Friday, September 13, 2019

Rais Magufuli kufungua mkutano wa wakuu wa polisi Afrika mashariki



Rais wa Tanzania, John Magufuli


 Rais wa Tanzania, John Magufuli anatarajiwa kufungua mkutano mkuu wa 21 wa shirikisho la wakuu wa polisi wa nchi za  Afrika Mashariki Septemba 19, 2019 jijini Arusha.
Mkutano huo utashirikisha wajumbe ambao ni ma Inspekta Jenerali wa Polisi kutoka nchi 14 za  Burundi, Comorro,Djibout , Congo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Shelisheli, Sudan Kusini, Sudan, Uganda na mwenyeji Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha nchini Tanzania leo Ijumaa, Septemba 13,2019, Msemaji wa Jeshi la Polisi la Tanzania, David Misime amesema maandalizi yote ya mkutano yamekamilika na wanaanza kupokea wageni  kuanzia leo.
Misime amesema kabla ya ufunguzi wa mkutano huo kutakuwa na vikao vya wakuu wa vitengo vya Interpol utakaofanyika kati ya Septemba 15 hadi  17,2019 kisha kufuatiwa na mkutano wa wakurugenzi wa upelelezi wa makosa ya jinai (DCI) na kikao cha wajumbe wa kamati ndogo ya mafunzo.
 Amesema kutakuwa na kikao cha kamati ndogo ya wataalamu wa sheria, vikao vya wajumbe wa kamati ya dawati la maswala ya unyanyasaji wa kijinsia pamoja na kikao cha  wajumbe wa masuala ya kukabiliana na ugaidi nchini.
Misime amesema mkutano huo utakaokuwa na kauli mbiu ya "Kuimarisha ushirikiano na ubunifu katika kupambana na uhalifu unaovuka mipaka"  ukiwa na  lengo la kuongeza ushirikiano katika kukabiliana na makosa yanayovuka mipaka na kuweka mikakati ya pamoja katika maazimio ya kukabiliana na uhalifu wa kuvuka mipaka.
“Katika mkutano huu, Inspekta Jenerali wa Polisi wa Tanzania  Simon Sirro atakabidhiwa uenyekiti wa shirikisho la wakuu wa polisi wa nchi za Afrika Mashariki,” amesema Misime.
Amesema katika mkutano huo, watatenga siku moja ya kuwapeleka wageni hao katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi Moshi (CCP) mkoani Kilimanjaro kuangalia madarasa na mabweni mapya yaliyojengwa na Serikali na wadau ili kuleta wanafunzi wao wa polisi kujifunza.

UDSM wamuomba Magufuli kuingilia kati vurugu Afrika kusini


Dar es Salaam. Serikali ya Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Daruso) nchini Tanzania kimelaani vikali mashambulio ya kibaguzi yaliyotokea nchini Afrika Kusini kwa watu wa mataifa mengine ya Afrika  huku wakimtaka Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc) kuingilia kati mzozo huo.

Taarifa iliyotolewa jana Alhamisi Septemba 12,2019 na Waziri wa Habari, Mawasiliano wa Daruso, Judith Mariki iliwaomba viongozi wa Afrika kukutana na kutumia maarifa na busara ili kudhibiti vitendo hivyo ambavyo ni kinyume cha maadili, mila na ubinadamu.
“Tunatoa wito kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Sadc, kuitisha mkutano wa dharura ili ujadili na viongozi wenzake kujadili mwafaka wa hali hiyo, ili kuwaleta pamoja kwa amani, kabla hali haijawa mbaya zaidi isipodhibitika,” alisema Mariki.
Alisema matukio hayo ya kinyama yanaharibu umoja na mshikamano wa Kiafrika kwa kuwa Waafrika wamekuwa wakiishi kama ndugu na kwa amani tangu wakati wa mapambano ya uhuru.
“Tusiruhusu mgawanyiko kutokana na tofauti zetu kwa sababu tunatokea nyumba moja kwa nini tugombee kipande cha mkate? Tunatoka bara moja kwa nini tuwadhalilishe ndugu zetu? Waafrika ni ndugu, ni walinzi wa ndugu zetu, mwafrika hawezi kuwa mgeni kwenye ardhi ya Afrika. Acha ubaguzi Afrika,” alisema Mariki.
Aliongeza, “Afrika ni kwa ajili ya Waafrika, tuache kuuana wenyewe kwa wenyewe kwa sababu tokea Afrika, umoja hautashindwa. Mungu ibariki Afrika, Mungu wabariki Waafrika.”

