Tuesday, January 28, 2020

Virusi vya Corona vyaanza kusambaa duniani



Dar es Salaam. Baadhi ya nchi zimeanza kutoa taarifa za wahisiwa wa ugonjwa wa virusi vya Corona, wakati mamlaka za China zikisema watu 106 wamepoteza maisha na zaidi ya watu 4,000 wameambukizwa.
Taarifa hiyo iliyotolewa leo Jumanne, Januari 28, 2020 na mashirika mbalimbali duniani, inaeleza baadhi ya nchi za Afrika zimeshatoa taarifa za kupata wahisiwa huku Ivory Coast ikiwa na mwathirika wa ugonjwa huo.
Licha ya kwamba Wachina wengi walisafiri kwa ajili ya sherehe za mwaka mpya na sasa wapo katika ratiba za kurejea nchi mbalimbali wanazoishi.
Hata hivyo, Mamlaka za China tayari zimeweka katazo kali la kusafiri na miji mikubwa kadhaa imesitisha huduma ya usafirishaji wa umma ili kuzuia maambukizi zaidi, hata hivyo katazo hilo halijataja iwapo raia hao hawaruhusiwi kutoka nje ya nchi hiyo.
Idadi ya walioambukizwa kimataifa imeongezeka kukiwa na taarifa za maambukizi mapya huko Singapore na Ujerumani.
Marekani, ambayo ina maambukizi ya watu kadhaa, imewataka raia wake, ''kufikiria upya suala la kusafiri'' kwenda China na imeshauri kutosafiri kwenda Hubei.

Sunday, January 26, 2020

Nguli wa kikapu, Marekani Kobe Bryant afariki dunia


Dar es Salaam. Nyota kikapu zamani wa timu ya L.A Lakers, Marekani Kobe Bryant amefariki dunia pamoja na wenzake wanne kwenye ajali ya helikopta iliyotokea California usiku wa kuamkia  leo tarehe 26 Januari 2020.

Taarifa kutoka Marekani zimeeleza kuwa Kobe Bryant alikuwa akisafiri kwa helikopta binafsi kabla haijalipuka na kuteketea kwa moto huko Calabasas.

Kwa mujibu wa Mamlaka jijini Los Angeles wameeleza kuwa jumla ya watu watano walikuwa kwenye helikopta hiyo na hakuna aliyenusurika katika ajali hiyo.

Kobe Bryant amefariki akiwa na umri wa miaka 41 akiwa na ameichezea timu ya mpira wa kikapu ya Los Angeles Lakers nchini Marekani kwa takribani miaka 20, hadi alipostaafu mwezi Aprili mwaka 2016

Miongoni mwa mafanikio ambaye Kobe Bryant alifanikiwa kuyapata ni pamoja na kuwa Mcheza kikapo mwenye thamani kubwa mwaka 2008, na mara mbili pia alikuwa ndiye mchezaji mwenye thamani hiyo kwenye fainali ya ligi ya NBA

Polisi Tanzania wamkamata Profesa Lipumba



Handeni. Mwenyekiti wa chama cha upinzani nchini Tanzania cha CUF, Profesa Ibrahim Lipumba amekamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Handeni Mkoa wa Tanga akidaiwa kufanya ziara bila kupewa kibali.
Profesa Lipumba amekamatwa leo Jumapili Januari 26, 2020 Kijiji cha Segera wilayani Handeni na kupelekwa kituo kikuu cha polisi wilayani humo kilichopo mjini Handeni.
Mkurugenzi wa Usalama wa CUF, Masoud Mhina amesema mwenyekiti huyo amekamatwa wakati akijiandaa kufungua tawi la chama hicho Kijiji cha Segera.
Amesema ameshangazwa na kitendo hicho cha polisi kumkamata Profesa Lipumba wakati tayari chama kilishawasilisha jeshi la polisi taarifa ya ziara hiyo.
Amesema Profesa Lipumba leo Jumapili ilikuwa anamaliza ziara yake ya siku saba mkoani Tanga na baada kumaliza mkutano wa ndani wa kijiji cha Mkata na kisha kwenda jijini Dar es Salaam.
Profesa Ibrahim Lipumba alianza ziara yake mkoani Tanga Jumapili iliyopita ambapo alianza Pangani, Mkinga, Muheza, Korogwe, Lushoto na leo alikuwa amalizie Handeni.
Jitihada za  kumpata Kamanda wa Polisi mkoa wa Tanga, Edward Bukombe zinaendelea ili kujua undani wa Polisi kumkamata Mwenyekiti huyo wa CUF.

