Wednesday, June 12, 2019

Uchaguzi Serikali za mitaa nchini Tanzania kugharimu Sh82 bilioni

Uchaguzi ,Serikali  mitaa ,Uchaguzi Mkuu, Serikali Tanzania, Mwananchi Habari, Bunge Bajeti, Bunge Dodoma, Upinzani Tanzania, Chama Tawala CCM,

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika Oktoba, 2019 utagharimu Sh82.9 bilioni huku ikivitoa hofu vyama vya upinzani kuwa utakuwa huru na wa haki.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatano Juni 12, 2019 bungeni jijini Dodoma na naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Mwita Waitara wakati akijibu swali la mbunge wa Mtambile (CUF), Masoud Abdallah Salim aliyetaka kujua kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo.
Katika majibu yake Waitara amesema Serikali imekamilisha maandalizi ya kanuni za uchaguzi zitakazotumika kuendesha uchaguzi huo na kutangaza katika gazeti la Serikali (GN) la Aprili 26, 2019
“Serikali imehakiki maeneo ya utawala na kufanya mafunzo na mikutano kwa wadau wa uchaguzi huo. Pia Serikali inaendelea na maandalizi ya ununuzi wa vifaa vya uchaguzi na imetenga Sh82.9 bilioni kwa ajili ya kuendesha uchaguzi huo,” amesema Waitara.
Katika swali  lake la nyongeza Salim alitaka kujua kauli ya Serikali kuelekea uchaguzi huo kutokana na yaliyojitokeza katika chaguzi zilizopita ambako wagombea wa upinzani walizuiwa kugombea kwa madai kuwa hawana sifa.
Mbunge huyo amesema mkoani Morogoro CCM wameanza kampeni ya Morogoro ya kijani na kufananisha jambo hilo na kuanza kampeni mapema.

Akijibu swali hilo Mwita amesema, “Uchaguzi utakuwa huru na haki na majina ya wapiga kura yatabandikwa vituoni. Nadhani wapinzani mna hofu kwa kuwa mnajua CCM ipo katika nafasi nzuri ya kushinda kutokana na mambo mazuri yanayofanywa na Rais John Magufuli.”
Kuhusu kampeni za Morogoro ya kijani, Waitara amesema huo ni makakati wa chama hicho kupata taarifa za wanachama wake na kwamba hata Chadema nao wana mikutano ya Chadema ni Msingi kwa ajili ya kukutana wanachama wao.
Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji  naye aliuliza swali la nyongeza akibainisha kuwa CCM ina mbinu nyingi katika uchaguzi na kuhoji kama moja ya mbinu hizo ni wakurugenzi  kutokuwepo ofisini wakati wagombea wa upinzani wakirudisha fomu.
“Mbinu za CCM ni ushindi safi sidhani kama wakurugenzi wanakimbia na ninajua kuwa wagombea wa CCM walikuwa na sifa na kimsingi hakuna mtu aliyekwenda mahakamani na kusema wakurugenzi walikimbia,” amesema Waitara.