Thursday, September 12, 2019

Rais Magufuli afanya uteuzi, mkurugenzi mkuu usalama wa taifa

Rais wa Tanzania, John Magufuli,Dk Modestus Kipilimba,Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kuchukua nafasi ya Dk Modestus Kipilimba

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua na kumuapisha Diwani Athuman kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Usalama wa Taifa kuchukua nafasi ya Dk Modestus Kipilimba.
Taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Septemba 12, 2019 na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa inaeleza kuwa uteuzi wake umeanza leo.
Kabla ya uteuzi huo,  Diwani aliyeapishwa Ikulu, Dar es Salaam leo alikuwa mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Akizungumza baada ya kumuapisha, Rais Magufuli amemtaka kuchapa  kazi kwa juhudi na maarifa na kuweka mbele maslahi ya Taifa.

Wednesday, September 11, 2019

Rais Magufuri afanya uteuzi bodi ya LATRA,TFRA


Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amemteua Dk John Ndunguru kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA).

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Septemba 11, 2019 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imemnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi ikisema uteuzi wa Dk Ndunguru umeanza Septemba 9, 2019.
Pia, taarifa hiyo imesema Rais Magufuli amemteua Profesa Antony Mshandete kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA).
Profesa Mshandete ni Naibu Makamu Mkuu wa Chuo (Taaluma, utafiti, ubunifu), Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) kilichopo mkoani Arusha.
Imesema uteuzi huo umeanza Septemba 9, 2019.

Aliyekuwa Waziri wa uchukuzi awamu ya nne afariki dunia

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Bodi ya kampuni ya simu za mkononi ya Airtel Tanzania, Dk Omary Nundu (71) amefariki dunia.

Taarifa iliyotolewa leo mchana Jumatano Septemba 11, 2019 na Kitengo cha Mawasiliano cha Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) Dar es Salaam kimesema, “Waziri wa zamani Omary Nundu alifikishwa leo MNH, akitokea nyumbani kwa gari binafsi la wagonjwa akiwa tayari ameshafariki.”
“Hivyo waliomleta waliamua wakahifadhi mwili wake katika hospitali ya rufaa ya Jeshi Lugalo,” imeeleza taarifa hiyo
Dk Nundu enzi za uhai wake aliwahi kuwa mbunge wa Tanga na Waziri wa Uchukuzi katika Serikali ya awamu ya nne  ya Tanzania.
Juni 12, 2019, Rais wa Tanzania, John Magufuli alimteua Dk Nundu kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania ikiwa ni utekelezaji wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na kampuni ya Bharti Airtel International.
Katika makubaliano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania pamoja na ofisa mkuu wa ufundi wanapaswa kuteuliwa na Serikali.
Kabla ya Dk Nundu aliyezaliwa Agosti 6 mwaka 1948 kuteuliwa alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL)

