Tuesday, November 20, 2018

Magufuli aahirisha sherehe za Desemba 9



Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameahirisha maadhimisho ya sherehe za uhuru zinazofanyika Desemba 9 kila mwaka na kuagiza fedha zilizotengwa zielekezwe kujenga hospitali jijini Dodoma itakayoitwa Hospitali ya Uhuru.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne, Novemba 20, 2018 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, imesema Rais Magufuli ameagiza Sh995.182 milioni zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo.
Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi leo Jumanne pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.
Amesema hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino  kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa  mkoani humo.
Kadhalika, waziri mkuu amesema Rais Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya kuandaa matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya Siku ya Uhuru.
“Wanaweza kutumia siku hiyo kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali,” amesema Majaliwa
Kutokana  na maagizo hayo, Majaliwa amewataka wananchi katika maeneo yote nchini kujiandaa kufanya shughuli za kijamii zitakazopangwa na wakuu wao wa mikoa na wilaya.
Hii ni mara ya pili kwa Dk Magufuli kuahirisha sherehe za uhuru. Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 2015 alipoagiza fedha zilizotengwa zitumike kupanua kipande cha barabara kutoka Morocco hadi makutano ya Mwenge jijini Dar es Salaam.

Rais Magufuli achangia milioni 50 matibabu ya Ruge Mutahaba



Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametoa dola za Marekani 20,000  ambazo ni wastani wa Sh50 milioni  ili kuchangia matibabu ya Mkurugenzi wa vipindi wa Clouds Media group, Ruge Mutahaba.
Ruge ambaye alianza kusumbuliwa na ugonjwa ambao bado haujawekwa wazi tangu  mwanzoni mwa mwaka huu anapatiwa matibabu Afrika Kusini.
Akizungumza leo katika kipindi cha  Clouds 360 kinachorushwa na televisheni ya Clouds, Mkuu wa Vipindi wa redio hiyo, mmoja wa wafanyakazi wa kampuni hiyo, Sebastian Maganga amesema hatua hiyo ya Rais imefikiwa baada ya kusikia Ruge anaumwa kwa muda na zilimsikitisha.
“Aliamua kumshika mkono kama baba afanyavyo kwa mwana wa kumzaa, kumshirikisha katika maombi na alinyoosha mkono kwetu akituambia changamoto za kiafya ni kubwa na la awali ambalo anataka kulifanya ni kuchangia mfuko wa kiafya na changamoto zisiwe gharama za kimatibabu,” amesema Maganga akinukuu maneno ya Rais Magufuli.
Mbali na Rais kutoa mchango wa matibabu pia Maganga amebainisha kuwa wameamua kuweka wazi juu ya afya ya Ruge kutokana na kuwepo kwa maneno mengi katika mitandao ya kijamii.
“Yalizungumzwa mengi na sisi tuliona wakati haukuwa mzuri sana kuzungumza na tuliona tukifanya yoyote tutaleta maswali mengi ambayo hata yeye hakupenda,”
"Katikati ya Mei kulelekea Juni hali ya Mkurugenzi haikuwa nzuri akatuomba kupata muda kidogo ili ashughulikie afya yake tuliona hili litakuwa dogo tu na tukatoa baraka zote,”
“Lakini ripoti za kitabibu zikasema muda wa kupumzika ni mdogo hivyo akaongezewa muda na katikati ya Juni na Julai alirejea na kasi ya kawaida kwenye kazi na wiki mbili tatu tukawa naye na hapo ndiyo tulikuwa tunakaribia kuanza Tigo Fiesta Moro,”
“Akatuambia anabidi aelekee kwenye taratibu za kimatibabu na nikiri bado changamoto hizo zipo na madaktari wanakiri Kiongozi wetu ni mpambanaji na bado anahitaji muda wa kupumzika na ni kweli hizo changamoto zilikuwepo" amesema Maganga na kuongeza kuwa
“Tunashukuru mara nyingi ukipata changamoto A ya kiafya changamoto B inajitokeza na tunashukuru taratibu hali yake inarudi na kuna hatua kubwa ya kimaendeleo." 