Tuesday, April 30, 2019

Magufuli ataja mambo matano yanayomfanya asinenepe



Rais wa Tanzania, John Magufuli ameyataja majukumu mazito anayoyafanya ikiwamo mambo makubwa matano aliyosema yanamfanya asinenepe.
Amesema wananchi wanapaswa kutambua Serikali iliyopo madarakani hailali usiku na mchana inafanya kazi kwa faida yao na waangalie walipotoka, walipo na wanapoenda.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 30 katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela mkoani Mbeya akiwa katiak ziara yake ya siku nane inayoendelea mkoani humo.
“Unafanya hiki unamaliza unaingia kingine, haiwezekani ukavifanya vyote unatengeneza barabara yenye gharama ya Sh60 bilioni barabara unamaliza, huku umeme kila mahali unaweka, elimu bure, huku unaajiri madaktari, walimu kule unajenga vituo vya afya, ndiyo maana nashindwa hata kunenepa,” amesema.
Amesema mwanzoni wa mwezi huu akiwa katika ziara yake mkoani Ruvuma alizindua vituo vya afya 352.
“Vituo vya afya Tanzania nzima vimekamilika havikujengwa na hewa ni fedha za walipa kodi mkiwamo ninyi, fedha hazikutolewa na wafadhili wowote, tungewapelekea wasingetoa tumejenga kwa gharama zetu. Umeme kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100. Fedha hizo zimepatikana baada ya kuwabana mafisadi na wala rushwa.”
“Tumewabana mafisadi ndiyo maana tumepata tusingefanya hivyo tusingefanikiwa. Tumeamua kupambana na wala rushwa na hiyo ni kazi ngumu kwa kuwa hawana alama katika uso, unaweza kukuta mwana CCM kumbe ni fisadi Chadema kumbe fisadi kwelikweli,” amesema.
Rais Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano imeongeza fedha za dawa kutoka Sh31 bilioni mpaka Sh270 bilioni kwa ajili ya kununua dawa, elimu bure kila mwezi Sh23.86 bilioni zinatolewa. Tunafanya haya kuhakikisha kila mwenye haki anapata haki yake, tumenunua ndege nane kwa mpigo tena mpya watu walipiga vita mno, mara kwa nini hatukopi, unayo fedha keshI unakopa ya nini?” amehoji.
Rais Magufuli amesema Tanzaniakwa sasa inapanua viwanja 11 vya ndege. “Tunataka maparachichi yabebwe moja kwa moja hadi kwenye masoko, unamkuta mtu mmoja amelewa tikiti maji anaongea vitu havieleweki.”
“Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kiwango kikubwa mno haya yote shetani hajalala wapo watakaotamka ambayo hata hayatakiwi, wapo watakaoona wivu kwa nini yanatokea,” amesema.

Saturday, April 27, 2019

JPM awapa eneo machinga Mbeya Uwanja wa ndege wa Mbeya



Mbeya/Dar. Rais John Magufuli amebadili matumizi ya eneo la uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya na kulifanya kuwa la wamachinga kufanyia shughuli zao.
Amesema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao ndogo kufanya biashara zao katikati ya mji, huku akiagiza mikoa yote kutenga maeneo kwa ajili yao.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana mjini Mbeya wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano inayoendelea mkoani humo.
Alisema kuanzia sasa eneo hilo litengenezewe miundombinu ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao katika mazingira mazuri ikiwemo vyoo, kituo cha mabasi na litakalobaki lijengwe kituo cha uuzaji madini.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kupokea maombi ya viongozi wa mkoa huo wakitaka kutengwa eneo maalumu kwa wamachinga ambao wanafikia 350,000 ili wafanye biashara zao kwa utaratibu mzuri tofauti na sasa wanavyojipanga kila mahali.

“Hili eneo nimelitoa bure, nendeni mkafanye biashara, lakini haina maana yale maeneo mengine mliyokuwa mnakaa msiende, endeleeni na shughuli zenu kote, wamachinga ndio walionipa kura na niliahidi kuwatetea, nitawatetea wafanye biashara zao,” alisema.

Thursday, March 28, 2019

Ndege ya Serikali mbioni kubeba abiria, yapakwa rangi kwa Sh5milioni



Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema ndege ya Serikali aliyoagiza ipelekwe Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kuanza kusafirisha abiria inakamilisha upakaji rangi kwa Sh5 milioni tofauti na Sh260 milioni zilizotajwa na wataalamu.
Rais Magufuli amesema wataalamu walishauri ndege hiyo ikapakwe rangi, kuandika maneno, na kuchorwa Twiga nje ya nchi wakati jambo hilo linawezekana kufanyika nchini.
Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam leo Machi 28, 2019  baada ya kupokea taarifa ya Takukuru na kumuapisha Balozi wa Cuba, Valentino Mlowola, Rais Magufuli amesema bado suala la rushwa ni tatizo.
 “Nchi hii ni hatari, kuna wajuaji wengi katika nchi hii, kuna maajabu mengi yanafanyika katika nchi hii,” amesema Rais Magufuli.
Akitoa mfano wa ndege, Rais Magufuli amesema aliposema ndege ya hiyo ipelekwe ATCL kuanza kusafirisha abiria, wataalamu walipokea na suala likawa kubadilisha maneno na twiga.
Amesema walimwambia kuwa suala hilo haliwezi kufanyika nchini na kutafutwa nchi tatu ambako, ndege hiyo ingeenda kupakwa rangi.

