Wednesday, January 30, 2019

Spika, Zitto waitwa Mahakama Kuu leo



Dar es Salaam. Kesi ya kikatiba kuhusu kinga ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), kwa mujibu wa Katiba ya Nchi na Mamlaka ya Bunge katika kuwaita na kuwahoji watu mbalimbali, leo inatajwa rasmi mahakamani.
Kesi hiyo ya Kikatiba namba 01/2019 imefunguliwa Mahakama Kuu, Masjala Kuu na mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe dhidi ya Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Mahakama hiyo imetoa wito kwa wadau wote (mdai- Zitto na mdaiwa-Spika) ikiwataka kufika mahakamani leo kesi hiyo itakapotajwa kwa mara ya kwanza.
Kesi hiyo imepangwa kusikilizwa na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Firmin Matogolo, Dk Benhajj Masoud na Elinaza Luvanda.
Katika kesi hiyo, Zitto ambaye pia ni Kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo anaiomba Mahakama Kuu itoe tafsiri ya kinga ya CAG iliyopo kikatiba na tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge katika kushtaki watu wanaosemekana kulidharau Bunge.
Zitto alifungua kesi hiyo baada ya Spika kupitia kwenye vyombo vya habari na baadaye kumwandikia barua CAG, Profesa Mussa Assad akimtaka afike mbele ya kamati ya Bunge kuhojiwa kutokana na kauli aliyoitoa akiwa Marekani kuwa Bunge ni dhaifu.
Profesa Assad alitoa kauli hiyo kama maoni yake wakati akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Redio ya Umoja wa Mataifa, kulingana namna taarifa zake za ukaguzi zinavyofanyiwa kazi.
Kesi hiyo ilisajiliwa Januari 21 baada ya kukwama kwa siku saba kutokana na mvutano uliokuwapo baina ya upande wa mdai na Mahakama kutokana na kasoro zilizoainishwa.

Sunday, January 27, 2019

Majaji, Ma-DC, DED walioteuliwa na Rais Magufuli hawa hapa



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya za Tarime na Mwanga huku akiteua majaji 15 wa Mahakama Kuu na sita wa Mahakama ya Rufani.
Pia Rais Magufuli amewateua wakurugenzi 10 ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi kwenye halmashauri za mikoa mbalimbali nchini.
Taarifa ya Rais Magufuli iliyosomwa leo Jumapili Januari 27, 2019 kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi imeeleza kiongozi huyo ametengua uteuzi wa wakuu wa wilaya za Tarime, Glorious Luoga na Aaron Mbogho wa Mwanga.
“Nafasi ya Luoga imechukuliwa na Charles Kabeho aliyekuwa kiongozi wa mbio mwenge mwaka jana. Wakati nafasi ya Mbogho imechukuliwa na Thomas Apson,” amesema Balozi Kijazi.
Balozi Kijazi amewataja majaji wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa ni Dk Rehema Sameji, Dk Mary Levira, Ignas Kitusi, Winnie Korosso, Lugano Mwandambo  na Sahel Barke.
Majaji wa Mahakama Kuu ni Cyprian  Mkeha, Dustan Ndunguru, Seif  Kulita,  Dk Mtemi Kilikamajenga, Zeferine Galeba, Dk Juliana Masabo,  Mustafa Ismail,  Upendo  Madeha, Willbard  Mashauri,  Yohanne Masara,  Dk Lilian Mongella,  Fahamu  Mtulya,  John Kahyoza, Athuman Kirati na Suzan Mkapa.
Balozi Kijazi amewataja wakurugenzi wapya walioteuliwa kuwa na halmashauri zao kwenye mabano ni Isaya Mbenje (Pangani) Dk Fatuma  Mganga (Hai) Regina Bieda (Tunduma) Jonas  Malosa (Ulanga) Ali Juma Ali (Njombe) Misana Kangura (Nkasi) Diocres Rutema (Kibondo) Neto Ndilito (Mufindi) Elizabeth Gumbo (Itilima) Stephen Ndaki (Kishapu).
Majaji hao watapishwa Jumanne Januari 29, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam na Rais John Magufuli. Pia, Ma DC na Wakurugenzi watapaswa kuhudhuria shughuli hiyo.

