Wednesday, August 14, 2019

Facebook kuja na lugha za kiasili Tanzania



Dar es Salaam. Pengine siku moja tutashuhudia mtandao wa Facebook ukiwa katika lugha ya Kisukuma, Kinyanyusa au lugha yoyote ya asili, binafsi sipati picha itakuwa vipi huko mtandano, ila lugha ya kwanza kuingizwa wenyewe watatamba sana.
Uwezekano wa hilo kutokea unatokana na nia ya mtandao wa Facebook ambao una watumiaji hai zaidi ya bilioni 2.3 duniani kote kueleza nia yake ya kuendelea  kuongeza lugha za asili za Kiafrika katika mtandao huo.
Jumatano Agosti 14,2019 mtandao huo ulisema lugha kadhaa za asili zitaongezwa katika mpango wake wa kutathimini uhakika wa maudhui ‘Third-Party Fact-Checking programme’ ili kusaidia watumiaji kupata taarifa kwa usahihi kupitia mtandao huo na kuzuia usambazaji wa taarifa potofu.
Mpango huo tayari unahusisha lugha za Kiyoruba, Kiigbo na Kihausa kwa upande wa Nigeria, Kiswahili, Kesnya, Kiwolof Senegali na lugha za asili sita za Afrika Kusini kikiwemo Kizulu na Kisetswana.
Mkuu wa sera za facebook Afrika, Kojo Boakye alisema mtandao huo unaendelea kuwekeza katika jitihada za kuzuia usambazaji wa taarifa za uongo kupitia jukwaa la mtandao huo lakini pia kujenga jamii ya pamoja iliyo salama na yenye taarifa.
“Kwa kuongeza wigo wa lugha za asili kutaongeza ubora wa taarifa zinazoonwa na watu katika mtandao wetu, tunafahamu bado tuna mengi ya kufanya na tuko tayari kufanya,” alisema Boakye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Africa Check, Noko Makgato alisema mpango huo kwao ni jambo jema kwakuwa wamepanua ghala la lugha. “Kwenye nchi za kiisimu kama Nigeria, Kenya, Afrika Kusini na Senegali kuangalia usahihi wa maudhui ni jambo muhimu,” anasema Makgato.

