Monday, September 21, 2020

Magufuli awapa maagizo mawaziri

 




RAIS John Magufuli ametoa maagizo kwa mawaziri watatu akitaka yatekelezwe haraka ili Wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma itoe huduma kwa ufanisi na kutatua kero za wananchi.

Mawaziri hao ni Seleman Jafo (Ofisi ya Rais – Tamisemi), Dk. Medard Kalemani (Nishati) na Inocent Bashungwa (Wizara ya Viwanda na Biashara).

Katika maagizo hayo, mawaziri hao wametakiwa kutekeleza kila mmoja kulingana na wigo wa wizara yake, huku wakiagizwa kuharakisha utekelezaji huo.

Rais Magufuli alitoa maagizo hayo jana akiwa njiani kuelekea mkoani Tabora akitokea Kigoma ambapo alisimama katika maeneo mbalimbali yakiwemo Kazuramimba, Uvinza, Mpeta, Nguruka, Kaliua na kuzungumza na wananchi.

Miongoni mwa changamoto kubwa katika maeneo hayo ni ubovu wa barabara, ukosefu wa umeme katika baadhi ya vijiji, maji na uendelezaji wa kiwanda cha chumvi cha Uvinza.

Akizungumza na wananchi katika kampeni za Uchaguzi Mkuu zinazoendelea, Rais Magufuli alisema hajaridhika na kasi ya usambazaji umeme katika wilaya hiyo na kuahidi kuwa vijiji 61 ambavyo bado havijapata umeme vitapelekewa.

“Naseme kwa uwazi kwamba suala la umeme katika vijiji na wilaya ya Uvinza hatujafanya vizuri sana, nitawabana watu wangu na waziri wangu wa umeme kama anasikia aanze kutekeleza kwa sababu bado ni waziri.

“Mheshimiwa Waziri Ndalichako (Elimu, Sayansi na Teknolojia) nataka ukamweleze Waziri Kalemani (Nishati) kwenye suala la umeme Uvinza sijafurahia, lakini nawaambia hivi vijiji 61 nitalibeba.

“Hatuwezi tukapeleka kwa miaka mitano vijiji 17 tu, tulitakiwa tuwe tumepeleka kwenye vijiji 61 vibaki 17 tu, hii ni kero lazima nibebe mimi mwenyewe,” alisema Rais Magufuli.

Kwenye miundombinu alisema barabara ya Uvinza – Malagarasi kilomita 150 itatengenezwa kwa kiwango cha lami na kwamba mwezi ujao zabuni itatangazwa.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli zaidi ya Sh bilioni 51 ambazo zinatarajiwa kutatumika katika ujenzi huo zimetolewa na Quwait Fund na Opec Fund.

Pia alisema katika barabara ya Uvinza – Mjini ambayo awali ilipangwa kutengenezwa kilimota moja, aliagiza ziongezwe kilometa nyingine 9 na kumtaka Waziri wa Nchi (Ofisi ya Rais – Tamisemi), Seleman Jafo kutafuta Sh bilioni 5 za ujenzi huo.

“Nataka siku moja nikija kuweka jiwe la msingi niikute lami mpaka Uvinza, natoa maagizo Jafo uwaletee bilioni tano kuanzia Jumatatu ziwe zimeshafika Uvinza,” alisema Rais Magufuli wakati akizungumza kwa njia ya simu na Jafo.

Aidha alimuagiza Waziri Bashungwa (Viwanda na Biashara) kufuatilia kiwanda cha chumvi ili kiweze kuendelezwa kuongeza fursa za ajira kwa vijana.

“Tuna kiwanda cha chumvi kikubwa sana tunataka tuki – promote kiwe kinauza mpaka Burundi, DRC na kwingine na vijana wetu wapate ajira, kwa hiyo, Waziri wa Viwanda naye hili akalibebe,” alisema.