Monday, November 19, 2018

Jinsi Mbunge CUF alivyobadili gia angani


Dar es Salaam. Nani anahama na nani anabaki, lilikuwa swali lililogonga vichwa vya wengi Alhamisi iliyopita ya Novemba 15 ambayo kwa mujibu wa CCM, ilikuwa siku ya mwisho kwa wabunge na madiwani kutoka upinzani kupokelewa ndani ya chama hicho na kupewa nafasi ya kugombea tena.
Joto lilipanda na kuwavuruga wabunge hasa baada ya mbunge wa Temeke (CUF), Abdallah Mtolea kutangaza ndani ya Bunge kuwa anajiuzulu ubunge na kuomba chama kinachotaka kufanya kazi na yeye kujitokeza.
Kuondoka kwa Mtolea ambaye jioni ya siku hiyo alihamia CCM na kufanya idadi ya wabunge wa upinzani waliojiunga na chama hicho kufikia 10 inaweza kuwa haikushtua sana, badala yake Mbunge wa Tandahimba (CUF), Katani Katani ndiye aliyetawala mjadala bungeni na hasa kwenye mitandao ya kijamii.
Duru za siasa, zilidai kwa vile Katani alionekana katika viunga vya Bunge asubuhi akiwa na Mtolea, jambo hilo liliwahusisha wawili hao kujiuzulu na baadaye ikatajwa kuwa wabunge wawili, James Mbatia (Vunjo-NCCR-Mageuzi) na Selemani Bungara ‘Bwege’ (CUF) walimnasua Katani.
“Ni kweli Katani alikuwa miongoni mwa waliotakiwa kuhama siku hiyo (Alhamisi), lakini kuna wabunge wawili walizungumza naye sana na kumsihi asihame, alikuwa njiani kuhama kama alivyofanya Mtolea bungeni,” alisema mbunge mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Katani alipozungumza na Mwananchi alisema hana wazo la kuhamia CCM, “Na kama nikihama chama, siwezi kwenda CCM, hao walioandika kwamba naondoka walikuwa na hoja zao.”
Alipoulizwa taarifa za yeye kuwa karibu na Mtolea siku aliyotangaza kuhama, alisema, “Mimi na Mtolea ni zaidi ya marafiki, anapajua nyumbani, familia yangu, watoto na wazazi wangu, lakini hadi anaondoka sikuwa najua kitu.”
Katani akijibu swali kuhusu madai kuwa Mbatia na Bungara walichangia asihame siku hiyo alikanusha akidai hakuwa na mpango wa kuhama.
“Siyo kweli, wabunge wengi hawapafahamu kwangu na mimi siku hiyo nilipotoka bungeni nilikwenda nyumbani peke yangu na niliporudi nilimpitia Bwege tukaenda sote bungeni.”
“Mimi nina mtaji wa wananchi, niliwahi kuwaeleza wananchi wangu kuwa nikihama sitakwenda CCM, hata kama nikifukuzwa na (Profesa Ibrahim) Lipumba siwezi kwenda CCM,” alisema.