Wednesday, March 13, 2019

Bajeti ya 2019/20 kuongezeka Sh600 bil



Dodoma. Serikali imepanga kuongeza bajeti yake kwa Sh600 bilioni tu kwa mwaka wa fedha 2019/2020.
Bajeti ya mwaka unaoishia Juni 30 ilikuwa Sh32.5 trilioni, lakini ya mwaka ujao imepanga kufikia Sh33.1 trilioni.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango alitoa takwimu hizo wakati akiwasilisha kwa wabunge Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti kwa mwaka 2019/2020.
Lakini kati ya fedha hizo, Serikali inatarajia kukusanya Sh23 trilionikutoka katika mapato ya ndani yakijumuisha halmashauri, wakati nakisi itajazwa na fedha nyingine zitakazotokana na wafadhili, mikopo nafuu na ya masharti.
Hii ni mara ya nne kwa Serikali ya Awamu ya Tano kusoma ukomo wa bajeti yake. Katika makadirio yake ya mwaka 2016/17 ilipanga bajeti ya Sh29.5 trilioni, ikiwa ni ongezeko la zaidi ya Sh7 trilioni ya bajeti iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Nne.
Kwa mikakati ya 2019/20, mapato ya Serikali yanatarajiwa kuwa Sh22.2 trilioni na kati ya hizo zinazotokana na kodi ni Sh19.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi ni Sh3.1 trilioni, wakati mapato ya halmashauri yanatarajiwa kuwa Sh765.4 bilioni.
Mikopo ya ndani inakadiriwa kuwa Sh4.9 trilioni na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara inakadiriwa kuwa Sh2.3 trilioni na misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ni Sh2.7trilioni.
Dk Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh20.8 trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, ambayo yatajumuisha gharama za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwishoni mwa mwaka na maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.
Kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, mishahara itakuwa Sh7.5 trilioni huku matumizi mengineyo ya uendeshaji yakipangiwa Sh3.57 trilioni.
Alisema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh12.24 trilioni na kati ya hizo Sh9.73 trilioni ni fedha za ndani na Sh2.51 trilioni ni fedha za nje.
Dk Mpango alisema hadi kufikia Januari, washirika wa maendeleo walikuwa wametoa Sh144 bilioni kati ya Sh2.13 trilioni zilizoahidiwa katika bajeti ya mwaka 2018/19.
Dk Mpango alisema fedha hizo ni kati ya Sh12 trilioni ambazo zilitengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh9.87 trilioni zikiwa ni fedha za ndani na Sh2.13 trilioni ni fedha za nje.
“Sh144 bilioni zilipokelewa kutoka kwa washirika wa maendeleo na kupelekwa moja kwa moja kwenye miradi ya maendeleo inayotekelezwa na wizara, taasisi na wakala wa serikali, sektarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa,” alisema Dk Mpango.
Alisema Sh3.8 trilioni zimetumika kulipa mikopo iliyotumika kutekelezea miradi mbalimbali ya maendeleo.
Fedha za miradi ya maendeleo
Dk Mpango alisema wanatarajia kutoa Sh1.43 trilioni kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo, kama wa kufua umeme kwa kutumia nguvu ya maji katika Mto Rufiji (MW2,115), maarufu kwa jina la Stigler’s Gorge.
Dk Mpango alisema katika kipindi cha kati ya Julai 2018 na Januari, Serikali ilitoa ridhaa ya matumizi ya Sh13.7 trilioni na kati hizo, Sh10.96 trilioni zilikuwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh 2.78 trilioni kwa ajili ya maendeleo.
“Mahitaji yaliyopewa kipaumbe katika utoaji wa fedha ni pamoja na ulipaji wa deni la Serikali, ikijumuisha Sh5.46 trilioni za michango ya mwajiri katika mifuko ya hifadhi ya jamii, huku Sh3.8 trilioni zikitumika kulipa mikopo iliyotumika kutekeleza miradi ya maendeleo,” alisema Mpango.
Alisema Sh3.8 trilioni zilitumika kulipa mishahara ya watumishi wa umma.
Utekelezaji wa miradi
Akizungumzia utekelezaji wa miradi, Dk Mpango alisema kukosekana kwa umeme wa uhakika katika baadhi ya viwanda kumesababisha hasara na kushindwa kupanua uwekezaji.
Alisema changamoto nyingine ni baadhi ya makandarasi kuwa na uwezo mdogo wa kukamilisha kazi ipasavyo, mawasiliano hafifu baina ya wadau wa miradi hususani watekelezaji, waratibu na wasimamizi.
Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kutopatikana kwa fedha kwa wakati, hali ambayo imeathiri utekelezaji wa miradi kulingana na ratiba na kuongeza gharama. Alisema uchakavu wa miundombinu na mitambo katika miradi kulisababisha uzalishaji kuwa chini ya kiwango kinachotakiwa.


