Tuesday, April 30, 2019

Magufuli ataja mambo matano yanayomfanya asinenepe



Rais wa Tanzania, John Magufuli ameyataja majukumu mazito anayoyafanya ikiwamo mambo makubwa matano aliyosema yanamfanya asinenepe.
Amesema wananchi wanapaswa kutambua Serikali iliyopo madarakani hailali usiku na mchana inafanya kazi kwa faida yao na waangalie walipotoka, walipo na wanapoenda.
Rais Magufuli ameyasema hayo leo Jumanne Aprili 30 katika viwanja vya Mwakangale wilayani Kyela mkoani Mbeya akiwa katiak ziara yake ya siku nane inayoendelea mkoani humo.
“Unafanya hiki unamaliza unaingia kingine, haiwezekani ukavifanya vyote unatengeneza barabara yenye gharama ya Sh60 bilioni barabara unamaliza, huku umeme kila mahali unaweka, elimu bure, huku unaajiri madaktari, walimu kule unajenga vituo vya afya, ndiyo maana nashindwa hata kunenepa,” amesema.
Amesema mwanzoni wa mwezi huu akiwa katika ziara yake mkoani Ruvuma alizindua vituo vya afya 352.
“Vituo vya afya Tanzania nzima vimekamilika havikujengwa na hewa ni fedha za walipa kodi mkiwamo ninyi, fedha hazikutolewa na wafadhili wowote, tungewapelekea wasingetoa tumejenga kwa gharama zetu. Umeme kwa fedha za Watanzania kwa asilimia 100. Fedha hizo zimepatikana baada ya kuwabana mafisadi na wala rushwa.”
“Tumewabana mafisadi ndiyo maana tumepata tusingefanya hivyo tusingefanikiwa. Tumeamua kupambana na wala rushwa na hiyo ni kazi ngumu kwa kuwa hawana alama katika uso, unaweza kukuta mwana CCM kumbe ni fisadi Chadema kumbe fisadi kwelikweli,” amesema.
Rais Magufuli amesema Serikali ya awamu ya tano imeongeza fedha za dawa kutoka Sh31 bilioni mpaka Sh270 bilioni kwa ajili ya kununua dawa, elimu bure kila mwezi Sh23.86 bilioni zinatolewa. Tunafanya haya kuhakikisha kila mwenye haki anapata haki yake, tumenunua ndege nane kwa mpigo tena mpya watu walipiga vita mno, mara kwa nini hatukopi, unayo fedha keshI unakopa ya nini?” amehoji.
Rais Magufuli amesema Tanzaniakwa sasa inapanua viwanja 11 vya ndege. “Tunataka maparachichi yabebwe moja kwa moja hadi kwenye masoko, unamkuta mtu mmoja amelewa tikiti maji anaongea vitu havieleweki.”
“Tanzania ni miongoni mwa nchi tano barani Afrika ambazo uchumi wake unakua kwa kiwango kikubwa mno haya yote shetani hajalala wapo watakaotamka ambayo hata hayatakiwi, wapo watakaoona wivu kwa nini yanatokea,” amesema.

Saturday, April 27, 2019

JPM awapa eneo machinga Mbeya Uwanja wa ndege wa Mbeya



Mbeya/Dar. Rais John Magufuli amebadili matumizi ya eneo la uwanja wa ndege wa zamani wa Mbeya na kulifanya kuwa la wamachinga kufanyia shughuli zao.
Amesema amechukua uamuzi huo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao ndogo kufanya biashara zao katikati ya mji, huku akiagiza mikoa yote kutenga maeneo kwa ajili yao.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo jana mjini Mbeya wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tano inayoendelea mkoani humo.
Alisema kuanzia sasa eneo hilo litengenezewe miundombinu ya kuwawezesha wafanyabiashara hao kuendesha shughuli zao katika mazingira mazuri ikiwemo vyoo, kituo cha mabasi na litakalobaki lijengwe kituo cha uuzaji madini.
Rais alitoa agizo hilo baada ya kupokea maombi ya viongozi wa mkoa huo wakitaka kutengwa eneo maalumu kwa wamachinga ambao wanafikia 350,000 ili wafanye biashara zao kwa utaratibu mzuri tofauti na sasa wanavyojipanga kila mahali.

“Hili eneo nimelitoa bure, nendeni mkafanye biashara, lakini haina maana yale maeneo mengine mliyokuwa mnakaa msiende, endeleeni na shughuli zenu kote, wamachinga ndio walionipa kura na niliahidi kuwatetea, nitawatetea wafanye biashara zao,” alisema.