Alipoulizwa kama wanawasiliana na Mtolea tangu ahame, alisema; “Nawasiliana kwa simu, sijawahi kukutana naye, nikikutana naye na hali hii, wanaweza kusema vingine lakini mimi siwezi kuhama.”
Lakini, Bungara alisema alikuwa anahisi hilo kwa Katani baada ya Mtolea kuhama.
“Lakini Katani wakati wote alinieleza kwamba mimi (Katani) sina hizo na jioni nitakwenda kutoa kauli bungeni,” alisema.
Alipoulizwa mazungumzo hayo yalifanyikia wapi, Bungara alisema; “Tulikwenda kuyafanyia nyumbani kwake kuanzia saa 7 hadi 10 jioni tuliporudi bungeni.”
Alisema walipofika bungeni kabla ya kuingia ukumbini, waliwakuta wabunge wa Chadema wakizungumzia suala hilo la Katani kujiuzulu, na wao walipomuuliza Katani aliwajibu anakwenda kutoa kauli bungeni hivyo wakamsindikiza.
Mbatia ambaye imeelezwa alihusika kumshawishi Katani asihame, alipoulizwa kuhusiana na sakata hilo alisema ni kweli alizungumza na Katani kipindi ambacho tayari “nilikwishatoka Ikulu kuzungumza na Rais John Magufuli mbali na mengine nilimwambia ‘Hekima, umoja na amani inalisimamisha Taifa.”
“Taifa hili ni letu sote na Tanzania ikiharibika, sote tunaangamia,” alisema Mbatia ambaye ni mwenyekiti wa Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD) huku akiahidi wiki hii kuzungumzia undani wa mazungumzo yake na Rais Magufuli.
Kuhusu Katani, Mbatia alisema; “Ni kweli aliniambia anataka afanye uamuzi mgumu kwa sababu anaona kuna giza nene katika chama chake (CUF).”
“Baada ya kunieleza hayo nilimweleza mambo manne ambayo ni majukumu ya mbunge tuliyofundishwa na spika mstaafu Pius Msekwa yanayopaswa kuzingatia kabla ya kufanya uamuzi.
Mbatia aliyataja mambo hayo kuwa ni taifa lake, jimbo lake, chama chake na mwisho dhamira binafsi.
“Nilimweleza kama anataka kufanya uamuzi afuate haya na haya alitufundisha Mzee Msekwa,” alisema Mbatia
Alisema mbali na Mzee Msekwa, aliyekuwa mwanasiasa kongwe nchini, Marehemu Kingunge Ngombale- Mwiru aliyewahi kusema, “Kabla ya kufanya uamuzi weka mbele maslahi ya nchi.”
Alisema hakujua kama Katani alikuwa anataka kuhama au ni uamuzi gani, “Lakini mimi nilimweleza hayo mambo manne na tukaachana.”