Aliyeua wauza madini naye ahukumiwa kunyongwa hadi kufa

Image result for mahakama ya rufaa


Dar es Salaam. Mahakama ya Rufani imetupilia mbali maombi ya marejeo ya aliyekuwa Mkuu Upelelezi wa Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Dar es Salaam nchini Tanzania, Mrakibu wa Polisi (SP) Christopher Bageni aliyehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ambaye alikuwa akiomba Mahakama hiyo ibadilishe uamuzi wake.
Uamuzi wa kutupilia mbali maombi hayo ya Bageni ulioandaliwa na jopo la majaji watatu wa mahakama hiyo waliosikiliza maombi hayo, umetolewa leo Jumatano, Agosti 14, 2019 na Naibu Msajili Mwandamizi wa  Mahakama ya Rufani, Elizabeth Mkwizu.
Jopo la majaji hao waliosikiliza na kutoa uamuzi wa maombi hayo namba 63 ya mwaka 2016 ni Stella Mugasha (kiongozi), Ferdinarnd Wambali na Rehema Kerefu.
Kwa uamuzi huo ambao ndio wa mwisho, sasa Bageni hana namna nyingine ya kufanya kwani hakuna ngazi nyingine ya mahakama nchini wala hatua nyingine ambayo anaweza kuichukua kuupinga.
Badala yake sasa atasubiri tu utekelezaji wake huku akiombea neema ya rais wa awamu ya sasa au awamu zijazo kumsamehe ama kumwachia huru au kumbadilishia adhabu pengine kuwa ya kifungo kwa mamlaka yake kikatiba kama ataguswa au kuona kuna sababu ya kufanya hivyo.
Ofisa huyo wa zamani wa Polisi alihukumiwa na mahakama hiyo adhabu hiyo Septemba 11, 2016, baada ya kupatikana na hatia ya mauaji ya wafanyabiashara watatu wa madini kutoka Mahenge, Morogoro na dereva teksi wa Manzese Dar es Salaam.
Alitiwa hatiani na mahakama hiyo kufuatia rufaa aliyoikata Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), akipinga hukumu ya Mahakama Kuu iliyomwachia huru yeye na maofisa wenzake wengine wa polisi katika kesi ya msingi.
Lakini siku chache baadaye, alifungua maombi hayo akiiomba mahakama hiyo ifanye marejeo ya hukumu yake hiyo kisha imuondolee hatia na kumfutia adhabu hiyo na iamuru aachiwe huru, akidai kuwa hiyo iliyomtia hatia ina kasoro za dhahiri.
Siku ya usikilizwaji wa maombi hayo, wakili wake Gaudiosus Ishengoma alidai mahakama hiyo ilimtia hatiani bila kumpa fursa ya kumsikiliza kwani ilimtia hatiani kwa ushahidi ambao haupo kwenye kumbukumbu za mahakama na wala haukujadiliwa kwenye rufaa ya DPP.
Hata hivyo, Mahakama hiyo katika uamuzi wake wa leo Jumatano, imetupilia mbali sababu hizo ikisema kwamba hazina msingi kwa kuwa hoja zake hazina msingi kwa kuwa hakuna jambo jipya ambalo Mahakama ililiibua na kwamba hakunyimwa haki ya kusikilizwa kwa kuwa alikuwa na wakili wakati wa rufaa hiyo.
Mkwizu alisema kuwa Mahakama hiyo ilitekeleza majukumu yake na kwamba katika kumtia hatiani ilifanya tu uchambuzi wa ushahidi uliowasilishwa mahakamani ukiwemo wa aliyekuwa mshtakiwa mwenza, aliyeeleza ukweli wa tukio na Bageni hakuupinga.
“Mwombaji ameshindwa kuonesha makosa kwenye hukumu hii (iliyomtia hatiani), kama alivyodai kwenye sababu zake za maombi. Kwa hiyo hatuna namna nyingine zaidi ya kuyatupilia mbali maombi haya, kwani.”, alisema Mkwizu.
Katika kesi ya msingi, Bageni na wenzake 13, walikuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji ya wafanyabiashara hao Sabinus Chigumbi (Jongo) na ndugu yake Ephrahim Chigumbi na mwenzao Mathias Lunkombe pamoja na Juma Ndugu, dereva teksi aliyekuwa akiwaendesha,
Walikuwa wakidaiwa kuwaua kwa kupigwa risasi katika msitu wa Pande wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Januari 14, 2008.
Kabla ya kuuawa, walitiwa mbaroni na askari hao eneo la Sinza Palestina nyumbani kwa mchimbaji mwenzao, ambao waliwafunga pingu wakiwatuhumu kuhisika katika uporaji wa pesa za kampuni ya Bidco na baadaye polisi walidai kuwa walifariki wakati wakirushiana nao risasi.
Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa Agosti 17, 2009 na aliyekuwa Jaji Kiongozi Salum Massati, aliyeisikiliza, ingawa alikiri kuwa kwa mujibu ushahidi uliowasilishwa mahakamani, Bageni alikuwepo ndiye aliyeongoza msafara wa washtakiwa kwenda eneo la mauaji, lakini iliwaachia huru wote.
Jaji Massati alisema kuwa kwa mujibu wa ushahidi uliotolewa mahakamani hapo, mauaji hayo yalitekelezwa na Koplo Saad Alawi, ambaye hakuwa miongoni mwa washtakiwa (hadi sasa hajulikani aliko) na kwamba hakuna ushahidi kwamba Bageni aliamuru au alisaidia au aliwezesha mauaji hayo.
Lakini baada ya DPP kukata rufaa, Mahakama ya Rufani katika hukumu iliyotolewa na jopo la majaji watatu Bernard Luanda (kiongozi wa jopo), Sauda Mjasiri na Semistocles Kaijage ilimtia hatiani Bageni na kumhukumu adhabu hiyo.

