Nairobi, Kenya. Mkufunzi wa usalama nchini Kenya, Inayat Kassam ambaye aliwaokoa mamia ya watu waliokuwa wametekwa kwenye jengo la Westgate mwaka 2013, ameibuka kinara tena kwenye tukio lililotokea jana nchini humo.
Tukio hilo lilikuwa la kigaidi ambapo Wakenya zaidi ya 800 walidhibitiwa kwenye jengo la Hoteli ya Dustid2 lililopo River Side jijini Nairobi.
Jengo hilo lilizingirwa na magaidi wa kundi la Al shabaab ambao walivamia jioni na kuua watu 14 kwa mujibu wa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo wamekuwa wakituma pongezi kwa Kassam ambaye alijitolea nguvu na maarifa kuwalinda na kuwaokoa watu kwenye mashambulizi hayo mawili.
Kassam ni raia wa nchi hiyo mwenye ujuzi wa kutumia silaha za moto na mkufunzi wa masuala ya usalama.
Mwaka 2013 alijitolea kuwaokoa watu ambao walinasa kwenye jengo la Westgate baada ya kuvamiwa na magaidi na kisha kuanza kushambulia ovyo katika maduka yaliyomo.
Kutokana na kujitoa kwake, Kassam ameendelea kujizolea umaarufu mitandaoni kutoka kwa Wakenya wakimsifu kwa ushujaa wake.
Katibu wa Halmashauri Kuu Itikadi na Uenezi Humphrey PolePole akizungumza wakati wa mkutano wa kutoa maoni ya mabadiliko ya muswada wa sheria ya vyama vya Siasa unaofanyika jijini, Dar es Salaam leo.
Dar es Salaam. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole amesema chama hicho tawala kinaunga mkono utoaji wa maoni ya muswada wa vyama vya siasa wa mwaka 2018.
Amesema sheria inayotumika sasa ina mapungufu mengi yanayopaswa kurekebishwa kulingana na mazingira yaliyopo nchini.
Akizungumza leo Jumatano Januari 16, 2019 kwenye mkutano wa utoaji maoni ya wanachama wa CCM kuhusu muswada huo, Polepole amesema si kweli kwamba muswada huo umetoa madaraka makubwa kwa msajili wa vyama vya siasa.
“Msajili anatakiwa awe huru kuhoji kuhusu vyama vyetu ikiwamo vikao vilivyoketi kupitisha wagombea, kwa sasa mamlaka hayo hana na atapata ikiwa muswada huu utapitishwa kuwa sheria,” amesema Polepole.
Amesema mswada huo unasimamia kuona vyama vya siasa vinajiwekea mfumo thabiti wa demokrasia ndani ya vyama vyao ikiwamo namna ya kupata viongozi na uwazi kwenye mapato na matumizi ya fedha.
“CCM tunasema tunataka kuwa na sheria itakayosaidia vyama vya siasa kuwa makini na kutofanya mchezo yanapokuja masuala ya kuwajibika,” amesema.
Polepole amesema wanaunga hoja kuwa msajili awe na mamlaka ya kufuatilia vyama vya siasa vyenye usajili wa kudumu.
“Apite kuuliza jamani vipi mmefanya uchaguzi? Mwenyekiti wenu amechaguliwa? Tunataka aje kuuliza kwa sababu sheria ya awali inayotumika sasa haikumpa mamlaka hayo,” amesema.
Awali katibu wa siasa na mahusiano ya kimataifa wa CCM, Kanali Mstaafu Ngemela Lubinga amewataka wanachana wa chama hicho kutoa maoni yao bila wasiwasi kuhusu muswada huo.
Amesema kusudi kubwa la muswada huo ni kutengeneza mazingira ya kuwaongoza Watanzania kulingana na mazingira yaliyopo.
Amesema muswada huo unapiga marufuku kuanzishwa kwa vikundi vya ulinzi na usalama ndani ya vyama vya siasa jambo ambalo ni sahihi. “Kwa hiyo niseme tu muswada huu ni njia ya demokrasia, tumepewa haki ya kujadili,” amesema.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana alieleza jinsi alivyosoma meseji za watendaji wake serikalini na kubaini baadhi yao wanagombana badala ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika maeneo yao.