Thursday, January 24, 2019

Majibu sita ya Magufuli kwa viongozi wa dini



Rais John Magufuli

Rais John Magufuli  
Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana kwa mara ya kwanza alikutana na viongozi wa dini na kujibu maombi yao waliyowasilisha kwake likiwamo la wananchi kuachwa wazungumze kwa kuwa hiyo ndio demokrasia.
Katika mkutano huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, viongozi hao walimuuliza pia kuhusu masuala ya uwekezaji, kamari, ajira, kilimo cha korosho, mabadiliko ya tarehe ya uchaguzi, maji, elimu ya dini pamoja na kilimo.
Katika majibu yake, Rais Magufuli alimtaka Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuyatafutia ufumbuzi baadhi ya masuala yaliyoelezwa na viongozi hao wa kiroho huku mengine akiyatolea majibu.
Kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Rais Magufuli aliwataka viongozi hao kusema ukweli na kutoa changamoto wanazoziona ili zifanyiwe kazi kwa sababu wao wanawakilisha kundi kubwa la jamii ya Watanzania.
“Leo ni siku ya kwanza kwa viongozi wa madhehebu mbalimbali kukaa kwa pamoja Ikulu hivyo nitapenda kusikiliza kutoka kwenu na nitazungumza machache baadaye kama yatakuwapo,” alisema.
Maswali na majibu
Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Amani Lymo alimuomba Rais Magufuli kuwaachia uhuru wananchi wa kuzungumza pale inapowezekana kwa sababu hiyo ndiyo demokrasia.
“Kwa kazi unayoifanya, watu hawatachagua maneno, bali watachagua kazi kwa hiyo kama kuna uwezekano waachie pumzi kidogo wazungumze lakini hawatakushinda kwa maneno yao,” alisema Lyimo.
Akijibu hoja hiyo, Rais Magufuli alisema kiongozi yeyote anaruhusiwa kuzungumza ikiwa ni pamoja na kufanya mikutano ya hadhara ndani ya majimbo yao kwa kufuata taratibu za kupata kibali kutoka polisi.
Alisema sababu ya kuzuiwa kufanya mikutano katika majimbo ya watu wengine ni kwa sababu za kiusalama hasa matumizi ya lugha za matusi.
“Nataka kuwahakikishia viongozi wa dini hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mkutano halali mahali alipo na bahati nzuri kwa mujibu wa sheria wanaotoa vibali ni polisi ukienda utapewa,” alisema.
“Wamefanya Dar es Salaam hapa sitaki kueleza yaliyotokea maana yapo mahakamani, wamefanya chaguzi zao ni mikutano, kwa hiyo nataka kukuhakikishia baba Mchungaji Lyimo hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano.”
Alisema anachotaka ni kuona vyama vinaiga mfano ya viongozi wa dini wanavyoheshimiana na kusaidiana kwa sababu ya umoja wao.
“Kama ni mbunge wa Ubungo afanye mkutano muda wote hakuna anayemzuia kwa sababu yeye ndiyo anawaongoza, mheshimiwa (Saed) Kubenea (mbunge wa Ubungo-Chadema) afanye hata siku nzima kwa sababu mimi naamini hiyo ndiyo demokrasia nzuri inayotakiwa,” alisema.
Kiongozi wa Maimamu Jimbo la Chalinze, Alhaj Hamisi Nassor alisema maji yamekuwa ni tatizo kubwa Chalinze jambo ambalo linafanya baadhi ya watu kushindwa kufanya ibada misikitini.
Alisema licha ya Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan kuambiwa kuwa ifikapo Desemba 31, mwaka jana tatizo hilo lingekuwa historia, badala yake limeongezeka.