Hakimu Luhwago alivyokutana na urais wa Majaji, Mahakimu njiani



Katika hali ya kawaida, uchaguzi wa kupata viongozi wa umoja ambao unajumuisha mahakimu na majaji, mtu mwenye wadhifa wa jaji angekubalika kirahisi na kushinda, lakini haikuwa hivyo kwa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT).
Hakimu ndiye aliyeshinda na kuwa kiongozi wa umoja huo na timu yake inayomjumuisha makamu wake, katibu, katibu msaidizi, mhazini na katibu mwenezi, ambao wataongoza kwa miaka mitatu ijayo.
Hiyo ni historia iliyowekwa kwa mara ya kwanza katika chama hicho tangu kilipoanzishwa mwaka 1984.
Msimamizi wa uchaguzi huo ambaye ni mkuu wa Taasisi ya Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Jaji Dk Paul Kihwelo alimtangaza Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Kishapu, Wilberforce Luhwago kuwa mshindi baada ya kuwabwaga wagombea wenzake wengine watatu, wakiwamo majaji wawili.
Hakimu Luhwago aliibuka na ushindi wa kishindo baada ya kupata kura 85 kati ya kura 147, akifuatiwa na Jaji Ilvin Mugeta aliyepata kura 41, wakati Jaji Sophia Wambura alipata kura 16 na Hakimu Mkazi Pascal Rwagesa akapata kura tano.
Kuokota embe chini ya mwarobaini
Jinsi Hakimu Luhwago alivyopata uongozi huo ni kama mtu aliyeokota embe chini ya mwarobaini, hakutumia nguvu wala kutokwa jasho jingi, kwani hakuwa amejiandaa wala kupanga kugombea nafasi hiyo. Mkutano huo wa uchaguzi ulifanyika Dodoma, ambako Hakimu Luhwago aliamua kusimama kwa muda kuhudhuria ndipo aendelee na safari ya kuelekea katika kituo chake cha kazi.
“Kwa kuwa kulikuwa na mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu jijini Dodoma, uliokuwa unaambatana na uchaguzi wa viongozi wakuu wa chama hicho, nikiwa mwanachama, niliamua kusimama hapo kushiriki kwanza mkutano huo ndipo niendelee na safari yangu,” alisema Hakimu Luhwago.
Anasema alipofika maeneo ya Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, alipata ajali baada ya gurudumu la gari lake kuchomoka. Licha ya gari kuharibika sana, alitoka salama na akafanya utaratibu kulivuta gari hilo hadi eneo la Mahakama Kuu.
Alisema baadaye alienda kulala na kupumzika siku iliyofuata kusubiri mkutano ambao ulikuwa Ijumaa.
“Nikiwa nimepumzika hotelini siku ya Alhamisi, nilifuatwa na watu wapatao 30 kunishauri nigombee,” anasema Hakimu Luhwago.
“Niliwauliza sababu za kufanya hivyo, wakanijibu kuwa chama kinaonekana kama kipo kwa jina tu, lakini hakionekani katika utekelezaji wa majukumu yake. Walisema wameona mimi ndio naweza kukifufua, kukipeleka na kurejeshea sifa yake kama chama cha kitaaluma.
“Hata hivyo, nikawaambia kuwa watangaza nia wameshatangaza karibu wiki mbili zilizopita. Mimi kuchukua fomu zikiwa zimebaki saa chache inanipa tabu kidogo.
Wakasema kwa kuwa katiba haijakataa tunachukua,” alisema.
Anasema alipotafakari maneno yao pamoja na malalamiko ya mahakimu, kama changamoto wanazokumbana nazo kwa mwajiri wao Tume ya Utumishi wa Mahakama, huku kukiwa hakuna wa kuwasemea, alikubali nao wakaenda kumchukulia fomu.
Luhwago anasema ili kuepuka fitina na mizengwe ya kiuchaguzi kama ambavyo huwa inatokea kwenye siasa, walikubaliana jina lake lisijulikane mapema bali iwe ni kushtukiza tu ili washindani wake wasipate muda wa kujiandaa.