Tuesday, September 10, 2019

Nape amuomba msamaha Rais Magufuli



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema amemsamehe mbunge wa Mtama (CCM),  Nape Nnauye huku akielezea namna ambavyo mbunge huyo amekuwa akimuomba radhi.
Akizungumza Ikulu leo Jumanne Septemba 10, 2019 Rais Magufuli amesema kwa muda mrefu Nape amekuwa akimuomba msamaha kupitia ujumbe mfupi wa simu ya mkononi na kuwatumia baadhi ya wazee wa chama hicho tawala.
Rais Magufuli amesema Nape alifikia hatua ya kwenda kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula, mjane wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere pamoja na Mkurugenzi Mkuu mstaafu  wa Idara ya  usalama  wa Taifa nchini Tanzania, Apson Mwang'onda
“Alienda kwa mzee Mangula, amefika mpaka kwa Mzee Apson, Mama Nyerere amehangaika kweli lakini baadaye ni katika hiyohiyo sisi tumeumbwa kusamehe.”
“Leo nimemuona asubuhi amekuja hapa baadaye nikaona siwezi nikamzuia, ngoja niache shughuli zangu nimuone nilikuwa na kikao kingine kikubwa anachozungumza ninaomba baba unisamehe,” amesema Magufuli.
Kiongozi mkuu huyo wa nchi amesema, “Na mimi nimeshamsamehe tena kwa dhati kutoka moyoni mwangu, nimeshamsamehe na nimeshamsamehe kweli. Nape nenda ukafanye kazi, Mungu akujalie.”
 “Unamuona kabisa huyu mtu anaomba msamaha na leo kaniomba aje anione na saa nyingine  wasaidizi wangu wamekuwa wakipata hizo habari,” amesema Rais Magufuli
Awali, akizungumza Nape aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM amesema, “nimekuja kumuona (Magufuli) kama baba yangu, lakini mwenyekiti wa chama changu, Rais wangu kwa sababu wote mnajua mambo yaliyopita yalitokea ni mengi hapa katikati na mimi kama mtoto wa CCM mwanaye niliona ni vizuri nije niongee na baba yangu.”
“Kwa hiyo baada ya kupata fursa nimekuja nimemuona na mle ambamo nilimkosea kama baba yangu nimeongea naye na baba amenielewa, ameniambia amenisamehe na amenipa ushauri ambao nitaufanyia kazi na naamini baada ya hapa mambo yatakwenda vizuri.”
Mbunge huyo amesema, “kwa kweli kwa dhati ya moyo wangu nimshukuru sana sana, amenipa fursa kubwa, ndefu na ameongea maneno mengi kwangu na ushauri wake nimeuchukua.”
Ingawa si Nape wala Rais Magufuli waliozungumza hasa kwa nini wamekutana lakini katika siku za hivi karibuni kuliibuka sauti za viongozi mbalimbali wakiwamo za wabunge wa CCM, January Makamba (Bumbuli) na Willium Ngeleja (Sengerema) wakizungumzia suala la waraka ulioandika na makatibu wakuu wa CCM waliopita, Yusuf Makamba na  Abdurahman Kinana.
Wazee hao wa CCM waliandika  waraka huo kulalamikia mambo mbalimbali kwenda kwa Katibu wa Baraza la ushauri wa viongozi wa CCM, Pius Msekwa wakizungumzia mmoja wa   wanaharakati  ambaye amekuwa akiwachafua bila hatua kuchukuliwa.
Mpaka sasa bado haijafahamika kama hatua zimechukuliwa na hivi karibuni, Rais Magufuli alisema January na Ngeleja walikwenda kumwomba radhi kuhusu sauti hizo alizodai kuwa ni za kwao.
Nape ni miongoni mwa wanaotajwa kuhusika katika sauti hizo.

Monday, September 9, 2019

Mahakama yakataa maombi ya Lissu kupinga kuvuliwa ubunge

Mahakama Kuu,Tundu Lissu,mbunge wa Singida Mashariki, mwananchi habari,

Mawakili wa upande wa Tundu lissu
Dar es Salaam. Mahakama Kuu imekataa maombi ya aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu kufungua shauri la maombi ya kutengua uamuzi wa Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai uliosababisha ubunge wake kukoma.
Imesema mwanasheria mkuu huyo wa Chadema hakupaswa kuwasilisha maombi hayo, alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi wa ubunge katika jimbo hilo.
Akisoma uamuzi huo wa mahakama leo Jumatatu Septemba 9, 2019 Jaji Sirillius Matupa amesema kama maombi yake yakikubaliwa yatasababisha uvunjaji wa katiba kwa kuwa italazimika kuwa na wabunge wawili kwenye jimbo moja.
Lissu alifungua maombi chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute  Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kumwakilisha, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Lissu aliomba kibali cha kufungua shauri kupinga taarifa ya Spika ya kukoma kwa ubunge wake na mahakama iteunge taarifa hiyo.Lissu yuko nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu ambao hadi sasa hawajajulikana, tangu Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa, katika makazi yake, jijini Dodoma akitokea bungeni.
Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika wa Bunge Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu, huku alijitetea kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba ya Nchi.
Alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Wednesday, September 4, 2019

Air Tanzania yaachiwa huru

Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg ,ndege ya Tanzania,mwananchi habari,


Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg nchini Afrika Kusini imeiruhusu ndege ya Tanzania iliyokuwa imezuiwa katika uwanja wa ndege wa Oliver Tambo nchini humo kuondoka.
Ndege hiyo aina ya Airbus A220-300 ilizuiwa katika uwanja huo Agosti 23, 2019 kwa amri ya mahakama hiyo baada ya Hermanus Steyn kufungua kesi katika mahakama hiyo akidai fidia ya dola 33 milioni.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumatano Septemba 4,2019 kutoka Afrika Kusini, Naibu Waziri Mambo ya Nje ya Tanzania, Dk Damas Ndumbaro amesema Serikali ya Tanzania imeshinda kesi hiyo bila kutoa fedha yoyote ambayo aliyetushitaki alitaka Serikali ya Tanzania tuweke fedha kama dhamana dola milioni 33.
“Tumeshinda na ndege imeruhusu kuondoka. Kwa sasa hakuna kesi yoyote.”
“Sisi tulivyokuwa tunatukanwa kwenye mitandao tulikuwa tunaangalia tu, tulikuwa tunajua kazi tunayoifanya. Lazima ujue huku zimekuja PhD tatu,” amesema Dk Ndumbaro kutoka Afrika Kusini leo Jumatano.
Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania, Dk Hassan Abbas kupitia akaunti yake ya twitter ameandika, “Mahakama Kuu ya Gauteng, Afrika Kusini, leo imetoa hukumu na kuamuru kuwa ndege ya @AirTanzania iliyokuwa ikishikiliwa nchini humo iachiwe na mlalamikaji alipe gharama za kesi. Tunawashukuru wote kwa uvumilivu wenu.”