Saturday, January 25, 2020

Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania(TMA) yatangaza mvua kubwa mikoa kumi nchini

Image result for mvua


Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari ya kunyesha kwa mvua kubwa katika mikoa mbalimbali nchini humo ikiwamo Jiji la Dar es Salaam.
Taarifa ya TMA imesema mvua hizo kubwa zinatarajia kunyesha leo Jumamosi Januari 25, 2020 kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na kusini mwa Mkoa wa Morogoro.
“Angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa Mbeya, Njombe, Iringa, kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, Pwani, Tanga, Dar es Salaam pamoja na visiwa vya Mafia, Unguja na Pemba,” imeeleza taarifa hiyo ya TMA
Imesema athari zinazoweza kujitokeza ni uharibifu wa miundombinu na mali kwa baadhi ya maeneo, baadhi ya makazi kuzungukwa na maji, hatari kwa maisha ya watu kutokana na maji yanayotiririka kwa kasi au maji yenye kina kirefu, ucheleweshwaji wa usafiri, kusimama kwa muda kwa baadhi ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kesho Jumapili Januari 26, 2020 TMA imesema mvua kubwa zitanyesha kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe, Ruvuma, Lindi, Mtwara pamoja na kusini mwa mkoa wa Morogoro.
Jumatatu Januari 27, 2020 angalizo la mvua kubwa limetolewa kwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Kigoma, Geita, Mwanza na Kagera huku Jumanne ijayo TMA ikitoa tahadhari ya mvua kubwa kwa baadhi ya maeneo ya Geita, Mwanza na Kagera.