Alisema hayo Ikulu jijini Dar es Salaam jana baada ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua. Alitoa mfano jinsi alivyosoma meseji za majibizano kati ya Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu na aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, (Tamisemi), Zainabu Chaula ambaye jana aliapishwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya. “Nilikuwa nazisoma meseji; meseji ya Waziri wa Afya na meseji ya Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi, wanajibizana wee na wote wanatoka Tanga. Huyu mwingine anakaa kimya, huyu mwingine anashindilia maneno, nikaona nani anashindiliwa maneno zaidi, nikasema hawa njia ya kuwakomesha niwaweke wizara moja,” alisema Rais Magufuli.
Alisema wote wawili wanafanya kazi vizuri, hivyo ameona bora wakae wizara moja. Alimpongeza Chaula kwa jitihada zake za kusimamia ujenzi wa hospitali zaidi ya 300 ndani ya miaka mitatu.
Mbali ya viongozi hao, Rais Magufuli pia alisema anafahamu jinsi watendaji katika baadhi ya halmashauri wanavyogombana. Alitolea mfano Halmashauri ya Nyasa ambako alisema mkurugenzi na mkuu wa wilaya hawaivi.
Alitaja mgogoro mwingine kuwa uko Gairo ambako alisema mbunge wa anagombana na mkuu wa wilaya. Mbunge wa Gairo ni Mbunge wa jimbo hilo Ahmed Shabiby (CCM), na Mkuu wa Wilaya ni Siriel Mchembe. Alisema mbunge amefikia hatua ya kutuma maneno ya kumtukana DC na kusema anashindwa kuelewa kwamba kuna kamati za nidhamu za CCM ambazo zinaweza kumfanya apoteze ubunge. “Nimewaangalia tu, I hope (natumai- mbunge) atafika siku moja aombe msamaha kwenye Bunge,” alisema Rais Magufuli na kuongeza:
“Pale Dodoma, mkurugenzi wa Jiji na DC walikuwa wanagombana, nika-send message (nikatuma ujumbe) kwamba ‘endeleeni kugombana tu, mtagombania vijijini siku moja. Wamenyamaza naona yameisha,”
Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma i Godwin Kunambi na DC ni Patrobas Katambi.
Alisema japo kuongoza kuna changamoto nyingi, watendaji wengi wanafanya kazi vizuri na anatumaini kwamba wataendelea kufanya kazi kwa ushirikiano kila mmoja kwa nafasi yake katika eneo alilopangiwa. Aliwataka viongozi hao aliowateua kwenda kufanya uamuzi bila woga katika kutekeleza majukumu yao.
Dar es Salaam. Rais John Magufuli amelipongeza Jeshi la Polisi na Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro kwa kufanikishwa kukamatwa kwa dhahabu iliyokuwa inasafirishwa kwenda nje ya nchi.
Akizungumza leo Jumatano Januari 9, 2019 wakati wa hafla ya kuwaapisha viongozi kadhaa aliowateua jana akiwemo waziri wa madini, Rais Magufuli amesema uimara wa kiongozi huyo ndio umefanikishwa kukamatwa kwa watuhumiwa hao na askari waliotaka kufanikisha utoroshaji huo.
Amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliowakamata wahalifu hao walikula njama na kutaka kuwasaidia kutoroka baada ya kuahidiwa Sh1 bilioni.
“Mie ninashangaa watu wanaongea vitu wasivyovijua, nina taarifa za kutosha na katika hili nimpongeze sana IGP alisimama kidete kuhakikisha wote wanakamatwa na dhahabu ile inapatikana,” amesema.
“Inauma unapoona kilo zaidi ya 300 zenye thamani ya zaidi ya Sh30 bilioni zinakamatwa zikisafirishwa. Wameshaiona Tanzania ni nchi ambayo unaweza kufanya lolote,” ameongeza.