“Mbunge analia, mkuu wa wilaya, mkoa wanalia maji, waziri mkuu analia, vilio hivi vimetoka huko chini hadi kufika huku juu. Hebu fikiria ule mradi wa Wami ni jipu basi watumwe watu ionekane pale kuna tatizo gani ambalo linafanya mradi usikamilike maji yawafikie watu,” alisema.
“Hadi tunanunua ndege tumefika mbali sana, sasa kwa nini pale Chalinze maji yasipatikane?”
Akijibu swali hilo, Rais Magufuli alisema makandarasi wamekula karibu fedha zote za mradi wa Chalinze na kwamba ili kumfukuza ni lazima atafute fedha za kutangaza upya mradi huo.
“Unajua ukikuta chungu kimeharibika kukifinyanga kikae sawa unachukua muda, huo ndio ukweli lakini nataka nieleze mradi wa Chalinze ni muhimu na ndio maana aliyekuwa waziri wa Maji hatukumpa mradi mwingine na aliyekuwa katibu mkuu hayupo kwa sababu wao ndiyo chanzo cha kuharibu mradi wa Chalinze na Lindi.”
Makamu mwenyekiti wa Jumuiya ya Mabohora Tanzania, Zainuddin Adamjee alisema miongoni mwa mambo yanayozungumzwa hivi sasa ni kamari kusema kauli ya Hapa Kazi Tu kwa kampuni za kamari imekuwa “hapa kamari tu.”
Kama ilivyokuwa korosho, kuhusu kamari Rais pia alimuagiza Waziri Mkuu Majaliwa kulifanyia kazi suala hilo kwa sababu linajenga tabia ya kutofanya kazi huku akitolea mfano kuwa katika nchi nyingine, mambo ya kamari hayatangazwi.
Askofu wa Kanisa la Biblia, John Mchopa alisema ana shaka na watu wanaofanya uhakiki wa korosho huku akibainisha kuwa anahisi kuna baadhi ya wakulima wataumizwa na suala hilo.
Alisema licha ya kuwa uamuzi uliochukuliwa na Serikali kununua korosho ni mzuri, uhakiki huo unafanyika taratibu mno na kuwafanya wananchi waendelee kuteseka.
“Kwa mfano, kanisa dogo la kijijini lina mikorosho yake michache sasa kwa sababu halina akaunti wakaamua kutumia ya mshirika mmoja na limekuwa tatizo mpaka leo hawajapata pesa zao,” alisema Mchopa.
“Sio kwamba wale wa kangomba peke yao tu ndiyo hawajalipwa, bali wapo baadhi ambao wana kilo 100 hawajapata malipo yao.”
Katika majibu yake katika hilo, Rais Magufuli aliwaagiza watendaji husika kuhakikisha malipo hayo yanafanyika huku akimuagiza Waziri Mkuu kusimamia.
“Kamati za uhakiki za korosho wasaini document (nyaraka) za watu wasikae wanawachelewesha watu kulipwa wakati pesa zipo, nataka wakulima wa korosho walipwe pesa mapema na fedha zipo.”
Kuhusu elimu na afya, Rais Magufuli alisema, “Serikali itaendelea kushirikiana nanyi katika utoaji wa huduma hizo hayo mengine ni changamoto na tutazishughulikia. Katika afya Serikali imesaini mikataba na hospitali 92 za taasisi za dini kwa ajili ya kuwapatia vifaa tiba.”
Kuhusu misamaha ya kodi, alisema taasisi za dini zinapostahili kupewa misamaha ya kodi zitapewa na mwaka 2016, zilisamehewa Sh19.66 bilioni, mwaka 2017 ilikuwa Sh17.6 bilioni na mwaka 2018 msamaha ulikuwa Sh46.84 bilioni.
Kuhusu mavazi yasiyo ya staha, Rais Magufuli alisema, “Tusaidiane katika kuhakikisha watu hawa kuheshimu maeneo mengine kama wanavyovaa nguo za heshima kanisani basi wafanye hivyo sehemu nyingine.”
Maombi mengine
Viongozi hao pia waligusia suala la kilimo cha umwagiliaji, ajira kwa vijana na kuwasilisha ombi la watendaji serikalini kujenga utamaduni wa kukutana na viongozi wa dini jambo ambalo Magufuli aliliridhia.
Viongozi hao pia walizungumzia suala la viongozi kuwaweka ndani watendaji mbalimbali.

