
Wizara ya afya nchini Tanzania imethibitisha kuwa watu 84 wapya wameambukizwa virusi vya corona na kufikisha idadi ya wagonjwa wa Covid-19 kufikia 254.
Wagonjwa 23 kati hao 84 waliothibitishwa ni wale waliotolwa na Wizara ya Afya ya Zanzibar Jumatatu.
Habari zaidi kutoka wizara hiyo zinaarifu kuwa watu watatu wapya wamefariki kutokana na sababu zinazohusiana na maradhi ya Covid-19.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo wagonjwa wote walioripotiwa Tanzania bara wanaendelea kupata nafuu isipokuwa wanne ambao wanahitaji uangalizi maalum.
Kufikia sasa katika eneo la Tanzania bara wagonjwa wameambukizwa kama ifuatavyo kwenye mabano Dar es Salaam(33), Arusha (4),Mbeya(3), Dodoma (3), Kilimanjaro(3), Pwani,(3) Tanga(3), Manyara(2), Tabora(1), Ruvuma(2), Morogoro(2) Rukwa(2), Kagera(1), Mara(1) na Lindi (1).
Marchi 17, Tanzania ilitangaza kufunga shule zote kwa siku 30 ikiwa ni hatua ya kuzuia kuenea kwa maambukizi ya corona nchini humo.
Pamoja na kuzuia mikusanyiko yote ya watu wengi yakiwemo matamasha ya muziki, mikutano ya hadhara mbalimbali ikiwemo ya kisiasa.
Awali Bunge la Tanzania lilithibitisha kwamba mmoja wa wabunge wake ameambukizwa virusi vya corona.
Taarifa hiyo imetolewa na naibu spika wa bunge Ackson Tulia japo hakutaja jina la mbunge huyo.
Aliongeza kuwa mbunge huyo anaendelea vizuri na kuongeza kuwa serikali inamuangalia na kumpatia matibabu stahiki.
Kulingana na maelezo ya mbunge huyo alisafiri na kwenda mjini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwa sasa vikao vya bunge hilo vimeahirishwa ili linyunyuziwe dawa ya kuzuia kusambaa kwa maambukizi ya virusi vya corona.
No comments:
Post a Comment