaofanyika leo na kesho katika ukumbi wamikutano wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC)
Dk Tax amesema uhimilivu wa uchumi ni nyenzo muhimu katika kuleta maendeleo kwa nchi wanachama na kuzihamasisha nchi nyingine kukua kiuchumi.
"Nchi zilizokidhi vigezo katika nchi wanachama ni nyingi zinafanya vizuri na Tanzania ni nchi pekee iliyofikia kigezo cha asilimia 7 katika ukuaji uchumi. Huu ni mfano wa kuigwa,” amesema Dk Tax.

Friday, August 16, 2019

waliopigania uhuru Kenya Wanawake wakutana na Mama Maria Nyerere



Dar es Salaam. Mke wa Baba wa Taifa, Mama Maria Nyerere jana Ijumaa Agosti 16, 2019 alitembelewa na wanawake walioshiriki harakati za kupigania uhuru wa Kenya nyumbani kwake Msasani jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa wanawake hao uliongozwa na mwanaharakati, Muthoni Likimani (94) na mwenyeji wao,  Dan Kazungu ambaye ni balozi wa nchi hiyo nchini Tanzania, kupokewa na Mama Maria, Balozi Getrude Mongela; Spika mstaafu wa Bunge, Anne Makinda na Waziri wa Afya wa Tanzania, Ummy Mwalimu.
Walisema lengo la kuja Tanzania ni kumjulia hali Mama Maria kama ilivyo ada kwa viongozi kutembeleana.
Wakati Mama Maria akiwakaribisha wageni hao, Makinda amesema ni jambo la kushukuru Mungu kwa wanawake kukutana pamoja.
“Huu ni undugu ndani ya damu, umri wao ni mkubwa lakini wamepanda ndege na kuja nchini,” alisema Makinda.
Naye Ummy amesema, “Hii ndio asili ya jamii zetu ukiwa una wageni waalike na wenzako. Nimesisimka sana, nakiri wizara yetu haijafanya kuhusu wazee, tunaahidi kila mwaka kutenga siku na kukaa na wazee hasa wanawake walioleta ukombozi wa Taifa.”

Akizungumza katika hafla hiyo, Likimani aliwataka wanawake wa mataifa hayo kusimama imara na kukataa masuala ya fujo kwenye jamii.
“Tukatae fujo kwa sababu ikitokea kina baba wanakimbia lakini nyie mnabaki na hamuwezi kukimbia. Simameni imara na msipende kutukanana,” amesema Likimani.


Rais wa Shelisheli atua Tanzania kushiriki mkutano wa SADC

Rais wa Shelisheli, Danny Faure (kushoto)

Dar es Salaam. Rais wa Shelisheli, Danny Faure amewasilini katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam nchini Tanzania.
Rais Faure amewasili leo Ijumaa Agosti 16, 2019 saa 2:18 asubuhi na kupokewa na viongozi mbalimbali akiwemo Waziri wa Viwanda na Biashara wa Tanzania, Innocent Bashungwa.
Kiongozi huyo wa visiwa hivyo amekwenda Tanzania kuhudhuria mkutano wa wakuu wa nchi 39 wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika kesho Agosti 17 na 18, 2019.
Faure ni Rais wa pili kuwasili Tanzania akitanguliwa na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye aliwasili juzi Jumatano Agosti 14,2019 kwa ziara ya siku mbili ya jana na leo kisha kesho atashiriki mkutano huo wa SADC.