Tuesday, March 12, 2019

Serikali ya Tanzania yaanika mwelekeo wa bajeti yake 2019/2020



Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema katika mwaka wa fedha 2019/2020 inatarajia kukusanya na kutumia Sh33.1 trilioni.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango akiwasilisha Mapendekezo ya Serikali ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na ukomo wa bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 leo Jumanne Machi 2019 amesema mapato ya ndani yakijumuisha yanayotokana na  halmashauri nchini yanatarajiwa kuwa Sh23 trilioni.
Dk Mpango amesema Serikali kuu itakusanya Sh22.2 trilioni, kati ya hayo yanayotokana na kodi (TRA) ni Sh 19.1 trilioni na mapato yasiyo ya kodi ni Sh 3.1trilioni.
Amesema mapato yanayotokana na halmashauri katika mwaka huu yatakuwa ni Sh 765.4bilioni.
Waziri huyo amesema mikopo ya ndani na nje itakuwa Sh 7.27 trilioni ambapo kati ya hiyo Sh 4.96 trilioni ni mikopo ya ndani na mikopo ya nje yenye masharti ya kibiashara inakadiriwa kuwa Sh 2.31trilioni.
Kwa upande wa misaada na mikopo yenye masharti nafuu kutoka kwa washirika wa maendeleo ni Sh 2.7trilioni.
Dk Mpango alisema kati ya fedha hizo Sh 20.8trilioni zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida, matumizi yatajumuisha gharama za uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka 2019 na maandalizi ya uchaguzi mkuu utakaofanyika mwaka 2020.
Amesema kati ya fedha hizo za matumizi ya kawaida, mishahara itakuwa 7.5trilioni huku matumizi mengineyo (OC) yakiwa ni Sh 3.57 trilioni.
Amesema matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa Sh 12.24 trilioni ambapo Sh 9.73 trilioni ni fedha za ndani na Sh 2.51trilioni ni fedha za nje.

Thursday, February 21, 2019

CCM yataja mtaji wa kura za 2020



Bukoba. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema CCM lazima ijiridhishe ina nusu ya kura au zaidi kuelekea uchaguzi mkuu na itapatikana kwa kunadi mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.
Amekariri kauli yake kuhusu ugumu waliopata wa kunadi ilani ya CCM mwaka 2015, kuwa hawako tayari kuingia mwaka 2020 na viongozi wabovu na baadaye wahangaishwe na mtu wanayemjua.
Akifungua kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Kagera leo Februari 21, 2019 mjini Bukoba, Waziri Mkuu amesema nusu hiyo ya kura itapatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema Serikali imejikita kwenye maeneo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja na kuwa ni wajibu wa viongozi kufuatilia utekelezaji umefanyika kwa kiwango gani katika maeneo yao.
"Leo tuna miaka mitatu, chama lazima kijiridhishe angalau tuna nusu ya kura tunazozihitaji au zaidi, tumejikita kwenye maeneo muhimu ambayo yanagusa wananchi moja kwa moja," amesema Majaliwa.
Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutoa taarifa kwenye vikao vya chama kwamba wajumbe wanataka kujua utekelezaji wa mambo yanayotekelezwa katika maeneo yao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amepewa jukumu la kulea mikoa ya Kigoma na Kagera kichama ametaka uwe mwisho wa misuguano iliyokuwa inaendelea kwenye chama hicho.
Amewataka kujipanga kwa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na kufanya tathmini ya maeneo waliyopoteza na kuandaa wagombea watakaoweza kukomboa maeneo waliyopoteza katika uchaguzi uliotangulia.
Kuhusu zao la kahawa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema msimu wa mwaka jana ulikuwa na lawama na kutaka changamoto zilizojitokeza zifanyiwe kazi kabla ya msimu mpya kuanza na mfumo uangaliwe kuanzia kwa mkulima hadi kwenye soko.