
Maelefu ya wajumbe wa CCM wanakutana hii leo jijini Dodoma katika mkutano mkuu.
Pamoja na mambo mengine, wajumbe wa mkutano huo watamchagua ni mgombea urais yupi atakae peperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktaba mwaka huu.
Jina la rais John Magufuli ndilo litakalopitishwa baada ya Halmashauri Kuu Taifa kumpendekeza bila kupingwa hapo jana.
Humphrey Polepole Katibu mwenezi wa CCM
Humphrey Polepole ambae ni Katibu mwenezi wa CCM amesema mkutano huo pia umehudhuriwa na wageni mbalimbali kutoka mataifa mengine ikiwemo viongozi wa vyama vya Ukombozi kutoka mataifa ya Afrika.
Dr Hussein Mwinyi tayari ametangazwa kuwa mgombea urais kupitia CCM Kwa upande wa Zanzibar.
Wawakilishi mbalimbali wahudhuria mkutano mkuu wa CCM
Baadhi ya nchi ambazo zimetuma wawakilishi wake katika mkutano wa leo ni pamoja na Vietnam, msumbuji, DRC, Burundi na Sudan Kusini.
Magufuli apitishwa kuwania awamu ya pili
Rais Magufuli wa Tanzania
Kikao cha siku ya Ijumaa kilimpitisha kwa pamoja rais John Pombe Magufuli kuwania awamu ya pili ya urais wa Tanzania.
Magufuli hakuwa na mpinzani katika mchakato huo kwa kuwa hakukuwa na mwanachama mwingine wa CCM aliyejitokeza kugombea nafasi hiyo.
"Niwaombe wote tukashirikiane kutafute ushindi...wakati mwengine kunakuwa na hali ya kujiamini. Tukijiamini hatutashiriki ipasavyo, tukafanye kazi kwa nguvu ili tukapate ushindi wa kishindo," alisema Magufuli baada ya kupitishwa.
Kama ilivyo kwa jina la Mwinyi, jina la Magufuli linapelekwa kwenye Mkutano Mkuu wa CCM Taifa ili lithibitishwe rasmi.
Bado haijabainika upinzani utamchagua nani kupambana na Magufuli katika kinyang anyiro cha uchaguzi wa rais.
Ingawa Magufuli anasifiwa kwa kuanzisha miradi kadhaa, wakosoaji wake ikiwemo makundi ya haki za binadamu wanasemma ametumia nafasi yake kukandamiza upinzani na uhuru wa habari.