Thursday, August 15, 2019

Alichozungumza Magufuli mbele ya Rais Ramaphosa

Rais John Magufuli akimpongeza Rais wa Afrika


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amezitaka nchi za Tanzania na Afrika Kusini kujikita katika ujenzi wa viwanda huku akifungua milango kwa wanaotaka kujenga viwanda nchini na kuweka wazi hali halisi ya sasa kiuwekezaji.
Akizungumza  Agosti 15, 2019 wakati wa mkutano wa baraza la wafanyabiashara wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) lililokutanisha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini.
Katika baraza hilo, limehudhuriwa pia na Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, mawaziri wa nchi hizo mbili pamoja na wafanyabiashara.
Mafuguli ameyataja maeneo ambayo wawekezaji kutoka nchi hiyo wanaweza kuwekeza ikiwemo ujenzi wa viwanda vya nguo, mazao yatokanayo na nyama, samaki, viwanda vya magari, viwanda vya dawa na maeneo mengine.
Amesema lengo ni kupunguza bidhaa ghafi zinazokwenda nje ambazo zikiachwa katika nchi husika zitaweza kuzalisha ajira nyingi kwa vijana.
“Tunahitaji kutengeneza nguo kwa pamba zetu na Tanzania ni ya pili kuwa na mazao ya nyama ikiongozwa na Ethiopia, tutaweza kuzalisha viatu na bidhaa zingine zitokanazo na ngozi, tunao samaki katika bahari na maziwa yetu, lengo kufikia mahali ambapo tunaweza kuzalisha bidhaa zetu hapahapa ndani ya nchi. Milango iko wazi kwa ajili ya uwekezaji,” amesema.

Akizungumza suala la kukuza viwanda na uwekezaji, Rais Magufuli amesema mifumo wezeshi inawekwa ili kuwezesha Tanzania ya viwanda akiitaja miradi kadhaa ikiwemo nishati katika bonde la Rufiji, ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara, reli, anga.
“Tumeweza kufufua shirika letu la Air Tanzania na hivi sasa kuna ndege inayotoka hapa nchini na kwenda Afrika Kusini mara nne kwa wiki, hii itasaidia kuwezesha biashara na uwekezaji lakini pia kukuza  utalii wa ndani kati ya nchi zetu mbili, lakini pia bandari zinatanuliwa na kujengwa,” amesema.
Aidha Magufuli amesema Afrika Kusini imefanikiwa kuwekeza katika makampuni 228 nchini Tanzania na kuzalisha ajira zipatazo 21,075 na hivyo kuwa nchi ya 13 yenye uwekezaji mkubwa kiuchumi ndani ya nchi.

Rais Magufuli, Ramaphosa watangazia fursa za uwekezaji



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amewakaribisha wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja kuwekeza nchini humo kwenye sekta mbalimbali zikiwemo sekta za afya, hoteli, utalii wa fukwe na uchakataji wa madini.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Alhamisi Agosti 15,2019 Ikulu jijini Dar es Salaam baada ya mazungumzo na Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ambaye aliwasili nchini jana Jumatano kwa ziara ya siku mbili kisha kushiriki mkutano wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Amesema Tanzania inatenga kila mwaka zaidi ya Sh270 bilioni kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba na asilimia 98 ya fedha hizo zinakwenda kununua nje ya nchi. Hivyo, amewakaribisha kuja kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa sababu ni fursa kubwa.
Pia, amewakaribisha kuwekeza kwenye sekta ya utalii hasa kwa kujenga hoteli na kuendeleza utalii wa fukwe wa kilomita 1,400 kuanzia Moa mpaka Msimbati. Amesema eneo hilo linahitaji wawekezaji ili kuongeza idadi ya watalii hapa nchini.
“Kupitia Rais Ramaphosa, nimewaalika wafanyabiashara kuja kujenga viwanda nchini ikiwemo viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vya madawa na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye madini,” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli amemhakikishia Rais Ramaphosa kwamba Tanzania itanunua vifaa ambavyo vinatengenezwa Afrika Kusini badala ya kwenda kununua nchi za mbali.

Amesema tayari wameanza kutekeleza hilo kwa kununua pikipiki ambazo zitatumika kwenye mkutano wa SADC.
Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amewakaribisha wafanyabiashara kwenda kuwekeza Afrika Kusini.
Amesema ni muhimu kwa nchi hizo kutumia fursa zinazojitokeza kwa manufaa ya wananchi wao.
Pia, Ramaphosa amesema nchi yake iko tayari kutumia fursa ya kujifunza lugha ya Kiswahili licha ya kuwepo kwa lugha mbalimbali zinazozungumzwa nchini mwake.
Amesema Afrika Kusini itatoa ushirikiano katika kipindi chote ambacho Tanzania itakuwa mwenyekiti wa SADC.
“Tunatambua Rais Magufuli anakuwa mwenyekiti wa SADC, nimemhakikishia kwamba tutampatia ushirikiano wote katika kudumisha amani, biashara na ushirikiano baina yetu,” amesema kiongozi huyo wa Afrika Kusini.