Akizungumzia mchongo mzima ulivyokuwa, Rais Magufuli amesema anazo taarifa za kutosha kuwa askari waliodai kuwafuatilia wahalifu hao nao walikuwa sehemu ya uhalifu
“Watuhumiwa walikamatwa tarehe 4 Misungwi (Mwanza), wakarudishwa mjini na kikosi cha polisi kilichoongozwa na Superintendent.”
“Walipoona wamewashika na mali ile wakawapeleka kituo cha polisi lakini hawakuwaingiza ndani wakakaa kwenye gari wakawa wanafanya majadiliano jinsi ya kuwahonga,” amesema.
Ameongeza, “Askari waliahidiwa Sh1 bilioni na wakapewa Sh700 milioni. Wakaondoka nao hadi kwenye Kivuko Kamanga wakawa wanawasindikiza wale wahalifu kwenda Sengerema kwa ajili ya kuwapatia milioni 300 iliyosalia.”
Amesema kundi hilo likiwa njia taarifa zikamfikia Kamanda wa Polisi Mkoa na mawasiliano yakafanyika hadi kumfikia yeye aliyeagiza wakamatwe.
Rais Magufuli amesema walipofika mbele walikuta kizuizi cha polisi wakasimamishwa ndipo gari la polisi lililokuwa nyuma likapiga king’ora na kudai walikuwa wakiwafuatilia.
Amesema aliagiza polisi hao wakamatwe na kunyang’anywa silaha kisha wakafungwa pingu na kurudishwa Mwanza ambapo watapelekwa mahakama ya kijeshi kisha baadaye mahakama za kiraia.
Dodoma/Dar. Unaweza kusema hapatoshi kati ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad na Spika Job Ndugai.
Hiyo ni baada ya jana Spika Ndugai kuitisha mkutano na waandishi wa habari ofisini kwake Dodoma na kumtaka Profesa Assad kufika mbele ya Kamati ya Maadili, Kinga, Haki na Madaraka ya Bunge Januari 21 kwa hiari yake kwa ajili ya kuhojiwa kuhusu madai ya kulidhalilisha Bunge, vinginevyo atapelekwa akiwa amefungwa pingu.
Mbali na CAG, mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee naye ameitwa katika kamati hiyo Januari 22 kwa madai ya kutoa kauli iliyounga mkono kilichosemwa na Profesa Assad.
Hatua hiyo ya Spika Ndugai imeibua mjadala mzito kwenye mitandao ya kijamii huku watu wa kada mbalimbali wakiwamo wanasheria na wabunge wakitoa maoni kupinga.
Akihojiwa hivi karibuni na Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa na mtangazaji Anord Kayanda kuhusu ukaguzi unaofanywa na ofisi yake kuonekana na wananchi kuwa haufanyiwi kazi CAG alisema, “Kama tunatoa ripoti zinazoonyesha kuna ubadhirifu halafu hatua hazichukuliwi, huo kwangu ni udhaifu wa Bunge. Bunge linatakiwa kusimamia na kuhakikisha pale panapoonekana kuna matatizo basi hatua zinachukuliwa.”
“Sisi kazi yetu ni kutoa ripoti. Na huu udhaifu nafikiri ni jambo lenye kusikitisha. Lakini ni jambo ambalo muda si mrefu huenda litarekebishika. Ni tatizo kubwa ambalo tunahisi Bunge linashindwa kufanya kazi yake kama inavyotakiwa.”
Kwa kauli hizo, Ndugai pia alimtaka pia Profesa Assad ajitathmini kama anatosha katika nafasi yake.
“Kama ni upotoshaji basi CAG na ofisi yake ndiyo wapotoshaji, huwezi kusema nchi yako vibaya unapokuwa nje ya nchi, na kwa hili hatuwezi kufanya kazi kwa kuaminiana,” alisema Ndugai.
“Mle ndani (bungeni) kuna mawaziri, Waziri Mkuu, spika na naibu wake. Kitendo hiki kimenikasirisha sikutegemea msomi kama huyo angeweza kutoa maneno ya kudhalilisha Bunge lililojaa wasomi zaidi ya mabunge yote tangu Uhuru.”