Wednesday, January 23, 2019

Magufuli: Mikutano ya siasa haijazuiwa



Rais John Magufuli

Rais John Magufuli 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema hakuna kiongozi aliyezuiwa kufanya mkutano katika jimbo lake bali kilichozuiwa ni kwenda kufanya mikutano katika majimbo ya wengine tena kwa fujo.


Amesema kufanya hivyo ni sawa na askofu kutoka katika kanisa lake na kwenda kuwatukana watu msikitini jambo ambalo linaweza kuvuruga amani.
“Kama ninyi mnavyoheshimiana na sisi tunataka vyama vyetu vya siasa hata kama vipo 50 viheshimiane,” amesema.
“Nataka kuwahakikishia viongozi wa dini hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mkutano halali mahali alipo na bahati nzuri kwa mujibu wa sheria wanaotoa vibali ni polisi ukienda utapewa.”
“Wamefanya Dar es Salaam hapa sitaki kueleza yaliyotokea maana yapo mahakamani, wamefanya chaguzi zao ni mikutano, kwa hiyo nataka kukuhakikishia baba Mchungaji Lymo (Amani) hakuna mtu aliyezuiliwa kufanya mikutano,” amesema Rais Magufuli.
Amesema anataka vyama viige mifano ya viongozi wa dini wanavyoheshimiana na kusaidiana kwa sababu moja ya jambo analozingatia ni amani.
“Kama ni mbunge wa Ubungo afanye mkutano muda wote hakuna anayemzuia kwa sababu yeye ndiyo anawaongoza afanye mheshimiwa Kubenea (Saed) kwa sababu mimi naamini hiyo ndiyo demokrasia nzuri inayotakiwa.’’
Amesema ndiyo maana hivi sasa huwezi kumsikia Hillary Clinton akizunguka kufanya mikutano sehemu mbalimbali bali ni Donald Trump pekee kwa sababu ndiyo muda wake na atapimwa katika kipindi kilichopangwa.

Mwingira amweleza Magufuli anavyochukizwa na amri za Ma-DC

Kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume Josephat

Kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume Josephat Mwingira 
Dar es Salaam. Kiongozi wa Kanisa la Efatha, Mtume Josephat Mwingira amewataka wakuu wa wilaya kupunguza mamlaka ya kutoa amri za kuweka watu ndani kwa kuwa hiyo inaweza kusababisha wananchi kuiona Serikali ni mbaya.
Mtume Mwingira ametoa rai hiyo leo Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akitoa mchango wake wa mawazo kwenye mkutano maalum wa Rais Magufuli na viongozi wa madhehebu mbalimbali ya dini nchini.
Amesema viongozi hao wa wilaya wamejipa mamlaka ya kupitiliza kwa kuwakamata watu na kuwaweka ndani, akitolea mfano wachungaji wa kanisa lake wawili ambao amedai wameshawahi kukamatwa.
“La tatu ni la viongozi wetu wa wilaya, wanatoa amri ya kutia watu lokapu, ningeomba viongozi wetu wa wilaya wasiwe na mamlaka hayo, wamevuka mno, wameenda mbali mmo.”
“Unamuweka tu ndani halafu badaye humfungulii mashtaka wala nini, unamuacha unaenda umemdhalilisha mi naona kama wanaidhalilisha Serikali.”
 “Wakamkamata mchungaji wangu wa kwanza wakamtia ndani, nikauliza mkuu wa mkoa inakuwaje (bila kumtaja mkuu wa mkoa aliyemuuliza) mkuu wa mkoa akampigia simu mkuu wa wilaya akamuachia.”
“Unamuweka mtumishi wa Mungu ndani, haya mwingine ni yule wa Sengerema akamuweka mchungaji wangu ndani, nikamuuliza aniambie ee nimemuweka, nikamuuliza unataka tuione Serikali yetu ni mbaya au?”   amesema huku akimuahidi Rais Magufuli kuwa jambo jingine ataongea naye akipata nafasi ya kukutana naye.
Mkutano huo unaoendelea Ikulu umeitishwa na Rais Magufuli kujadili masuala mbalimbali ya kitaifa na viongozi wa dini.

Friday, January 18, 2019

Magufuli asema changamoto zilizosalia hazitapata kiongozi wa kuzitatua



Rais John Magufuli 

Rais john magufuli amesema kama kuna changamoto ambazo bado hazijafanyiwa kazi na uongozi wake hana uhakika kama kiongozi atakayekuja atakuwa na uwezo wa kuzitatua na kufafanua kuwa safari ya kutatua changamoto ina magumu mengi.

Magufuli ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 18, 2019 katika hafla ya makabidhiano ya mfumo wa kusimamia uwazi katika mawasiliano ya simu (TTMS) wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA).
Amesema katika safari ya kutatua changamoto anakutana na magumu mengi na ndiyo maana amekuwa akihitaji nguvu za Mungu kutekeleza majukumu yake.
“Viongozi wa dini endeleeni kuliweka Taifa hili kwenye mikono ya Mungu. Hii ni vita kama ilivyo nyingine na vita ya uchumi inahitaji maombi sana, bila maombi kazi hii haiwezi kufanyika,” amesema.
“Hao wanaokaa gizani hauwezi kujua ana kisu, ana panga au ameweka nyoka mfukoni lakini huko gizani huwa wanatolewa kwa maombi, yatawapumbaza huko gizani wasitake kufanya walichokusudia.”
Amesema kufanya hivyo kutawafanya viongozi wa nchi kusimamia misingi ya uadilifu na upendo wa kweli katika kulitumikia Taifa tajiri, lenye changamoto nyingi zinazohitaji kutatuliwa.