Magufuli aionya CCM kuhusu upinzani

Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais John Magufuli


Dar es Salaam. Wakati joto la uchaguzi mkuu kwa mwaka huu likianza, Rais John Magufuli amewataka viongozi wa CCM wasibweteke na uimara wa chama hicho, akisema wapinzani nao wamebadilika na sasa wana mikakati mingi ya kutaka kushinda.
Mwenyekiti huyo wa chama hicho tawala alitoa onyo hilo katika mkutano wa viongozi wa chama hicho wa ngazi zote uliofanyika kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mkutano huo uliohusisha wenyeviti na makatibu wa CCM wa mikoa na wilaya zote nchini, ulilenga kusalimiana na kushirikisha viongozi hao kuhusu serikali yao.
Amesema hayo ikiwa takriban miaka minne baada ya mchuano mkali uliojitokeza katika uchaguzi wa mwaka 2015 ulioshuhudia wapinzani wakiungana na kufanikiwa kupata idadi kubwa ya kura za urais, huku wakiingiza idadi ya wabunge iliyoweka rekodi tangu kurejeshwa kwa siasa za ushindani mwaka 1992.
Katika uchaguzi huo, Magufuli alipata kura milioni 8.8 huku mgombea wa upinzani, Edward Lowassa, aliyeungwa mkono na vyama vinne, akipata kura milioni 6.07.
“Lazima sisi kama chama tujitathmini,” alisema Rais Magufuli, ambaye pia ameahidi uchaguzi ujao kuwa wa amani, huru na wa haki.
“CCM ya leo si kama ya nyuma. Lakini tutambue kwamba washindani wetu wa leo si sawa na wa nyuma. Nao wanabadilika, wanabuni mikakati mingi ya wazi na ya ndani, tusibweteke.”
Na ingawa CCM ilishinda kwa zaidi ya asilimia 90 katika uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa, Rais alisema ushindi huo usiwafanye wabweteke.
Hata hivyo, vyama kadhaa vya upinzani, vikiwemo vya Chadema, ACT Wazalendo na NCCR-Mageuzi vilisusia uchaguzi huo kwa madai ya wagombea wao kutotendewa haki na hivyo wagombea wa CCM kutangazwa washindi bila kupigiwa kura kutokana na kukosa wapinzani.
Lakini alikuwa na neno la faraja kwa viongozi hao wa wilaya na mikoa.
“Licha ya wao (wapinzani) kujipanga, ukitazama kwa umakini, Tanzania kwa sasa haina vyama vya upinzani vilivyo imara sana vinavyoweza kushindana na CCM,” alisema Magufuli.
“Unapoona watu wengi wanahama huko wanakuja CCM, ujue chama kina mvuto. Chama kiko imara. Tusibabaishwe na kelele ndogondogo za washindani wetu ambao nguvu zao zimekwisha.”
‘Hakuna mazingira sawa’
Lakini wapinzani walipokea kauli ya Rais kuwa nguvu za “washindani wao zimekwisha” kwa maoni tofauti, huku mjumbe wa Kamati Kuu ya CUF, Abdul Kambaya akisema “hakuna mazingira sawa ya ushindani katika uchaguzi”.
“Wakati tunaingia katika uchaguzi wa serikali za mitaa, wapinzani hatukupewa nafasi ya kurudisha fomu. Sasa unawezaje kupima nguvu yetu? Nadhani kwa kuwa alikuwa akiongea na viongozi wa CCM, alitaka kuwajengea ari ya kujiamini, wawe na morali wa uchaguzi,” alisema Kambaya.
Naye mkurugenzi wa mawasiliano wa Chadema, John Mrema alikosoa kikao hicho akisema kinaonyesha hofu ya chama dhidi ya upinzani kwa sababu hakipo katika chama hicho.
Hata hivyo, Mrema alisema anashangaa mwenyekiti wa CCM kukiri kwamba upinzani una mikakati mingi ya wazi. Alisema jambo hilo ndiyo linalomtia hofu na kuudhibiti upinzani wakati wa uchaguzi na wakati wote.
“Kama wanadhani upinzani ni dhaifu, kwa nini wasiweke Tume huru ya uchaguzi, tuingie uwanjani tushindane kwa haki? Hicho kitu hawataki kwa sababu wanajua nguvu yetu,” alisema Mrema.
Uchaguzi mkuu, ambao huhusisha uchaguzi wa Rais, wabunge, wawakilishi na madiwani, unatarajiwa kufanyika wiki ya mwisho ya mwezi Oktoba na Rais Magufuli alikuwa na neno kwa viongozi hao wa CCM.
“Wakati wa mchakato wa uchaguzi, tusiende na majina mfukoni; kwamba huyu ni wa mwenyekiti, huyu ni wa katibu,” alisema mwenyekiti huyo wa CCM.
“Wakati mwingine unakuta mwenyekiti na katibu wanagombana. Tuweke maslahi ya chama chetu mbele.
“CCM ina misingi, kanuni na taratibu za kupitisha majina ya wagombea wanaofaa, lakini baadhi ya viongozi hawaifuati.”
Alisema tabia hiyo imefanya chama kuwa kinapoteza wagombea wazuri kwa sababu ya migogoro ya ndani licha ya kuwa na wanachama wazuri ambao hunyimwa fursa ya kugombea kwa sababu tu viongozi wana watu wao.
Awapa majukumu viongozi
Rais Magufuli aliwakumbusha viongozi hao wajibu wao wanapokuwa maeneo ya kazi, akiwapa majukumu matatu ambayo ni kuisimamia Serikali katika maeneo yao, kukijenga chama kwenye ngazi ya mashina na matawi pamoja na kuitetea Serikali na kutangaza mafanikio yaliyopatikana.
Alisema miradi mingi ya Serikali inafanyika wilayani na mikoani, hivyo, aliwataka viongozi hao kufuatilia utekelezaji katika maeneo yao na wakiona haiendi vizuri, watoe taarifa kwa katibu mkuu.
Aliwataka viongozi hao kutangaza mafanikio yaliyofikiwa katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwa mambo mengi makubwa yamefanyika, hivyo, ni wajibu wao kuwaeleza wananchi.
“Nitashangaa kama kuna kiongozi wa CCM ambaye hatambui mageuzi makubwa yaliyofanyika katika awamu hii.
“Tumejenga hospitali 69 za wilaya, huduma za umeme mpaka vijijini, ujenzi wa reli ya kisasa kwa takribani Sh7 trilioni, mradi wa kufua umeme wa Stiglers. Mambo ni mengi,” alisema Rais Magufuli.
Pia, Rais Magufuli aliwataka viongozi hao kukiimarisha chama kwenye ngazi ya mashina na matawi kwa sababu nguvu ya chama inaanzia huko. Aliwataka kuongeza nguvu katika kuimarisha mashina na matawi katika maeneo yao.
Wajumbe 1,780 wahudhuria
Mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi 1,780 huku wajumbe 20 wakishindwa kuhudhuria.
“Ndugu mwenyekiti, ulinipa maelekezo ya kuitisha mkutano huu na ndani ya siku saba, wajumbe 1,780 wamehudhuria kati ya wajumbe 1800 waliotakiwa kuwepo,” alisema Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.
Wakati huohuo, Dk Bashiru amesema CCM iko kwenye mchakato wa kuandaa ilani ya uchaguzi na makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ataongoza kamati hiyo huku Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan akiwa makamu mwenyekiti na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwa mjumbe.