Ajari ya moto Morogoro vifo vyaongezeka

Image result for ajali morogoro


Dar es Salaam. Majeruhi 6 kati ya 38 wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili wamefariki dunia na kufanya idadi ya waliofariki hadi sasa kufikia 82
Majeruhi hao ni wa ajali ya moto iliyotokea Morogoro baada ya lori la mafuta kupinduka na kuwaka Moto.
Akitoa taarifa hiyo leo Agosti 14, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano (MNH), Aminiel Aligaesha amesema kwa sasa wamebaki majeruhi 32.
Kati ya majeruhi hao 17 wapo katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) huku wengine 15 wakiendelea kupatiwa matibabu katika wodi ya Sewahaji.
Mkuu huyo wa mawasiliano amesisitiza watu kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa kuwa bado kuna uhitaji mkubwa.
“Wapo wanakuja na kutuletea vijana wa kuchangia damu, niwashukuru kwa hilo na niwasisitize wengine waendelee kuja, damu inahitajika sana,”amesema Aminiel

Akizungumza katika eneo la kuchangia damu msanii Ahmed Olotu maarufu kama Mzee Chilo amesema ameguswa na tukio hilo na ndiyo sababu iliyomfanya kuhamasisha vijana kuchangia damu.
“Nimepatwa na uchungu mno lakini kwa kuwa umri wangu hauruhusu kuchangia damu, nimeona niwahamasishe vijana ninaofanya nao kazi waje kujitolea damu tuokoe maisha ya wengine,” amesema Mzee Chilo

Tuesday, August 13, 2019

Neema kwa wakulima wa mbogamboga nchini Tanzania



Arusha. Wakulima wa mbogamboga na maua nchini Tanzania waliokuwa wakipata hasara kutokana na  kushindwa kuhifadhi kwa muda mrefu mazao yao sasa wataanzania kuwa na nyuso za furaha.
Ni kutokana na tume ya nguvu za Atomic kuja na mradi wa kiwanda cha mionzi ya kuhifadhi maua na mbogamboga.
Kiwanda hicho kinatarajiwa kugharimu Sh4 bilioni na kitajengwa mkoani Arusha ambako kuna uzalishaji mkubwa wa maua na mbogamboga
Mtafiti mwandamizi wa tume hiyo, Yesaya Sungita akizungumza na Mwananchi amesema mradi wa kiwanda hicho tayari umeandikwa na kufikishwa serikalini.
“Tunatarajia mradi huu ukipitishwa na Serikali na kupatikana fedha, kitajengwa viwanda mkoani Arusha na kingine jijini Dar es Salaam,” amesema
Amebainisha kuwa kama mradi huo ukipitishwa na kupatikana fedha ndani ya miaka minne , kiwanda cha kwanza kinaweza kuwa kimekamilika na kusaidia sekta ya maua na mbogamboga.

"Afrika Kusini, Nigeria  na Misri wana viwanda vya aina hii na vimekuwa na faida kubwa kwa wakulima wa mbogamboga na maua,” amesema.
Wakizungumza mradi huo, baadhi ya wakulima wa maua na mbogamboga, wameshukuru tume hiyo kwa kuja na mradi huo utakaosaidia kuwapunguzia hasara.
Jane Minja, mkulima wa mbogamboga eneo la Tengeru wilayani Arumeru, amesema kwa muda mrefu wamekuwa wakipata hasara ya mboga kuharibika kabla ya kusafirishwa.
“Mbogamboga na maua vina soko zaidi nje ya nchi sasa kama huwezi kuhifadhi kabla ya kusafirisha utapata hasara,” amesema.
Naye Peter Pendaeli amesema hulazimika kusafirisha maua nchini Nairobi ili kupata ndege zinazokwenda moja kwa moja barani Ulaya, kwamba ujio wa viwanda hivyo ni nafuu kwao

Basi lapata ajari mkoani Kilimanjaro abiria wanusurika



Hai. Watu zaidi ya 40 wamenusurika kifo baada ya basi la kampuni ya Kaprikon walilokuwa wanasafiria kutoka Singida kwenda Moshi mkoani Kilimanjaro  nchini Tanzania kupata ajali na kupinduka eneo la KIA wilaya ya Hai Mkoa wa Kilimanjaro.
Akizungumza na Mwananchi, George Benedict Mberessero ambaye ni mmiliki  wa mabasi hayo amesema ajali hiyo imetokea leo Jumanne Agosti 13,2019.
Amesema ajali hiyo imetokea saa 10  jioni baada ya basi hilo kulipisha gari lililobeba  fedha ambalo lililokuwa likitoka jijini Dar es Salaam kwenda mkoani Arusha.
"Ni kweli gari limepata ajali maeneo ya KIA likitokea mkoani Singida kuja Moshi na kwamba chanzo cha kupinduka kwa basi hilo inatokana na kupisha gari... lililobeba fedha ndipo lilipoanguka,” amesema Mberessero
"Hakuna madhara yoyote  yaliyojitokeza kwani basi lilikuwa kwenye mwendo wa taratibu," amesema
Jitihada za kumpata Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro zinaendelea