Wednesday, January 16, 2019

Shujaa uokoaji shambulizi la ugaidi Kenya amwagiwa sifa




Nairobi, Kenya. Mkufunzi wa usalama nchini Kenya, Inayat Kassam ambaye aliwaokoa mamia ya watu waliokuwa wametekwa kwenye jengo la Westgate mwaka 2013, ameibuka kinara tena kwenye tukio lililotokea jana nchini humo.

Tukio hilo lilikuwa la kigaidi ambapo Wakenya zaidi ya 800 walidhibitiwa kwenye jengo la Hoteli ya Dustid2 lililopo River Side jijini Nairobi.
Jengo hilo lilizingirwa na magaidi wa kundi la Al shabaab ambao walivamia jioni na kuua watu 14 kwa mujibu wa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo wamekuwa wakituma pongezi kwa Kassam ambaye alijitolea nguvu na maarifa kuwalinda na kuwaokoa watu kwenye mashambulizi hayo mawili.
Kassam ni raia wa nchi hiyo mwenye ujuzi wa kutumia silaha za moto na mkufunzi wa masuala ya usalama.
Mwaka 2013 alijitolea kuwaokoa watu ambao walinasa kwenye jengo la Westgate baada ya kuvamiwa na magaidi na kisha kuanza kushambulia ovyo katika maduka yaliyomo.
Kutokana na kujitoa kwake, Kassam ameendelea kujizolea umaarufu mitandaoni kutoka kwa Wakenya wakimsifu kwa ushujaa wake.


CCM waunga mkono marekebisho muswada vyama vya siasa

Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi

Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi Humphrey PolePole akizungumza wakati wa mkutano wa kutoa maoni ya mabadiliko ya muswada wa sheria ya vyama vya Siasa  unaofanyika jijini, Dar es Salaam leo. 
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho tawala kinaunga mkono utoaji wa maoni ya muswada wa vyama vya siasa wa mwaka 2018.
Amesema sheria inayotumika sasa ina mapungufu mengi yanayopaswa kurekebishwa kulingana na mazingira yaliyopo nchini.
Akizungumza leo Jumatano Januari 16, 2019 kwenye mkutano wa utoaji maoni ya wanachama wa CCM kuhusu muswada huo, Polepole amesema si kweli kwamba muswada huo umetoa madaraka makubwa kwa msajili wa vyama vya siasa.
“Msajili anatakiwa awe huru kuhoji kuhusu vyama vyetu ikiwamo vikao vilivyoketi kupitisha wagombea, kwa sasa mamlaka hayo hana na atapata ikiwa muswada huu utapitishwa kuwa sheria,” amesema Polepole.
Amesema mswada huo unasimamia kuona vyama vya siasa vinajiwekea mfumo thabiti wa demokrasia ndani ya vyama vyao ikiwamo namna ya kupata viongozi na uwazi kwenye mapato na matumizi ya fedha.
“CCM tunasema tunataka kuwa na sheria itakayosaidia vyama vya siasa kuwa makini na kutofanya mchezo yanapokuja masuala ya kuwajibika,” amesema.
Polepole amesema wanaunga hoja kuwa msajili awe na mamlaka ya kufuatilia vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
“Apite kuuliza jamani vipi mmefanya uchaguzi? Mwenyekiti wenu amechaguliwa? Tunataka aje kuuliza kwa sababu sheria ya awali inayotumika sasa haikumpa mamlaka hayo,” amesema.
Awali katibu wa siasa na mahusiano ya kimataifa wa CCM, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amewataka wanachana wa chama hicho kutoa maoni yao bila wasiwasi kuhusu muswada huo.
Amesema kusudi kubwa la muswada huo ni kutengeneza mazingira ya kuwaongoza Watanzania kulingana na mazingira yaliyopo.
Amesema muswada huo unapiga marufuku kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa jambo ambalo ni sahihi. “Kwa hiyo niseme tu muswada huu ni njia ya demokrasia, tumepewa haki ya kujadili,” amesema.