Friday, January 24, 2020

VIDEO: Mkutano wa Magufuli viongozi 1,780 wa ccm wahudhuria



Dar es Salaam. Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amesema mkutano wa chama hicho tawala ulioitishwa na Rais John Magufuli  umehudhuriwa na wajumbe 1,780 kati ya 1,800 waliotakiwa kuwepo.
Dk Bashiru ameyasema hayo leo Ijumaa Januari 24, 2020 katika mkutano huo unaofanyika katika ukumbi wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.

Walioshiriki mkutano huo ni viongozi wa CCM ngazi ya mikoa na wilaya kutoka Mikoa yote nchini.
Amesema wajumbe 20 wameshindwa kuhudhuria mkutano huo kwa sababu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na baadhi ya maeneo kutokuwa na viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya.                  

  
 “Ulinipa maelekezo (Magufuli-mwenyekiti wa CCM) ya kuitisha mkutano huu na wajumbe 1,780 wamehudhuria kati ya wajumbe 1,800 waliotakiwa kuwepo," amesema kiongozi mkuu huyo wa nchi.
Dk Bashiru amesema chama hicho kinajiandaa kuadhimisha miaka 43 tangu kuanzishwa kwake na kauli mbiu itakuwa, Tumeahidi, tumetekeleza.
Amesema chama hicho pia kinaandaa Ilani ya uchaguzi mkuu wa 2020 na kwamba makamu mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula ndiyo mwenyekiti wa kamati hiyo.
Amesema makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan ni makamu wa kamati hiyo na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ni mjumbe.
Amemhakikishia mwenyekiti wa chama hicho kwamba CCM iko imara na imejiandaa kushinda uchaguzi wa mwaka 2020 kutokana na utendaji mzuri wa viongozi wake wa ngazi mbalimbali.
Takribani wiki moja iliyopita zilisambaa taarifa za Rais Magufuli kuwaita viongozi wa CCM wa mikoa na wilaya kwa mazungumzo Ikulu jijini Dar es Salaam, kuzua mjadala kwenye baadhi ya mitandao ya jamii, huku baadhi ya viongozi wa CCM waliotafutwa kwa simu wakithibitisha kualikwa kuhudhuria mkutano huo.
Hata hivyo, baadhi ya viongozi waandamizi wa CCM waliopatikana walisita kuthibitisha kuwepo kwa mkutano huo, ambapo licha ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kutumiwa barua hiyo kwa njia ya mtandao baada ya kuiomba lakini hakujibu chochote.
Naye Katibu wa Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Kanali Ngemela Lubinga alipotafutwa kwa simu, alisema hana taarifa kwa kuwa yuko safarini, huku akimtaka mwandishi kuandika kama alivyoona kwenye mitandao ya jamii.
Barua iliyosambaa katika baadhi ya mitandao ya jamii  ilisema Januari 24, 2020 Rais Magufuli, ambaye ni Mwenyekiti wa CCM atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa chama hicho wa mikoa, wilaya na jumuiya zake Ikulu jijini Dar es Salaam.
Licha ya barua hiyo iliyotolewa na Torry Mkama ambaye ni katibu myeka wa katibu mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, ikionyesha kutolewa Januari 17, 2019 katika maelezo yake imeonyesha wajumbe wote watakaoshiriki mkutano huo wanatakiwa kuwasili jijini humo Januari 23, 2020.
Ila leo badala ya mkutano huo kufanyika Ikulu kama ilivyokuwa imeelezwa katika taarifa hiyo, umefanyika katika ukumbi wa JNICC.