Mahakama Kuu Tanzania yamuita Tundu Lissu

Image result for tundu lissu


Dar es Salaam. Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa hati ya wito wa kufika mahakamani kwa mbunge wa zamani Singida Mashariki, Tundu Lissu kwa ajili ya shauri la maombi yake kuanza kutajwa.
Wito huo kwa Lissu umetolewa leo Jumanne, Agosti 13, 2019 na kusainiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Lssu amefungua maombi mahakamani hapo chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo.
Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Tanzania, kupinga kuvuliwa ubunge wake.
Shauri hilo ambalo litasikilizwa na Jaji Sirillius Matupa limepangwa kutajwa keshokutwa Alhamisi, Agosti 15, 2019.
Katika hati hiyo ya wito wa kufika mahakamani, Mahakama hiyo imemtaka kufika mahakamani tarehe hiyo bila kukosa na pia awasilishe vielelezo vyote ambavyo anakusudia kuvitumia, katika kesi hiyo.

Mwanasheria huyo Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), yuko nchini Ubelgiji kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana.
Lissu ambaye pia alikuwa Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni amekuwa nje ya nchi kwa matibabu baada ya kunusurika katika jaribio hilo la mauaji kwa takribani miaka miwili, tangu  Septemba 7, 2017, aliposhambuliwa.
Uamuzi wa kumvua ubunge ulitangazwa na Spika wa Bunge, Job Ndugai Juni 28, 2019 wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge huku akitaja sababu mbili.
Spika Ndugai alizitaja sababu hizo ni kushindwa kuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na sababu ya pili ikiwa ni kutokuja taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Lissu alifungua shauri la maombi  Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala Kuu, Dar es Salaam, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), akiomba kibali cha kufungua shauri la kupinga uamuzi huo.
Kwa mujibu wa hati ya shauri hilo la maombi namba 18 la mwaka 2019, Lissu anaiomba mahakama hiyo, impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo itoe amri ya kumtaka Spika Ndugai ampe (Lissu) taarifa yake ya kumvua ubunge.
Pia, anaiomba mahakama hiyo impe kibali cha kufungua kesi ili mahakama hiyo iite taarifa ya uamuzi wa Spika wa kumvua ubunge na kisha itengue na kutupilia mbali uamuzi huo wa Spika Ndugai kumvua ubunge.
Vilevile  Lissu anaomba Mahakama hiyo impe kibali afungue shauri ili mahakama itoe amri ya kusimamisha kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu wa Chama cha Mapinduzi (CCM).

PROFESA KABUDI; Zimbabwe kuondolewa vikwazo vya kiuchumi

Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri SADC, Profesa

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amekabidhiwa rasmi  uenyekiti wa baraza la mawaziri la Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kugusia nchi ya Zimbabwe kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.

Makabidhiano hayo yamefanyika leo Agosti 13, 2019 mbele ya Sekretarieti ya SADC, na Profesa Kabudi kuchukua nafasi iliyokuwa ikishikiliwa na naibu waziri mkuu na waziri wa mambo ya nje wa Namibia,  Netumbo Nandi-Ndaitwah.
"Katika kipindi chetu tutahakikisha jumuiya ya kimataifa kuondoa vikwazo vya kiuchumi Zimbabwe. Lazima viondolewe  kwa kuwa kiongozi aliyekuwepo ameshaondoka madarakani na wananchi wanaendelea vizuri kwa sasa,” amesema Profesa Kabudi.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa, Profesa Kabudi amesema  Tanzania katika kipindi hicho cha mwaka mmoja wa uongozi wake, itatekeleza kauli mbiu ya maendeleo shirikishi ya viwanda, kuongeza ajira pamoja na kusimamia kwa weledi masuala ya watoto, wanawake na afya.
"Tutazingatia suala la maendeleo endelevu na kuhakikisha tunaongeza viwanda, ajira pia asilimia 60 ya raia katika nchi 16 za SADC ni vijana hivyo lazima kuhakikisha tunaendeleza ajira," amesema.
Profesa Kabudi amesema suala muhimu kwa sasa ni kuhakikisha Kiswahili kinakuwa lugha rasmi ya SADC kwa kukuza lugha hiyo ambayo kwa sasa ni ya Tisa duniani.