Thursday, January 10, 2019

Magufuli aeleza alivyosoma meseji za wateule wake



Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alieleza jinsi alivyosoma meseji za watendaji wake serikalini na kubaini baadhi yao wanagombana badala ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo yao.
Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua.
Alitoa mfano jinsi alivyosoma meseji za majibizano kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Zainabu Chaula ambaye jana aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya.
“Nilikuwa nazisoma meseji; meseji ya Waziri wa Afya na meseji ya Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, wanajibizana wee na wote wanatoka Tanga. Huyu mwingine anakaa kimya, huyu mwingine anashindilia maneno, nikaona nani anashindiliwa maneno zaidi, nikasema hawa njia ya kuwakomesha niwaweke wizara moja,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wote wawili wanafanya kazi vizuri, hivyo ameona bora wakae wizara moja. Alimpongeza Chaula kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa hospitali zaidi ya 300 ndani ya miaka mitatu.
Mbali ya viongozi hao, Rais Magufuli pia alisema anafahamu jinsi watendaji katika baadhi ya halmashauri wanavyogombana. Alitolea mfano Halmashauri ya Nyasa ambako alisema mkurugenzi na mkuu wa wilaya hawaivi.
Alitaja mgogoro mwingine kuwa uko Gairo ambako alisema mbunge wa anagombana na mkuu wa wilaya. Mbunge wa Gairo ni Mbunge wa jimbo hilo Ahmed Shabiby (CCM), na Mkuu wa Wilaya ni Siriel Mchembe.
Alisema mbunge amefikia hatua ya kutuma maneno ya kumtukana DC na kusema anashindwa kuelewa kwamba kuna kamati za nidhamu za CCM ambazo zinaweza kumfanya apoteze ubunge. “Nimewaangalia tu, I hope (natumai- mbunge) atafika siku moja aombe msamaha kwenye Bunge,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Pale Dodoma, mkurugenzi wa Jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha,”
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma i Godwin Kunambi na DC ni Patrobas Katambi.
Alisema japo kuongoza kuna changamoto nyingi, watendaji wengi wanafanya kazi vizuri na anatumaini kwamba wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano kila mmoja kwa nafasi yake katika eneo alilopangiwa.
Aliwataka viongozi hao aliowateua kwenda kufanya uamuzi bila woga katika kutekeleza majukumu yao.

Wednesday, January 9, 2019

Magufuli aanika mchongo wa wanaodaiwa kuiba dhahabu



Dar es Salaam. Rais John Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kwa kufanikishwa kukamatwa kwa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akizungumza leo Jumatano Januari 9, 2019 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi kadhaa aliowateua jana akiwemo waziri wa madini, Rais Magufuli amesema uimara wa kiongozi huyo ndio umefanikishwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao na askari waliotaka kufanikisha utoroshaji huo.
Amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliowakamata wahalifu hao walikula njama na kutaka kuwasaidia kutoroka baada ya kuahidiwa Sh1 bilioni.
“Mie ninashangaa watu wanaongea vitu wasivyovijua, nina taarifa za kutosha na katika hili nimpongeze sana IGP alisimama kidete kuhakikisha wote wanakamatwa na dhahabu ile inapatikana,” amesema.
“Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote,” ameongeza.
Akizungumzia mchongo mzima ulivyokuwa, Rais Magufuli amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliodai kuwafuatilia wahalifu hao nao walikuwa sehemu ya uhalifu
“Watuhumiwa walikamatwa tarehe 4 Misungwi (Mwanza), wakarudishwa mjini na kikosi cha polisi kilichoongozwa na Superintendent.”
“Walipoona wamewashika na mali ile wakawapeleka kituo cha polisi lakini hawakuwaingiza ndani wakakaa kwenye gari wakawa wanafanya majadiliano jinsi ya kuwahonga,” amesema.
Ameongeza, “Askari waliahidiwa Sh1 bilioni na wakapewa Sh700 milioni. Wakaondoka nao hadi kwenye Kivuko Kamanga wakawa wanawasindikiza wale wahalifu kwenda Sengerema kwa ajili ya kuwapatia milioni 300 iliyosalia.”
Amesema kundi hilo likiwa njia taarifa zikamfikia Kamanda wa Polisi Mkoa na mawasiliano yakafanyika hadi kumfikia yeye aliyeagiza wakamatwe.
Rais Magufuli amesema walipofika mbele walikuta kizuizi cha polisi wakasimamishwa ndipo gari la polisi lililokuwa nyuma likapiga king’ora na kudai walikuwa wakiwafuatilia.
Amesema aliagiza polisi hao wakamatwe na kunyang’anywa silaha kisha wakafungwa pingu na kurudishwa Mwanza ambapo watapelekwa mahakama ya kijeshi kisha baadaye mahakama za kiraia.