Thursday, January 23, 2020

Virusi hatari vyazidi kusambaa, Serikali yasema imejipanga

Abiria wa usafiri wa ndege wakiwa wamefunika


 Wakati Shirika la Afya Duniani (WHO) likikutana leo jijini Geneva kuamua kama mlipuko wa virusi hatari nchini China unastahili kutangazwa kama “janga la dharura la afya kimataifa”, Tanzania imesema inafuatilia kwa karibu na imeweka tahadhari mipakani.
Virusi hivyo vya corona vinavyofanana na ugonjwa wa SARS (ugonjwa unaoathiri mfumo wa hewa), hadi jana ulikuwa umeua watu tisa nchini China na ulikuwa ukienea sehemu kadhaa, huku mgonjwa mmoja akibainika Marekani na Uingereza ikichukua hatua kudhiti wasafiri katika ndege zinazotoka moja kwa moja China.
Tayari virusi hivyo vimeshaathiri watu 440 nchini China na wengi wao wakitoka Wuhan, AFP imeripoti. Li Bin wa Kamisheni ya Afya ya Taifa ya China alikaririwa na AFP akisema watu 1,394 walikuwa wakiendelea kuangaliwa na wauguzi.
Lakini Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema tayari mifumo ya udhibiti ipo katika maeneo yote wanayopita wageni kuingia nchini.
“Kwa kuwa dunia ni kama kijiji, Serikali ya Tanzania inafuatilia kwa karibu mlipuko wa ugonjwa huu huko China,” alisema Dk Ndungulile.
“Hawa ni wenzetu na tuna ukaribu nao. Wataalamu wa afya hapa nchini tayari wanafanya ufuatiliaji kupitia mifumo yetu ambayo ipo tayari kugundua wagonjwa.
“Utaona hata huko China wenzetu pia wana vifaa kama vya kwetu vya thermo scanner. Sisi tumeifunga katika maeneo yote ambayo wageni wanaingia.”
Dk Ndugulile alisema wamefunga vifaa hivyo katika viwanja vya ndege ili kubaini mwenye homa, baada ya hapo tutamchukua na kumhoji ametoka wapi, historia yake ya safari. Yeyote anayehisiwa tunamuweka pembeni kwa uchunguzi zaidi.”
Naibu waziri huyo alisema mashine hizo zina uwezo wa kuwatambua watu wengi.
“Hata wawe 100 au ndege nzima vifaa vyetu ni vya kisasa sana. Si lazima kukagua mtu mmoja mmoja, hivyo vina uwezo wa kumbaini mgonjwa na tukamchukulia hatua za kumwangalia zaidi,” alisema.
Sampuli ya virusi vilivyochukuliwa kutoka kwa mgonjwa na kuchunguzwa katika maabara na maafisa wa serikali ya China pamoja na wale wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha ugonjwa huo unafanana na SARS kwa asilimia 80.
Korea Kusini pia iliripoti mtu aliyebainika kuwa na virusi hivyo Jumatatu baada ya Thaialnd na Japan.
Jijini Geneva, WHO inatarajiwa kutoa tamko la hali ya dharura iwapo itabaini virusi hivyo ni “hatari, vya dharura, si vya kawaida au havikutegemewa”.
Tamko hilo litamaanisha virusi hivyo vina hatari ya kusambaa zaidi duniani na kunahitajika kuchukuliwa hatua na jumuiya ya kimataifa.
Na tamko hilo likitolewa litakuwa likipitiwa kila baada ya miezi mitatu na kamati ya dharura ya WHO.
Kuhusu Coronavirus
Virusi hivyo ni familia kubwa ya virusi sita na kirusi hicho kipya kitaongeza idadi hiyo kufikia saba na ni maarufu kwa kusababisha ya maambukizi miongoni mwa binadamu.
Akiongea na AFP, Dk Nathalie MacDermott wa Chuo cha King jijini London alisema inaonekana kuna uwezekano mkubwa virusi hivyo vinasambazwa na kwa matone yanayoingiwa hewani baada ya mtu kukohoa au kupumua.
Jumanne, madaktari katika Chuo Kikuu cha Hong Kong walichapisha andiko la awali likionyesha kusambaa kwa virusi hivyo, likisema kuwa kuna watu 1,343 wanaohisiwa kuwa na virusi hivyo jijini Wuhan -- sawa na makisio ya wiki iliyopita ya watu 1,700 yaliyofanywa na wataalamu wa Chuo cha Imperial cha London.
Taarifa hizo mbili ni kubwa kuliko taarifa rasmi.
Mlipuko huo umekuja wakati China ikijiandaa kwa sherehe za mwaka mpya maarufu kama Lunar New Year Holiday, ambazo huhudhuriwa na mamilioni ya watu wanaosafiri sehemu mbalimbali kuona familia.
Profesa Antoine Flahault, mkurugenzi wa Taasisi ya Afya ya Dunia katika Chuo Kikuu cha Geneva aliiambia AFP kwamba kutokana na ukweli kwamba virusi havionekani kuwa hatari kwa watu wengi, kimsingi hilo linatakiwa litie hofu zaidi kwa kuwa hali hiyo huwezesha watu kusafiri umbali mrefu kabla ya kubainika kuwa na virusi.
“Wuhan ni sehemu kubwa ya makutano na kwa kuwa usafiri ndio kitu kikubwa kinachofanyika wakati wa kuelekea mwaka mpya wa China, wasiwasi unatakiwa kuendelea kuwa mkubwa,” alisema Dr Jeremy Farrar, mkurugenzi wa taasisi ya Wellcome.