Monday, September 2, 2019

Rais Magufuli azungumza na watendaji wa kata nchi nzima

Rais  wa Tanzania, John Magufuli,kikao cha watendaji wa kata, mwananchi habari, habari mwananchi,

Dar es Salaam. Rais  wa Tanzania, John Magufuli amewataka watendaji  wa kata nchini kutoa taarifa kuhusu wakurugenzi, mawaziri  na wakuu wa mikoa wanaofanya matendo yanayokiuka misingi ya utawala bora.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Septemba 2, 2019 Ikulu jijini Dar es Salaam alipokutana na watendaji hao kutoka mikoa yote nchini.
Amebainisha kuwa mtendaji wa kata ndio bosi wa  eneo  lake, “Hata kama kuna kiongozi wa nafasi gani yuko chini yako na anapoonekana kuenenda visivyo unapaswa kumwajibisha au kutoa taarifa kwa mamlaka yake.”
“Katika kata kuna mkurugenzi wa halmashauri, RC (mkuu wa Mkoa), waziri au nani, wewe (mtendaji kata) ndio msimamizi, kama wewe upo katika kata na ambayo kuna waziri, RC, mkurugenzi  sijui  nani wewe ndiyo msimamizi,” amesema Magufuli.
Ameongeza, “Usiogope kumlima (barua) na kumwandikia maoni, hata kama anakuzidi cheo kwamba katika kata hii namwona mtumishi huyu anakwenda kinyume na maadili. Na ukimwona ni mkubwa sana, piga nakala hapa kwangu, lazima watu tujifunze kuogopana.”
Huku akizungumza zaidi kwa mifano amesema, “Kila siku anapigana (kiongozi) baa katika kata yako kwa sababu ni mkubwa unaacha kumripoti, chalaza kalamu na ndio maana watendaji kata wana kalamu na saini zao.”
Huku akiwataka kutokubali kudharaulika katika maeneo yao, Magufuli amesema, “Hapa (Ikulu) ni kwenu na mimi ni mpangaji tu hapa na mnaoamua nani aende Ikulu ni nyinyi na wananchi.”
“Hapa wamekaa hadi Wajerumani, amekaa  Nyerere (Julius) akaondoka, akaja Mwinyi (Ali Hassan) akaondoka, amekuja Mkapa (Benjamin) akaondoka, amekuja Kikwete (Jakaya)  akaondoka na mimi nitakaa na kuondoka,” amesema.
“Ndio maana sikusita kuwakaribisha , najua mko mahali pema salama na nilifikiri ni eneo hili tu tunaweza kukaa na kuzungumza vizuri. Nikija wilayani hawawasogezi karibu,” amesema.

Sunday, September 1, 2019

Mwendokasi lateketea lote kwa moto


Dar es Salaam. Basi la Kampuni ya Mwendo Haraka (Udart) maarufu 'Mwendokasi' lililokuwa likitoka Mjini kwenda Kimara Mwisho Dar es Salaam nchini Tanzania limeteketea lote kwa moto.


Tukio hilo limetokea leo usiku  wa Jumapili Septemba 1, 2019 eneo la Kimara Mwisho na kusababisha adha kwa watumiaji wa usafiri huo huku watu wengi wakijitokeza kushuhudia basi hilo ambalo limetekelea lote.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Teopista Malya amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema hakuna madhara kwa binadamu yaliyotokana na ajali hiyo.

Kamanda Malya amesema basi hilo lilitoka Mjini likiwa na abiria na lilipofika eneo la Kimara Mwisho walifanikiwa kushuka kabla halijateketea kwa moto.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na kukusanya taarifa zaidi za ajali hiyo, ikiwemo hasara iliyosababishwa na ajali hiyo