Tuesday, January 8, 2019

VIDEO: CAG Assad, Ndugai hapatoshi

Dodoma/Dar. Unaweza kusema hapatoshi kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na Spika Job Ndugai.
Hiyo ni baada ya jana Spika Ndugai kuitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma na kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge Januari 21 kwa hiari yake kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu madai ya kulidhalilisha Bunge, vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.
Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa katika kamati hiyo Januari 22 kwa madai ya kutoa kauli iliyounga mkono kilichosemwa na Profesa Assad.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai imeibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii huku watu wa kada mbalimbali wakiwamo wanasheria na wabunge wakitoa maoni kupinga.
Akihojiwa hivi karibuni na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na mtangazaji Anord Kayanda kuhusu ukaguzi unaofanywa na ofisi yake kuonekana na wananchi kuwa haufanyiwi kazi CAG alisema, “Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.”
“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”
Kwa kauli hizo, Ndugai pia alimtaka pia Profesa Assad ajitathmini kama anatosha katika nafasi yake.
“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.
“Mle ndani (bungeni) kuna mawaziri, Waziri Mkuu, spika na naibu wake. Kitendo hiki kimenikasirisha sikutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu Uhuru.”
Ndugai alisema si kweli kwamba Bunge ni dhaifu na kwamba wameipokea kauli hiyo kwa masikitiko kwa kuwa taarifa za CAG zinafanyiwa kazi.
“Sikatai Bunge kukosolewa, lakini nachukizwa na dharau na kwa kweli kama ni upotoshaji basi ofisi ya CAG ni wapotoshaji namba moja. Huwezi kusema una uhuru wa kuongea katika nafasi yako halafu unakwenda kutoa maneno ya tuhuma ya kudhalilisha nchi yako nje ya nchi,” alisema Ndugai.
Alisema kuna watu lazima watajitokeza na kuhoji kuhusu uhuru wa ofisi ya CAG na kusisitiza kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Alisema kilichozungumzwa na Profesa Assad ni sawa na mkimbizi ambaye anaweza kusema chochote, kwamba mtu mwenye misingi ya utaifa hawezi kusema vibaya Serikali yake akiwa nje ya nchi.
Alimtaka CAG kupeleka maelezo ya hoja moja baada ya nyingine ambazo hazikujibiwa au kufanyiwa kazi ili Bunge chini ya kamati zake mbili ambazo zinaongozwa na wabunge wa upinzani wakazifanyie kazi.
Kamati za Bunge zinazoongozwa na wapinzani ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kuhusu Mdee, Ndugai alisema aliunga mkono kilichozungumzwa na Profesa Assad, hivyo naye anapaswa kufika mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa.
Baada ya kauli ya Spika
Baada ya kauli hiyo, waandishi wetu walizungumza na baadhi ya wanasheria kupata maoni yao kuhusu hatua hiyo ya Spika. Akitoa maoni yake, wakili wa kujitegemea, Faraja Mangula alisema kwa mujibu wa Katiba wa nchi, Bunge linaweza kumuita mtu yeyote linapomhitaji bila kujali yeye ni nani, lakini alikosoa utaratibu ulioutumiwa na Spika.
“Katiba imelitaja Bunge kama chombo huru na CAG naye ametajwa kama taasisi huru ambayo haipaswi kuingiliwa na wote Katiba imewalinda. Kwa mfano, mchakato wa kumuondoa CAG madarakani ni mrefu na ilifanyika hivyo ili kumlinda,” alisema Mangula.
Alisema licha ya kuwa Bunge limepewa mamlaka ya kumuita mtu yeyote, lakini CAG ambaye Katiba inamlinda hajatendewa haki kwa namna alivyoitwa.
“Kwa maoni yangu naona Spika alipaswa kutumia njia za ndani kumuita kiongozi huyo badala ya kutumia kauli za kusherehesha kama vile kuna jambo baya sana amefanya.”
Wakili Albert Msando alisema Spika anapaswa kujitathmini kwani jambo alilolifanya linasababisha mgongano usio wa lazima baina ya Serikali, Bunge na ofisi ya CAG.
“CAG hawezi kuitwa kwa mkutano wa waandishi wa habari na Spika tayari ameitisha kamati ya maadili imshauri, lakini amekimbilia kufanya kazi ya kamati hiyo na anatoa lugha ya vitisho vya pingu na kumuita CAG,” alisema.
Alisema hoja ya Ndugai kuwa mtu hapaswi kusema vibaya mambo yanayohusu nchi akiwa ughaibuni haina mashiko kwani CAG alitoa kauli hiyo kulingana na mazingira, lakini vilevile ni haki yake kutoa maoni kuhusu jambo lolote.
Wakili Fulgence Masawe alisema Ndugai hakushauriwa vizuri kabla ya kutoa kauli hiyo na kwamba CAG amewekewa kinga katika Katiba ambayo ndio sheria mama na hakuna kanuni inayoweza kuwa juu ya msingi wa Katiba.
“Spika anamuita kwa mujibu wa kanuni ambazo ziko chini ya Katiba, haziwezi kuwa na mamlaka hayo, CAG anatakiwa kuwa huru kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa hiyo unapoanza kumwajibisha na kumwita mbele ya suala hili ni kuathiri utendaji na ukiukwaji wa sheria inayompatia uhuru wa kutekeleza majukumu yake,” alisema Masawe