Ndugai alisema si kweli kwamba Bunge ni dhaifu na kwamba wameipokea kauli hiyo kwa masikitiko kwa kuwa taarifa za CAG zinafanyiwa kazi.
“Sikatai Bunge kukosolewa, lakini nachukizwa na dharau na kwa kweli kama ni upotoshaji basi ofisi ya CAG ni wapotoshaji namba moja. Huwezi kusema una uhuru wa kuongea katika nafasi yako halafu unakwenda kutoa maneno ya tuhuma ya kudhalilisha nchi yako nje ya nchi,” alisema Ndugai.
Alisema kuna watu lazima watajitokeza na kuhoji kuhusu uhuru wa ofisi ya CAG na kusisitiza kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania.
Alisema kilichozungumzwa na Profesa Assad ni sawa na mkimbizi ambaye anaweza kusema chochote, kwamba mtu mwenye misingi ya utaifa hawezi kusema vibaya Serikali yake akiwa nje ya nchi.
Alimtaka CAG kupeleka maelezo ya hoja moja baada ya nyingine ambazo hazikujibiwa au kufanyiwa kazi ili Bunge chini ya kamati zake mbili ambazo zinaongozwa na wabunge wa upinzani wakazifanyie kazi.
Kamati za Bunge zinazoongozwa na wapinzani ni ile ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ya Hesabu za Serikali (PAC).
Kuhusu Mdee, Ndugai alisema aliunga mkono kilichozungumzwa na Profesa Assad, hivyo naye anapaswa kufika mbele ya kamati hiyo kwa ajili ya kuhojiwa.
Baada ya kauli ya Spika
Baada ya kauli hiyo, waandishi wetu walizungumza na baadhi ya wanasheria kupata maoni yao kuhusu hatua hiyo ya Spika. Akitoa maoni yake, wakili wa kujitegemea, Faraja Mangula alisema kwa mujibu wa Katiba wa nchi, Bunge linaweza kumuita mtu yeyote linapomhitaji bila kujali yeye ni nani, lakini alikosoa utaratibu ulioutumiwa na Spika.
“Katiba imelitaja Bunge kama chombo huru na CAG naye ametajwa kama taasisi huru ambayo haipaswi kuingiliwa na wote Katiba imewalinda. Kwa mfano, mchakato wa kumuondoa CAG madarakani ni mrefu na ilifanyika hivyo ili kumlinda,” alisema Mangula.
Alisema licha ya kuwa Bunge limepewa mamlaka ya kumuita mtu yeyote, lakini CAG ambaye Katiba inamlinda hajatendewa haki kwa namna alivyoitwa.
“Kwa maoni yangu naona Spika alipaswa kutumia njia za ndani kumuita kiongozi huyo badala ya kutumia kauli za kusherehesha kama vile kuna jambo baya sana amefanya.”
Wakili Albert Msando alisema Spika anapaswa kujitathmini kwani jambo alilolifanya linasababisha mgongano usio wa lazima baina ya Serikali, Bunge na ofisi ya CAG.
“CAG hawezi kuitwa kwa mkutano wa waandishi wa habari na Spika tayari ameitisha kamati ya maadili imshauri, lakini amekimbilia kufanya kazi ya kamati hiyo na anatoa lugha ya vitisho vya pingu na kumuita CAG,” alisema.
Alisema hoja ya Ndugai kuwa mtu hapaswi kusema vibaya mambo yanayohusu nchi akiwa ughaibuni haina mashiko kwani CAG alitoa kauli hiyo kulingana na mazingira, lakini vilevile ni haki yake kutoa maoni kuhusu jambo lolote.
Wakili Fulgence Masawe alisema Ndugai hakushauriwa vizuri kabla ya kutoa kauli hiyo na kwamba CAG amewekewa kinga katika Katiba ambayo ndio sheria mama na hakuna kanuni inayoweza kuwa juu ya msingi wa Katiba.