Anasema wapigakura wengine walibaini katika hatua za mwisho kuwa anagombea baada ya msimamizi wa uchaguzi kutangaza majina ya wagombea.
Anasema baada ya taratibu zote za uchaguzi kukamilika, alitangazwa kuwa mshindi, akiwa amepata kura 85 na kuwazidi wagombea wote kwa pamoja kwa kura 23 na hivyo kuwa rais mpya wa chama hicho.
Ajenda ya utawala wa sheria
Pamoja na kutofanya kampeni, Hakimu Luhwago anasema anadhani kilichompa ushindi ni ajenda yake kuweka mbele utawala wa sheria.
“Ajenda yangu ilikuwa moja tu, utawala wa sheria. Utawala wa sheria ndani na nje ya mahakama. Ndani ya mahakama ni kwamba mwajiri anapowashughulikia watumishi wake anatakiwa awashughulikie kwa mujibu wa utawala wa sharia,” anasema.
“Sio kuna watu wa Escrow, anawafunika lakini wanaotumia mihuri vibaya anawashughulikia. Hilo likitokea ni lazima mahakama i-expect serious counter statement (itarajie tamko kali la kupinga) kutoka kwa rais wa JMAT.”
Katika kashfa ya akaunti ya escrow, iliyohusisha uchotwaji wa Sh306 bilioni kutoka akaunti ya pamoja ya kampuni binafsi ya IPTL na Tanesco, majaji walituhumiwa kuhusika na baadhi kutajwa kuwa walipata mgawo wa fedha, lakini muhimili huo haukutoa tamko la kulaani kitendo hicho.
Kwa mujibu wa mmoja wa wapigakura ambaye ni hakimu kutoka Mwanza, siri ya kumtaka Luhwago kuwania nafasi hiyo na kisha kumchagua ni misimamo yake katika kusimamia haki, sheria na taratibu.
“Kabla ya kumjua kwa sura Mheshimiwa Luhwago, nilikuwa namsikiasikia tu wakati akiwa hapo Mahakama ya Wilaya ya Ilala Dar es Salaam. Hivyo kitu kilichofanya watu wengi wamkubali ni kuwa huyu jamaa anafuata zaidi utaratibu na sio siasa,” anasema hakimu huyo bila kutaka jina lake litajwe. Hakimu huyo anasema kuwa yeye alifika Dodoma akiwa amepanga kumchagua mgombea mwingine ambaye ni jaji.
“Lakini tulivyokuwa tukitembea watu wakawa wanasema Jaji (anamtaja jina) kweli ni mzuri, lakini wale wameshakuwa watu wakubwa (hivyo) hawezi tena kuwakumbuka watu wa chini,” anasema hakimu huyo.
“Halafu wakasema hata huku chini pia tuchague mtu ambaye ana misimamo ambaye anaweza kutetea haki za wengine bila woga na ambaye anafuata utawala wa sheria. Mtu aliyetajwa wa kwanza ni Hakimu Luhwago.”
Anasema katika kumjadili Hakimu Luhwago ilielezwa kuwa kutokana na msimamo wake aliwahi kumwandikia Jaji Kiongozi wito wa kufika mahakamani aliyetaka kumpa maelekezo katika kesi moja, ili akaeleze mahakamani kama alikuwa analijua jambo hilo.
“Sasa hicho kitu kikawa-impress (wavutia) watu wengi kwamba huyu mtu inawezekana akatuvusha kwa sababu ana msimamo na ujasiri, mkweli na si mwoga, maana kuna changamoto ambazo zinataka mtu asiye mwoga, mkweli, anayeweza kusimamia jambo kwa haki na kwa data bila kutetereka.”
Kwa upande wake Hakimu Honorina Kambadu wa Kibaha anasema Hakimu Luhwago ni mkweli na muwazi, aliye tayari kutetea haki sawa kwa wote.
“Ni mtu anayeweza kupigania haki hata kwa mambo ambayo anaona ni changamoto katika kazi na maslahi kwa wote. “Hata katika uchaguzi huu alifanikiwa kupata kura nyingi kutokana na weledi wake, heshima na maadili aliyo nayo hasa katika kufanya kazi kwa kufuata utawala wa sheria. Hakika anastahili nafasi hiyo na ninaamini anaweza kuongoza vizuri.”