Rais wa Afrika kusini akutana na R ais Magufuli ikulu ya Tanzania



Dar es Salaam. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amemtembelea Rais John Magufuli wa Tanzania katika Ikulu ya Dar es Salaam leo Alhamisi Agosti 15,2019.
Rais Ramaphosa ameongozana na mke wake, Dk Tshepo Motsepe ambao wamepokelewa na mwenyeji wao, Rais Magufuli na mkewe, Janeth katika viwanja vya Ikulu.
Mara baada ya kuwasili, Kiongozi huyo wa Afrika Kusini amepata heshima ya kupigiwa wimbo wa taifa na mizinga sanjari na kukagua gwaride maalum lililoandaliwa maalum kwa ajili yake. 
Kiongozi huyo aliwasili jana usiku Jumatano Agosti 14,2019 kwa ziara ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, John Magufuli ambapo baada ya ziara hiyo, Rais Ramaphosa atashiriki Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika nchini humo Agosti 17 na 18, 2019.
Baada ya kutoka Ikulu hiyo ya Tanzania, Rais Ramaphosa atakwenda ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kwenye Jukwaa la Biashara na kesho Ijumaa ya Agosti 16, 2019 saa 3 asubuhi, Rais Ramaphosa atatembelea kambi ya wapigania uhuru Mazimbu mkoani Morogoro.


Wednesday, August 14, 2019

Rais wa Afrika Kusini atua Tanzania

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa

Dar es Salaam. Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa ameingia nchini Tanzania usiku wa kuamkia leo Alhamisi Agosti 15,2019 kwa ziara ya siku mbili kufuatia mwaliko wa Rais wa nchi hiyo, John Magufuli.
Ziara hiyo itawawezesha viongozi hao kujadili mambo yanayohusu nchi hizo, Bara la Afrika na mambo ya kimataifa na kujihakikishia wajibu wao katika ushirikiano wa karibu.
Ziara hiyo inakuja zikiwa zimebaki mbili kuelekea mkutano wa kawaida wa 39 wa viongozi wa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) utakaofanyika jijini Dar es Salaam Agosti 17 na 18, 2019 katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere.
Leo Alhamisi Agosti 15, 2019 saa 2: 00 atafanya mazungumzo Ikulu ya Dar es Salaam na mwenyeji wake Rais Magufuli na saa 5 hadi 8 mchana atakuwa ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) kwenye Jukwaa la Biashara.
Ijumaa ya Agosti 16, 2019 saa 3 asubuhi, Rais Ramaphosa atatembelea kambi ya wapigania uhuru Mazimbu mkoani Morogoro.
Mwaka 2011 makubaliano ya kuanzisha tume ya mataifa mawili (BNC) kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulisainiwa.

Uzinduzi wa BNC ulifanyika Tanzania mwaka 2017 na nchi ya Afrika Kusini itahodhi mkutano kama huo katika tarehe itakayopangwa.
Tanzania inaagiza bidhaa mbalimbali kutoka Afrika Kusini katika eneo la uzalishaji wa viwanda, mashine, vifaa vya kimakanika, karatasi, bidhaa za mpira, magari, vyuma, teknolojia na huduma.
Kwa upande mwingine, Tanzania inasafirisha Afrika Kusini bidhaa ambazo ni dhahabu, kahawa, korosho na pamba.
Kuna zaidi ya kampuni 170 za Afrika Kusini zinazofanya kazi Tanzania katika nyanja zote za kiuchumi.
Rais Ramaphosa ataambatana na mawaziri akiwemo waziri wa ulinzi, maveterani wa jeshi, waziri wa viwanda na biashara, madini na nishati na usalama wa ndani.
Baada ya ziara hiyo Rais Ramaphosa atauongoza ujumbe wake katika mkutano wa 39 wa viongozi wa SADC.