Wednesday, January 22, 2020

Jafo kumkabidhi Magufuli majina ya wakurugenzi wavivu



Dodoma. Waziri wa nchi Tamisemi, Seleman Jafo amesema ana majina ya wakurugenzi wasiokwenda na kasi ya utendaji kazi wa Serikali ya Tanzania, atayakabidhi kwa Rais John Magufuli Aprili, 2020.
Jafo ameeleza hayo leo Jumatano Januari 22, 2020 mjini Dodoma wakati akikabidhi mashine 7227 za kukusanyia mapato kwa halmashauri zote.
Mashine hizo zimetolewa  na balozi wa Norway nchini Tanzania,  Elisabeth Jacobsen.
Waziri huyo amesema ameshindwa kuzivumilia baadhi ya halmashauri  kwa kuwa zinatekeleza majukumu yake kinyume na miongozo ya Serikali, ikiwa ni pamoja na kutokusanya fedha ipasavyo.
"Wiki ijayo nitatoa taarifa ya makusanyo yote kwa halmashauri, lakini taarifa yangu ya mwezi Aprili  nitaorodhesha majina na kumkabidhi mwenye mamlaka, nitatoa mapendekezo ikibidi wakurugenzi waachiwe maana hawatufai," amesema Jafo.
Amebainisha kuwa kuna halmashauri zinadaiwa madeni makubwa, zikiwemo posho za madiwani, “kuna halmashauri inadaiwa Sh758 bilioni ambazo ni malimbikizo ya posho za wabunge, mkurugenzi wake anapaswa kujitathimi.”