DC Jerry Muro ampongeza Magufuli kuwateua vijana

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha,Jerry

Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoa wa Arusha,Jerry Muro akizungumza wakati wa mkutano wa pili wa mwaka wa vijana katika nchi za Afrika Mashariki uliofanyika katika taasisi ya MS TCDC leo.
Arusha. Mkuu wa wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, Jerry Muro amesema Serikali ya Tanzania imepiga hatua katika kuwawezesha vijana kwa kuwapa nafasi mbalimbali za uongozi serikalini.
Muro amesema hayo leo Jumatatu Novemba 19, 2018 wakati akitoa salamu za Serikali kwenye mkutano wa pili wa mwaka wa vijana katika nchi za Afrika Mashariki unaofanyika katika kituo cha MS TCDC.
"Rais John Magufuli ameonyesha imani kubwa kwa kuwaamini vijana na amewateua kushika nyadhifa zikiwemo mawaziri, naibu mawaziri, wakuu wa mikoa na wilaya," amesema Muro.
Muro hata hivyo, amekemea tabia ya vijana kutumia teknolojia ya mawasiliano vibaya kwa kuweka picha zisizo na maadili badala ya kuchangamkia fursa hiyo kutangaza biashara na kazi za ubunifu.

Sunday, November 18, 2018

Majaliwa asema Rais hapendi watu walipe nauli kufuata huduma za afya



Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametembelea kituo cha afya cha Nkowe na kukagua ujenzi wa gereza la Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya askari magereza wa gereza hilo.
Waziri Mkuu ametembelea miradi hiyo leo Jumapili, Novemba 18, 2018 akiwa katika ziara yake ya kikazi Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi ambapo amewataka wananchi kulinda kituo hicho cha afya.
Amesema kwa sasa wananchi hao hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya kwani baadhi yake kama upasuaji, maabara, mama na mtoto zinapatikana katika kituo hicho.
“Rais John Magufuli anataka kila Mtanzania apate huduma za afya karibu na makazi yake ili asilipe nauli au kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya,” amesema Majaliwa.
Mganga Mfawidhi wa kituo hicho, Dk Paul Mbinga amesema kituo hicho kinahudumia  wakazi 5,264 wa Kata ya Nkowe, Chienjele, Nandagala, Likunja na Mnacho.
Dk Mbinga amesema mradi wa ujenzi wa kituo hicho cha afya uliogharimu Sh500 milioni, umepunguza gharama kama kwenda kutibiwa katika hospitali ya wilaya ambayo ipo umbali wa kilomita 20. “Mradi huu umeimarisha mifumo ya huduma kwa watoto, wazee, watu wenye ulemavu na vijana”.


Friday, November 16, 2018

Benki ya Dunia yaimwagia mabilioni Tanzania

Rais John Magufuli akiwa katika mazungumzo na

Rais John Magufuli akiwa katika mazungumzo na Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia kwa Kanda ya Afrika, Hafez Ghanem Ikulu jijini Dar es Salaam leo Ijumaa. 
Dar es Salaam. Benki ya Dunia (WB) imeridhia kuipatia Tanzania Dola za Marekani 300 milioni sawa na Sh680.5 bilioni kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kuongeza ubora wa elimu ya sekondari.
Mradi huo unakusudiwa kujenga vyumba vya madarasa, mabweni, maabara, nyumba za watumishi na kununua vifaa vya kufundishia. 
Taarifa iliyotumwa leo Ijumaa Novemba 16, 2018 na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu imesema Rais John Magufuli amekutana Ikulu jijini Dar es Salaam na  Makamu wa Rais wa WB Kanda ya Afrika, Dk Hafez Ghanem.
Katika mazungumzo yao, Rais Magufuli amesema pamoja na kuridhia kutoa fedha za mradi huo, Benki hiyo inaendelea kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo nchini Tanzania.
Amesema miradi hiyo yenye thamani ya Dola za Marekani 5.2 bilioni sawa na zaidi ya Sh13 trilioni inatekelezwa kutokana na uhusiano na ushirikiano mzuri baina yake  na Tanzania.
Dk Ghanem amesema katika mazungumzo hayo wamejadili juu ya maendeleo ya miradi hiyo na kazi nzuri ambayo inafanywa na Tanzania kuimarisha uchumi.
Aidha amempongeza Rais Magufuli kwa matokeo mazuri ya mapambano dhidi ya rushwa na kuimarisha huduma za kijamii.
Kwa upande wake, Rais Magufuli ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mzuri baina yake na Benki ya Dunia huku akiahidi Serikali itaendeleza na kukuza uhusiano huo.
Amesema Serikali itahakikisha fedha zote zinazotolewa kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinatumika kwa miradi iliyokusudiwa.
Namshukuru Dk Hafez Ghanem na Benki ya Dunia kwa kuendelea kutoa fedha kwa ajili ya miradi ya Tanzania, baadhi ya watu wasiotutakia mema walisema zimefyekelewa mbali,” amesema.
Rais Magufuli amesema benki hiyo pia imetoa fedha zinazofadhili miradi mbalimbali ya elimu, nishati, barabara, kilimo, afya na maji, ni miradi mikubwa na mingi.
“Kwa hiyo amekuja kututhibitishia kuwa Benki ya Dunia haitatuacha” amesema Rais Magufuli.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James ameitaja baadhi ya miradi inayoendelea kutekelezwa kwa ushirikiano na Benki ya Dunia kuwa ni mradi wa uboreshaji wa Bandari ya Dar es Salaam ambayo ujenzi wake umefikia asilimia 24, ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, mradi wa ujenzi wa miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (BRT) kwa awamu ya kwanza na ya pili na miradi mingine mbalimbali.