Thursday, February 21, 2019

CCM yataja mtaji wa kura za 2020



Bukoba. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema CCM lazima ijiridhishe ina nusu ya kura au zaidi kuelekea uchaguzi mkuu na itapatikana kwa kunadi mafanikio ya Serikali ya awamu ya tano.
Amekariri kauli yake kuhusu ugumu waliopata wa kunadi ilani ya CCM mwaka 2015, kuwa hawako tayari kuingia mwaka 2020 na viongozi wabovu na baadaye wahangaishwe na mtu wanayemjua.
Akifungua kikao cha halmashauri kuu ya CCM mkoa wa Kagera leo Februari 21, 2019 mjini Bukoba, Waziri Mkuu amesema nusu hiyo ya kura itapatikana kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Amesema Serikali imejikita kwenye maeneo muhimu yanayogusa wananchi moja kwa moja na kuwa ni wajibu wa viongozi kufuatilia utekelezaji umefanyika kwa kiwango gani katika maeneo yao.
"Leo tuna miaka mitatu, chama lazima kijiridhishe angalau tuna nusu ya kura tunazozihitaji au zaidi, tumejikita kwenye maeneo muhimu ambayo yanagusa wananchi moja kwa moja," amesema Majaliwa.
Pia amewataka wakurugenzi wa halmashauri kutoa taarifa kwenye vikao vya chama kwamba wajumbe wanataka kujua utekelezaji wa mambo yanayotekelezwa katika maeneo yao.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye amepewa jukumu la kulea mikoa ya Kigoma na Kagera kichama ametaka uwe mwisho wa misuguano iliyokuwa inaendelea kwenye chama hicho.
Amewataka kujipanga kwa uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa na kufanya tathmini ya maeneo waliyopoteza na kuandaa wagombea watakaoweza kukomboa maeneo waliyopoteza katika uchaguzi uliotangulia.
Kuhusu zao la kahawa, Waziri Mkuu Majaliwa amesema msimu wa mwaka jana ulikuwa na lawama na kutaka changamoto zilizojitokeza zifanyiwe kazi kabla ya msimu mpya kuanza na mfumo uangaliwe kuanzia kwa mkulima hadi kwenye soko.

Wednesday, February 20, 2019

Alichokisema Jenerali Ulimwengu kuhusu Magufuli

Muasisi wa Kampeni ya ChangeTanzania, Maria

Muasisi wa Kampeni ya ChangeTanzania, Maria Sarungi akibadilishana mawazo na Mwanahabari Mkongwe, Jenerali Ulimwengu (katikati) pamoja na Mchora Katuni, Masoud Ally wakati wa mjadala kuhusu haki na wajibu wa rai ulifanyika jijini Dar es Salaam jana. 
Dar es Salaam.  Mwandishi wa habari mkongwe nchini Tanzania, Jenerali Ulimwengu amempongeza Rais John Magufuli kwa hatua mbalimbali anazochukua za kuwaletea maendeleo wananchi.
Hata hivyo, amemshauri mkuu huyo wa nchi kuachia jukwaa la  wananchi kuhoji na kutoa mawazo mbadala juu ya uwajibikaji na utekelezaji wa masuala yanayohusu maendeleo yao.
Ametoa kauli hiyo leo Jumatano Februari 20, 2019 katika kongamano la ‘Wenye Nchi ni Wananchi’ lililoandaliwa na Jukwaa la Tanzania yenye Mabadiliko.
 “Huwa sipendi sana kumsifu (Rais Magufuli) lakini kuna mambo mengi sana ambayo amefanya kwa uthubutu, wakati mwingine anakosea lakini anathubutu angalau, anachohitaji ni kusikiliza zaidi watu wanamwambia nini pale ambapo tunadhani amekosea,” amesema.
“Watu wanayo nia njema ya kumsaidia Rais lakini wakati mwingine anaonekana kama hasikilizi sawasawa, lakini angalau kwa uthubutu anao.”