“Spika anamuita kwa mujibu wa kanuni ambazo ziko chini ya Katiba, haziwezi kuwa na mamlaka hayo, CAG anatakiwa kuwa huru kwa mujibu wa sheria hiyo, kwa hiyo unapoanza kumwajibisha na kumwita mbele ya suala hili ni kuathiri utendaji na ukiukwaji wa sheria inayompatia uhuru wa kutekeleza majukumu yake,” alisema Masawe
Dodoma. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amezitaka kampuni zote zinazosambaza nguzo za umeme kulipa ushuru wa asilimia tano kwa kila nguzo kwa halmashauri wanakotoa nguzo hizo kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa.
Alitoa uamuzi huo jana mjini Dodoma ikiwa zimepita siku mbili tangu alipowataka Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi kufika ofisini kwake mjini hapa, ili wamweleze sababu zinazofanya nguzo za umeme kuzuiwa zisitoke kwenye halmashauri ikiwamo ya Mufindi.
Wito huo uliwahusu pia wakuu wa wilaya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri zilizozuia nguzo hizo kusafirishwa.
Akiwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Kijiji cha Nyoni wilayani Mbinga mkoani Ruvuma, Jumamosi iliyopita, Majaliwa alisema ni jambo la ajabu wananchi kukosa umeme kutokana na ukosefu wa nguzo wakati zipo, lakini zinazuiwa na watu wachache kwa masilahi yao.
Jana, katika taarifa iliyotolewa na ofisi yake, alisema ameagiza ushuru ulipwe baada ya kupata taarifa kuhusu kampuni ya New Forest ambayo ina mkataba na Shirika la Umeme (Tanesco) wa kusambaza nguzo za umeme.
Alisema kwa muda mrefu kampuni hiyo imekuwa ikikaidi kulipa ushuru wa asilimia tano ya gharama ya kila nguzo na kusababisha ufike Sh2.9 bilioni, jambo lililoufanya uongozi wa Mkoa wa Iringa kuzuia nguzo hizo zisitoke.
Baada ya kupata maelezo hayo, alimuagiza Hapi kuiandikia madai kampuni hiyo ili ilipe ushuru huo kuanzia Julai 2018 walipoanza kusambaza nguzo.
Viongozi wengine waliohudhuria kikao hicho ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenista Mhagama; Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani; Naibu Waziri Tamisemi, Josephat Kandege; Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji; Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya pamoja na maofisa wengine wa Serikali.
Gabon.Kundi la wanajeshi wa Gabon wametangaza kuipindua Serikali ya nchi hiyo inayoongozwa na Rais Ali Bongo.
Kwa mujibu wa ripoti ya BBC leo Jumatatu Januari 7, 2019 wanajeshi wenye vifaru na magari ya kivita wanashika doria kwenye barabara za mji mkuu wa Libreville.
Amri ya kutotoka nje imetangazwa kupitia kituo cha redio ya Taifa ambacho kimedhibitiwa na wanajeshi hao kuanzia saa 11 alfajiri.
Katika matangazo yao redioni, wanasema kumekuwa na wasiwasi juu ya uwezo wa Rais Bongo kuongoza Taifa hilo kwa madai kwamba afya yake si nzuri.
Wanajeshi hao wamesema wamechukua hatua hiyo kurejesha demokrasia. Wametangaza kwamba wataunda Baraza la Ukombozi ambalo ndilo litakaloongoza Serikali.
Wamekosoa hotuba iliyotolewa na Rais Bongo Desemba 31, wakisema mawazo yake hayakuwa kwenye mtiririko mzuri na sauti yake ilikuwa dhaifu, jambo ambalo linaonyesha kwamba afya yake si nzuri.
Rais Bongo amekuwa nje ya nchi akipata matibabu nchini Morocco kwa miezi miwili sasa kutokana na maradhi ambayo hayajabainishwa wazi.
Familia ya Bongo imetawala Taifa hilo kwa miaka 51 iliyopita huku ikituhumiwa kujilimbikizia mali na utajiri mkubwa kutokana na rasilimali za Taifa hilo.
Rais Bongo alichukua madaraka mwaka 2009 kutoka kwa baba yake, Omar Bongo ambaye aliiongoza nchi hiyo kwa miaka 40. Alishinda uchaguzi wa marudio mwaka 2016, uchaguzi huo uligubikwa na ghasia na udanganyifu.