Monday, January 7, 2019

Waziri Mkuu atoa uamuzi sakata la mawaziri wawili, RC

 


Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka kampuni zote zinazosambaza nguzo za umeme kulipa ushuru wa asilimia tano kwa kila nguzo kwa halmashauri wanakotoa nguzo hizo kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Alitoa uamuzi huo jana mjini Dodoma ikiwa zimepita siku mbili tangu alipowataka Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kufika ofisini kwake mjini hapa, ili wamweleze sababu zinazofanya nguzo za umeme kuzuiwa zisitoke kwenye halmashauri ikiwamo ya Mufindi.
Wito huo uliwahusu pia wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri zilizozuia nguzo hizo kusafirishwa.
Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Jumamosi iliyopita, Majaliwa alisema ni jambo la ajabu wananchi kukosa umeme kutokana na ukosefu wa nguzo wakati zipo, lakini zinazuiwa na watu wachache kwa masilahi yao.
Jana, katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, alisema ameagiza ushuru ulipwe baada ya kupata taarifa kuhusu kampuni ya New Forest ambayo ina mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco) wa kusambaza nguzo za umeme.
Alisema kwa muda mrefu kampuni hiyo imekuwa ikikaidi kulipa ushuru wa asilimia tano ya gharama ya kila nguzo na kusababisha ufike Sh2.9 bilioni, jambo lililoufanya uongozi wa Mkoa wa Iringa kuzuia nguzo hizo zisitoke.
Baada ya kupata maelezo hayo, alimuagiza Hapi kuiandikia madai kampuni hiyo ili ilipe ushuru huo kuanzia Julai 2018 walipoanza kusambaza nguzo.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama; Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Naibu Waziri Tamisemi, Josephat Kandege; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya pamoja na maofisa wengine wa Serikali.



Rais Bongo wa Gabon apinduliwa na wanajeshi wake



Gabon. Kundi la wanajeshi wa Gabon wametangaza kuipindua Serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Ali Bongo.

Kwa mujibu wa ripoti ya BBC leo Jumatatu Januari 7, 2019 wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita wanashika doria kwenye barabara za mji mkuu wa Libreville.
Amri ya kutotoka nje imetangazwa kupitia kituo cha redio ya Taifa ambacho kimedhibitiwa na wanajeshi hao kuanzia saa 11 alfajiri.
Katika matangazo yao redioni, wanasema kumekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wa Rais Bongo kuongoza Taifa hilo kwa madai kwamba afya yake si nzuri.
Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo kurejesha demokrasia. Wametangaza kwamba wataunda Baraza la Ukombozi ambalo ndilo litakaloongoza Serikali.
Wamekosoa hotuba iliyotolewa na Rais Bongo Desemba 31, wakisema mawazo yake hayakuwa kwenye mtiririko mzuri na sauti yake ilikuwa dhaifu, jambo ambalo linaonyesha kwamba afya yake si nzuri.
Rais Bongo amekuwa nje ya nchi akipata matibabu nchini Morocco kwa miezi miwili sasa kutokana na maradhi ambayo hayajabainishwa wazi.
Familia ya Bongo imetawala Taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita huku ikituhumiwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za Taifa hilo.
Rais Bongo alichukua madaraka mwaka 2009 kutoka kwa baba yake, Omar Bongo ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 40. Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, uchaguzi huo uligubikwa na ghasia na udanganyifu.